Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Ni rasmi Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa wabunge, madiwani na urais, utakaofanyika baadaye mwaka huu, baada ya chama hicho, kususia kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima amewaambia wanahabari jijini Dodoma leo kwamba Chadema hakitashiriki uchaguzi mkuu, wala chaguzi ndogo zitakazofuata baada ya kugomea kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kinachofuata hivi sasa baada ya vyama vya siasa, Serikali na INEC kusaini kanuni hizo, wanakwenda kuzichapisha katika gazeti la Serikali kama ilivyo taratibu.
“Utaratibu wa kusaini kanuni hizi upo leo tu, hakutakuwa na siku nyingine, kwa hiyo chama ambacho hakijasaini hakitaweza kushiriki uchaguzi na chaguzi nyingine ndogo zitakazofuata kwa muda wa miaka mitano,” alisisitiza Kailima.
Hivyo basi, kutokana na hatua hiyo, Chadema italazimika kusubiria hadi mwaka 2030, ndipo ishiriki Uchaguzi Mkuu mwingine lakini siyo wa mwaka 2025, baada ya kupoteza fursa hiyo.
Kusainiwa kwa kanuni hizo ni takwa la kifungu cha 162 cha Sheria ya Uchaguzi wa Marais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024, kinachovitaka vyama vya siasa, Serikali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kusaini kanuni hizo.
Wakati Chadema wakisusia mchakato huo, vyama vingine vikubwa vya siasa nchini vimeridhia na kusaini kanuni hizo, vikiwemo vya CCM, ACT Wazalendo, ADC, NLD, Chauma, AAFP, Demokrasia Makini, CUF, UDP, DP, UPDP, NCCR-Mageuzi, NRA, Ada -Tadea, UMD, TLP na CCK na SAU.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya mfumo wa vyama vingi nchini, uchaguzi mkuu 2025 utasimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi, ambayo ni zao la kikosi kazi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, mwaka 2023 aliyetaka kuwepo kwa uwanja sawa wa demokrasia katika mchakato wa uchaguzi.
Crédito: Link de origem