Migori. Katika hali isiyo ya kawaida, Rais wa Kenya, William Ruto, amejikuta akipigwa na kiatu mkononi kilichorushwa kutoka kwenye umati wa watu aliokuwa akiwahutubia katika mji wa Kehancha Magharibi mwa Kenya.
Tovuti ya Nation ya nchini humo imeripoti kuwa tukio hilo la kushtukiza kwa Ruto limetokea leo Jumapili, Mei 4, 2025, katika siku ya tatu ya ziara yake katika Kaunti ya Migori magharibi mwa nchi hiyo.
Kipande kifupi cha video kilichosambazwa mitandaoni kuhusiana na tukio hilo kinaonyesha kiatu kikimfikia Rais Ruto katika mkono wake wa kushoto alipokuwa akihutubia umati huo.
Kikosi cha usalama wa Rais kilichukua hatua mara moja kumlinda kiongozi huyo wa nchi, ingawa tayari kiatu kilikuwa kimempiga kichwani.
Tayari maofisa wa polisi katika eneo la Kuria Magharibi, Kaunti ya Migori, wamethibitisha kuwakamata watu watatu wanaoshukiwa kurusha kiatu hicho kwa Rais Ruto.
Ofisa usalama aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina kutokana na unyeti wa suala hilo amethibitisha kuwa uchunguzi unaendelea na washukiwa zaidi wanatafutwa.

Aliongeza kuwa matokeo ya awali yanaashiria kuwa tukio hilo linaweza kuwa na msukumo wa kisiasa na huenda lilipangwa kabla ya ziara ya Ruto.
Ofisa huyo pia alieleza kuwa mamlaka zimekaribia kumbaini mshukiwa mkuu anayeaminika kuwa muhusika muhimu katika tukio hilo, jambo ambalo linaweza kusaidia pakubwa katika uchunguzi wake.
“Tupunguze gharama ya…” Rais Ruto anasikika akisema kabla ya kupigwa na kiatu kichwani.
Ruto alisitisha hotuba yake kwa muda mfupi, hotuba ambayo ilikuwa ikilenga kuzungumzia jitihada za Serikali kupunguza gharama ya pembejeo kwa wakulima wa Kehancha.
Maofisa wa usalama waliokuwa wakimlinda Rais walikimbilia haraka jukwaani, na mkutano huo ukakatizwa kwa dakika chache.
Baadhi ya wabunge wamelaani tukio hilo wakisema kuwa lilihatarisha maisha ya Rais.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari
Crédito: Link de origem