Dar es Salaam. Changamoto ya ubovu wa barabara ni kero kwa wananchi, hususani barabara za mitaa, wanana vijijini na pembezoni mwa miji, hali inayochangia ugumu wa maisha kutokana na miundombinu kuharibika.
Uharibifu huu wa miundombinu ya barabara yakiwamo madaraja, baadhi kutokana na mvua una athari kwa jamii kutokana na nauli kupanda, bidhaa kuongezeka bei, huku wananchi wakipata wakati mgumu kuzifikia huduma zingine za kijamii kama vile za shule na hospitali.
Ni kutokana na changamoto wanazopitia, baadhi ya wananchi kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa huunganisha nguvu pamoja kufanya ukarabati au ujenzi wa maeneo ya miundombinu iliyoharibika.

Wananchi wa Goba kwa Awadhi wakiwa wamejitolea kutengeneza barabara ambapo walijichangisha fedha kwa ajili ya matengenezo hayo.
Katika kutekeleza hilo, wapo ambao huchangia nguvu kazi na wengine fedha licha ya ukweli kuwa, kazi hiyo ni jukumu la Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) ulianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Wakala za Serikali Sura Na. 245 na kutangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali Na. 211 la Mei 12, 2017.
Wakala huo ulioanza kufanya kazi Julai Mosi, 2017 unalenga kukabiliana na changamoto zilizojitokeza wakati jukumu la Menejimenti ya Mtandao wa Barabara za Wilaya lilipokuwa chini ya mamlaka za serikali za mitaa na mabadiliko katika sekta ya barabara kwa nia ya kuboresha huduma na kuongeza ufanisi.
Jukumu kubwa la Tarura ni kusimamia matengenezo, ukarabati na ujenzi wa mtandao wa barabara za wilaya zilizokuwa zikisimamiwa na mamlaka za serikali za mitaa na kuratibiwa na Ofisi ya Rais –Tamisemi chini ya Idara ya Miundombinu.
Wakala pia hupima na kufanya tafiti kuhusu vifaa vya ujenzi kupitia Kitengo cha Maabara Kuu ya Vifaa na Utafiti, kudhibiti uzito wa magari barabarani na kulinda maeneo ya hifadhi za barabara.

Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Tangini Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani wakiendelea na kazi ya kujitolea ya kutengeneza barabara ya mtaa huo ambayo imeharibika na kusababisha magari kushindwa kupita kuelekea kwenye makazi yao. Picha na Sanjito Msafiri
Wakala hutekeleza majukumu yake kwa kuingia mikataba maalumu (APA) kati yake na Mfuko wa Barabara kwa kazi za matengenezo ya barabara na Ofisi ya Rais –Tamisemi kwa kazi za miradi ya maendeleo.
Wakazi wa Mtaa wa Tangini katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mkoa wa Pwani Mei 16, 2025 waliunganisha nguvu kutatua kero ya ubovu wa barabara inayotoka Mailimoja hadi mtaani kwao baada ya changamoto hiyo kuwapo kwa muda mrefu pasipo mamlaka husika kuitatua.
Kwa mujibu wa wananchi hao, barabara hiyo imekuwa mbaya kiasi cha magari kushindwa kufika mtaani, hivyo kuwa kikwazo hasa wakati wa dharura kwa wagonjwa au wajawazito wanaohitaji kufikishwa hospitalini usiku.
“Tumeamua kuchukua hatua sisi wenyewe. Kila mmiliki wa nyumba anachangia Sh5,000 na mpangaji Sh3,000. Tunakusudia kutumia fedha hizo kununua vifusi, mawe na kushirikiana na mafundi wa ujenzi wa barabara ili kuifanya ipitike,” anasema Salina Yombayomba, mkazi wa mtaa huo.
Amesema wako tayari kushiriki shughuli za maendeleo wakisubiri kuungwa mkono na Serikali.
Mwenyekiti wa mtaa huo, Iddi Mfaume amesema serikali ya mtaa inafahamu changamoto hiyo na imeshapeleka maombi kwa halmashauri, wakisubiri msimu wa mvua upite ili kuanza matengenezo kupitia mamlaka husika.
“Siyo barabara ya Tangini pekee iliyoharibika ni nyingi. Tunawasihi wananchi kuwa wavumilivu, lakini pia tunapongeza juhudi za wananchi kwa kuonyesha mfano wa kuchukua hatua,” amesema.
Baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Kinzudi, Kata ya Goba wilayani Ubungo, Dar es Salaam walianzisha kampeni kuchangia Sh180 milioni ili kujenga barabara na mitaro kukabiliana na adha wanayopata msimu wa mvua.

