top-news-1350×250-leaderboard-1

Samia kuzuru makumbusho, kuunguruma bungeni Angola

Angola. Ikiwa leo ni siku ya pili ya ziara ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan nchini Angola yenye lengo la kukuza na kuimarisha zaidi uhusiano wa kihistoria baina ya nchi mbili hizi, asubuhi atatembelea makumbusho ya Antonio Agostino Neto, muasisi wa Taifa la Angola.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Sharifa Nyanga, akiwa hapo, Rais Samia ataweka shada la maua kwenye eneo maalumu lililopo kaburi la muasisi huyo.

Itakumbukwa uhusiano wa nchi mbili hizi uliasisiwa na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na hayati Rais Antonio Neto waliokuwa na maono ya kutaka kuiokomboa Afrika na watu wake kutoka mikononi mwa wakoloni.

Nyanga amesema baadaye leo mchana, Rais Samia atalihutubia Bunge la Angola kabla ya kutembelea kiwanda cha kusafisha mafuta (Luanda Oil Refinery).

Huko atapokelewa na Waziri wa Madini wa Angola, Diamantino Pedro Azevedo

Rais Samia amealikwa na Spika wa Bunge la Angola, Carolina Cerqueira. Samia anakuwa Rais wa kwanza mwanamke kutoka barani Afrika kuhutubia Bunge hilo.

“Lakini pia Rais Samia atazungumza na waandishi wa habari baada ya kulihutubia Bunge huko Ikulu,” amesema Nyanga.

Uhusiano huo umeendelea kuimarika siku hadi siku na sasa unajikita katika kukuza uchumi hasa katika sekta za biashara, uwekezaji, maendeleo ya miundombinu, mafuta na gesi, madini, uchumi wa buluu, afya, elimu na utalii kama zilivyoainishwa kwenye Tume ya pamoja ya Ushirikiano.

Aidha, wakati wa ziara hiyo itashuhudia pia uwekaji saini wa hati za makubaliano (MOU) katika masuala yanayolenga kufungua fursa za biashara na uwekezaji na jitihada za kuimarisha ulinzi na usalama.

Ziara hii imekuja miaka 19 tangu marais wa Tanzania kufanya ziara za kiserikali nchini Angola.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.