Krasnodar. Rais wa Urusi, Vladimir Putin amependekeza Ukraine iwekwe chini ya utawala wa muda ili kuruhusu uchaguzi mpya kufanyika huku akisisitiza kuwa takwa hilo likitekelezwa atakuwa tayari kwa ajili ya kutiwa saini kwa makubaliano muhimu ya kusitisha vita kati ya mataifa hayo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, Rais Putin alitoa kauli hiyo jana Alhamisi wakati wa ziara yake katika bandari ya Kaskazini ya Murmansk nchini Urusi.
Kauli hiyo ya Putin imekuja wakati ambao Marekani inapambana kufanikisha makubaliano ya kumaliza vita kati ya mataifa hayo kwa kurejesha mawasiliano na Russia na kushiriki mazungumzo ya aina tofauti na mataifa hayo hasimu.
Kiongozi huyo wa Russia alisema anaamini kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump, anataka amani kwa dhati.

Tangu kuanza operesheni zake za kijeshi nchini Ukraine, Februari 2022, Urusi imeyatwaa maeneo ya Ukraine ikiwemo katika Mkoa wa Donetsk, Luhansk, Kherson, Zaporizhia, Pokrovisk na Crimea iliyotwaliwa tangu mwaka 2014.
Vita hiyo inatajwa kusababisha vifo vya makumi kwa maelfu kwa kila pande na mamia kwa maelfu wakijeruhiwa, huku mamilioni wakigeuzwa kuwa wakimbizi.
Pia, imesababisha uharibifu wa miundombinu ya makazi, miji na kusababisha mvutano mkubwa zaidi kati ya Russia na mataifa ya Magharibi kwa miongo kadhaa.
Pendekezo la Putin la kuanzishwa kwa utawala wa muda linaonekana kulenga malalamiko yake ya muda mrefu kwamba mamlaka za Ukraine, haziko madarakani kihalali wa mazungumzo, kwani Rais Volodymyr Zelenskyy ameendelea kuwa madarakani baada ya muda wake wa utawala kikatiba kumalizika Mei 2024.
“Kimsingi, bila shaka utawala wa muda unaweza kuanzishwa Ukraine chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, Marekani, mataifa ya Ulaya na washirika wetu,” amenukuliwa akisema alipokuwa akizungumza na mabaharia katika Bandari ya Murmansk.

“Hii itakuwa kwa madhumuni ya kuandaa uchaguzi wa kidemokrasia na kuleta madarakani serikali yenye uwezo na inayotegemewa na wananchi, kisha kuanza mazungumzo nao kuhusu makubaliano ya amani.”
Alisema juhudi za Trump kuanzisha mazungumzo ya moja kwa moja na Russia kinyume na mtangulizi wake Joe Biden, ambaye aliepuka mawasiliano, zinaonyesha kuwa rais huyo mpya wa Marekani anataka amani.
“Kwa maoni yangu, rais mpya wa Marekani kwa dhati anataka kumaliza mzozo huu kwa sababu kadhaa,” alisema.
Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani, alipoulizwa kuhusu kauli hiyo ya Putin kuhusu utawala wa muda, alisema utawala wa Ukraine unaamuliwa na katiba yake na wananchi wake. Hata hivyo, hakukuwa na kauli yoyote ya haraka kutoka kwa Ukraine.
Viongozi wa Ulaya wameendelea na jitihada zao, wakiahidi katika mkutano wa Paris, Ufaransa jana Alhamisi kuimarisha Jeshi la Ukraine ili kuhakikisha kuwa linakuwa msingi wa usalama wa nchi hiyo siku zijazo.
Ufaransa na Uingereza zinajaribu kupanua msaada kwa kikosi cha uhakikisho wa usalama cha kigeni iwapo kutakuwa na makubaliano ya kusitisha mapigano na Urusi.
Zelenskyy amekataa madai yoyote yanayohoji uhalali wake wa kisiasa, akisema kuwa sheria ya Ukraine hairuhusu uchaguzi kufanyika chini ya sheria ya kijeshi na hata kama ingekuwa inawezekana, kufanya uchaguzi wakati wa vita ni jambo lisilowezekana.

Katika siku za hivi karibuni, Zelenskyy amemshtumu Putin kwa kutaka kuendelea na vita.
Utawala wa Trump umependekeza makubaliano mapya na makubwa zaidi kuhusu madini na Ukraine, kulingana na vyanzo vitatu vinavyojua mazungumzo yanayoendelea na muhtasari wa rasimu ya pendekezo hilo uliopatikana na Reuters.
Trump amesema makubaliano ya madini yatasaidia kufanikisha mkataba wa amani kwa kuipa Marekani maslahi ya kifedha katika mustakabali wa Ukraine.
Katika kauli yake, Putin amesema Urusi inaendelea kusonga mbele kwa uthabiti katika kufanikisha malengo yake ya operesheni yake nchini Ukraine.
“Urusi inaunga mkono suluhisho la amani kwa mizozo yote, ikiwemo huu, kwa njia za amani lakini si kwa hasara yetu,” amesema.
“Katika mstari mzima wa mapigano, wanajeshi wetu wanashikilia mpango wa kimkakati. Tunapiga hatua labda si kwa kasi ambayo baadhi wangependa lakini kwa uthabiti na kwa kujiamini tunasonga kuelekea kufanikisha malengo tuliyojiwekea tangu mwanzo wa operesheni hii,” amesisitiza.
Zaidi ya miaka mitatu tangu uvamizi mkubwa wa Ukraine, vikosi vya Urusi sasa vinadhibiti takriban asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine.
Vikosi vyake pia vimerejesha maeneo mengi iliyoanza kuyapoteza wakati wa uvamizi wa Ukraine mwezi Agosti mwaka jana katika mkoa wa Kursk, magharibi mwa Urusi.
Putin alisifu juhudi za umoja wa Brics katika kutafuta suluhisho, akitaja China na India kwa namna ya pekee.
Alisema Urusi iko tayari kushirikiana na mataifa mengi, ikiwa ni pamoja na Korea Kaskazini, kusaidia kumaliza vita.
Vyanzo vya magharibi na Ukraine vinasema kuwa zaidi ya wanajeshi 11,000 wa Korea Kaskazini wamepelekwa kusaidia vikosi vya Urusi katika Mkoa wa Kursk, ingawa Moscow haijathibitisha hilo.
Putin alisema Urusi pia iko tayari kushirikiana na Ulaya, lakini akasema bara hilo linafanya maamuzi yasiyo thabiti.
“Mataifa ya Ulaya yanajaribu kutuvuruga, lakini ni sawa, tumezoea. Natumai hatutafanya makosa yoyote kutokana na kuwaamini kupita kiasi washirika wetu wa kigeni,” amesema.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika ya Habari.
Crédito: Link de origem