Na Mwandishi Wetu
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua Benki ya Ushirika (Coop BankTanzania), lengo likiwa ni kufufua benki za kijamii zilizofilisika nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 10, Dodoma, Waziri wa Kilimo, Husein Bashe amesema Wizara ilipokea maagizo ya Rais Samia, kuhakikisha benki za kijamii zilizofilisika zinarejea na katika hatua za awali Aprili 28, 2025 Rais anatarajiwa kuzindua Benki ya Ushirika nchini.
Amesema benki hiyo itazinduliwa ikiwa na matawi manne ambayo yanapatikana Dodoma, Mtwara, Kilimanjaro na Tabora.
“Hatua ya pili itahusisha matawi ya Kagera, Mwanza,Dar es Salaam, Mbeya na Katavi.
Mafunzo kwa mawakala yanaendelea hivyo mbali na matawi hayo kutakuwa na mawakala nchi nzima na kabla ya uzinduzi mnamo Aprili 28 kutatanguliwa na kongamano la wanaushirikika Aprili 27,”amesema Bashe.
Amesema, benki nyingi za ushirika zimefilisika na Rais Dk.Samia ameona haja ya kurejesha benki hizo ili kuinua uchumi kwa jamii hususani wa wakulima.
“Lengo hapa ni wakulima na jamii kuwa na benki ambazo zitawasaidia na kuwaondolea adha wanazokutana nazo katika Benki za kibiashara,” amesema.

Waziri Bashe ameongeza kuwa, mbali na hatua hiyo ya uzinduzi wa benki hiyo, Wizara inaendelea na mazungumzo na Wizara ya Fedha na Mipango kuona haja ya kuiacha Benki ya Kilimo (TADB) ifanye kazi zake za msingi za kuwawezesha wakulima.
“TADB ni Benki ya Kilimo si ya biashara hivyo hata mikopo yake inatakiwa isiwe ya kibishara wakulima wetu hawawezi mikopo ya marejesho ya miaka miwili ama mitatu inawaumiza,” amesema.
Ametoa wito kwa washiriki wa mkutano huo kujiandikisha kwa wingi na kutumia fursa hiyo kunufaika na huduma za kibenki zitakazotolewa.
Crédito: Link de origem