top-news-1350×250-leaderboard-1

PPRA yasisitiza matumizi ya mfumo wa ununuzi wa Nest

Dodoma. Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imevitaka vitengo vya ugavi vya sekretarieti ya mikoa, halmashauri na ngazi za serikali za mitaa kuhakikisha kuwa ununuzi wa umma unafanyika kwa kutumia mfumo wa kidijitali wa Nest kwa mujibu wa sheria.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Machi 7, 2025 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Denis Simba wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo wataalamu wa ununuzi kutoka halmashauri 184.

Mafunzo hayo yamewahusisha pia wakuu wa vitengo vya ununuzi na maofisa wa ununuzi na ugavi, wataalamu wa Tehama kutoka halmashauri zote na wakuu wa vitengo vya ununuzi kutoka ofisi za sekretarieti za mikoa 26.

Simba amesema kupitia sheria ya ununuzi wa umma, taasisi za ununuzi zote zikiwemo ngazi za serikali za mitaa zinatakiwa kutumia mfumo wa Nest katika ununuzi wowote wanaoufanya, na mfumo huo unaongeza uwazi na ushindani katika shughuli za mnyororo wa ununuzi na ugavi.

“Mfumo huu umewasaidia wanaoutumia, lakini kwa ambao bado wana changamoto ndiyo maana tunatoa elimu hii ili na waweze kufikia viwango vya wenzao ambao mpaka sasa wanafurahia matumizi ya mfumo huu wa Nest,” amesema Simba.

Amesema mfumo huo unatoa fursa kwa wazabuni wadogo na wakubwa, makundi maalumu, wanawake na vijana kuhusika katika ununuzi wa umma na kwamba ununuzi wa umma hauhusishi tu kampuni kubwa bali pia unaongeza fursa za kiuchumi kwa wadau wadogo na wa kati katika jamii.

“Tunapokuja kwenye makundi maalumu ambapo Serikali iliamua kutenga asilimia 30 kwa ajili yao ni hatua ya kizalendo kwelikweli na sisi tuna nafasi ya kuhakikisha kwamba tunatekeleza hilo,”

“Sisi ndiyo chanzo cha kuhakikisha makundi hayo yanaingia na mimi nina uhakika kwamba tukiweza kutekeleza hili la asilimia 30 tunazungumzia takribani Sh5 hadi Sh6 trilioni ambayo tunaweza tukaingiza kwenye haya makundi maalumu na wao hata kama siyo ajira za moja kwa moja wakapata kufanya biashara na serikali ambazo zitawapa kipato cha vipindi vifupivifupi na wenyewe watakuwa wameshaingia kwenye mfumo rasmi wa malipo kupitia serikali.”

 “Ni jukumu letu sisi wakuu wa vitengo vya ununuzi na maofisa ununuzi na wote ambao tunaanzisha michakato, kuhakikisha tunatekeleza jukumu letu ili tuweze kutengeneza kampuni kubwa za wazawa na kama wengi wanavyosema kutengeneze mabilionea wa Kitanzania,” amesema.

Mshiriki wa mafunzo hayo kutoka Halmashauri ya Kondoa, Winfrida Mwabuki amesema wanakutana na changamoto wakati wa kufanya ununuzi ikiwemo kuwa na makisio ya bajeti yasiyo na uhalisia, hivyo kufanya wazabuni washindi kutopatikana.

Amesema pia  kuwa na gharama kubwa za wazabuni kulinganisha na bei ya taasisi nunuzi, zabuni zilizopata wazabuni lakini wameshindwa au wamechelewa kuanza utekelezaji wa mikataba na baadhi ya wazabuni kuwa na mikataba mingi, hivyo kushindwa kuitekeleza kwa wakati.

Pia, kuna mwamko mdogo wa wazabuni kujisajili kwenye mfumo wa Nest, uelewa mdogo kwa watumiaji wa mfumo kwa upande wa taasisi nunuzi, uelewa mdogo kwa wazabuni katika kujaza bei katika mfumo wa Nest, kutopata wazabuni kwa wakati jambo linalochelewesha utekelezaji wa miradi na mafundi wanaoomba kazi kuwa wachache.

Naye meneja wa kujenga uwezo na huduma za ushauri  kutoka PPRA, Gilbert Kamnde amesema mafunzo hayo yametolewa kwa watumishi wa mamlaka za serikali za mitaa kwa kuwa ndiyo watekelezaji wa kwanza wa mfumo kwa huduma wanazozitoa kila siku katika jamii kupitia ununuzi na ugavi.

Amesema baada ya mafunzo hayo hawatarajii kuona manunuzi yanafanyika nje ya mfumo kwa kisingizio chochote, kwani ni takwa la kisheria la kutumia mfumo wa kidijitali kufanya ununuzi wa umma.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.