Walianza ujenzi baada ya kukusanya Sh22 milioni, wakieleza kwa zaidi ya miaka 10 wamesubiri mamlaka husika kufanya kazi hiyo bila mafanikio.
Hata hivyo, Meneja wa Tarura, Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Mkinga alipoulizwa kuhusu ujenzi huo, amesema anafahamu suala hilo na wametenga bajeti ya kuwaongezea.
“Serikali kupitia Tarura tumetenga kwenye bajeti Sh239 milioni kwa ajili ya kwenda kuunga mkono juhudi zao kwa kuitengeneza barabara hiyo kwa kilomita zote mbili,” alisema alipozungumza na Mwananchi Machi 19, 2024.
Mkazi wa eneo hilo, Mhandisi Edson Misana amesema barabara hiyo inayoitwa Awadhi ina urefu wa kilomita mbili inatoka Goba na kutokea Salasala.
“Sisi wananchi wa eneo hili tunaitumia njia hii kwenda kwenye shughuli zetu na kurudi, hatuna njia nyingine mbadala na kipindi cha mvua gari ikikwama usafiri unaacha njiani, unaenda nyumbani kwa miguu maana hata pikipiki haipiti,” amesema.
Amesema michango inakusanywa kulingana na watu walivyojaliwa kipato lakini waliweka kiwango cha kuanzia Sh400,000 hadi Sh500,000.
Mwenyekiti wa usimamizi wa ujenzi huo kwa niaba ya wananchi wa eneo hilo, Joseph Mboya amesema barabara hiyo hutumiwa na wakazi wengi yakiwamo magari ya watoto wa shule.
“Tuliona kusubiria bajeti ya Serikali tunaweza kuchelewa kufanya mambo yetu mengine na kuna wakati tunawabeba watoto hadi barabarani wakapande gari waende shule,” amesema.
Changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara katika eneo la Kiruweni, Kata ya Mwika Kusini wilayani Moshi iliwalazimu wananchi wa eneo hilo waishio maeneo mbalimbali nchini kuchangishana fedha na kuanza ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 72 kwa kiwango cha changarawe.
Eneo hilo ambalo wananchi wanajishughulisha na uzalishaji wa ndizi na kilimo cha mazao mbalimbali, limekuwa na changamoto ya miundombinu ya barabara hivyo iliwalazimu kusafirisha mizigo kwa kichwa hadi sokoni.
Chimbuko la wazo la ujenzi wa barabara lilianzia katika Usharika wa Kiruweni wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), baada ya mvua zilizonyesha mwishoni mwa Machi na Aprili, 2024.
Akizungumza kuhusu ujenzi huo mwaka jana, Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kiruweni, Joram Mamuya amesema barabara zilifikia hatua mbaya na kufanya wananchi kushindwa kutumia vyombo vya usafiri, hivyo kulazimika kubeba mazao kichwani kupeleka sokoni, huku wakitembea umbali mrefu.
“Tuliwaomba Tarura wakafika, wakakagua barabara na kutupa ushauri namna bora ya kuzifanyia kazi. Sisi kwa pamoja tukaona tuanzie hapo. Gharama walizotupa zilikuwa kubwa, zaidi ya Sh180 milioni, lakini haikutukatisha tamaa. Tuliungana kwa pamoja kama jamii na kuanza kazi hii,” alisema.

Caren Boniface, mkazi wa Kimara King’ongo wilayani Ubungo, Dar es Salaam amesema madereva wa bajaji na pikipiki walichanga fedha wakaweka kifusi kuwezesha barabara kupitika maeneo yenye utelezi.
Maiko Joram, mkazi wa eneo hilo ambaye ni dereva bodaboda amesema walilazimika kupandisha nauli kutoka Sh2,000 hadi Sh3,000 huku bajaji ikitoka Sh1,000 hadi Sh2,000 kwa mtu mmoja kwa umbali usiozidi kilomita tatu kutokana na ubovu wa barabara.
Amani Kyaro, mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi Mtaa wa Zingiziwa, amesema magari yanayowapelekea mizigo yamekuwa yakikwama, hivyo walilazimika kuchangishana wenye maduka ili kutengeneza barabara kwa kushirikiana na serikali ya mtaa.
Mwenyekiti wa Kitunda Relini, Wilaya ya Ilala, Sospeter Marwa amesema wananchi wamekuwa wakichangishana fedha ili kurekebisha barabara.
Meneja wa Tarura Mkoa wa Dar es Salaam, Godfrey Mkinga amesema wananchi wanapojitolea kutengeneza barabara wanapaswa kuandika barua kwa wakala huo kueleza wanataka kujenga ya aina gani (ya muda mrefu au mfupi). Pia waainishe ni ya udongo, changarawe, lami au zege.
Sharti lingine ni lazima washirikishe ofisi ya serikali ya mtaa ambayo itasimamia uchangishaji.
Kwa upande wa Tarura amesema watatoa wakandarasi washauri wa kusimamia kazi kuhakikisha barabara inatengenezwa kwa kiwango kinachotakiwa.
“Katika ujenzi wa barabara ukiacha wananchi, wapo pia watu binafsi wamekuwa wakifanya hivyo, mfano barabara zilizojengwa kwa mtindo huo ni ile ya Rose Garden na Senga za Mikocheni, zenye zaidi ya kilomita 300,” amesema.
Hata hivyo, amesema wakati sekta nyingine zikihamasisha uchangiaji ujenzi, wao huhamasisha zaidi utunzaji wa barabara hizo, ikiwamo kuheshimu njia za dharura, za wapita kwa miguu na zile za akiba.
“Tunasisitiza hili kwa kuwa tunapokuja kufanya utanuzi wa barabara kutokana na wananchi wengi kuvamia hifadhi za barabara tunatumia gharama kubwa na muda mwingi kushughulikia fidia badala ya ujenzi,” amesema.
Akieleza namna walivyojipanga kushughulikia ubovu wa barabara, amesema kwa sasa wanasubiri mvua ziishe, akieleza ndiyo sababu ya malalamiko kuwa barabara nyingi ni mbovu.
Amesema hawawezi kufanya chochote kwa sasa labda kuwe na dharura kuwa barabara husika haipitiki kabisa.
Ameongeza kuwa endapo mtu hatafuata utaratibu atalazimika kutengeneza tena barabara hiyo kwa gharama zake kama amesababisha uharibifu na kuleta kero kwa watumiaji.
Alisema anaweza kupewa adhabu ya kulipa faini Sh1 milioni au kifungo cha mwaka mmoja hadi miwili kwa mujibu wa sheria ya barabara na kanuni zake ya mwaka 2007.
Crédito: Link de origem