Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amewataka wanafunzi katika utafutaji elimu na maisha, wakumbuke kusimamia ukweli na kutetea haki za watu badala ya kutaka kujinufaisha wenyewe.
Akitoa mfano wa yeye alivyosimamia haki za wengi akafukuzwa kazi, Othman amesema iwapo wakifanya hivyo si tu wanachangia kupata jamii yenye maadili lakini jambo hilo litawapa heshima na amani katika nafsi zao.
Othman ametoa kauli hiyo jana Machi 27, 2025 alipojumuika na wanafunzi wa shule ya High View katika futari aliyowaandalia.
“Tunapotafuta elimu na maisha tukumbuke kuzingatia haki za wengi na kusimamia ukweli, jambo ambalo wengi hawafanyi. Hili litakuachia amani ya nafsi na heshima kwa kulinda jamii,” amesema.
“Binafsi nilikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu na baadaye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa takribani miaka 22 nilikuwa katika uteuzi wa Rais, lakini lilipokuja suala la kuchagua baina ya haki ya watu na kazi yangu, mimi nilichagua kusimamia haki ya watu,” amesema.
Mwaka 2014 wakati wa Bunge la Katiba jijini Dodoma, Othman alipiga kura ya wazi akipingana na wajumbe wenzake kuhusu Zanzibar kuwa na mamlaka kamili.
Akitoa salamu na nasaha kwa wanafunzi hao wa kidato cha sita na wanaotarajia kufanya mtihani mwaka huu, Othman amesema wanafunzi wanatakiwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu mbele na kufanya juhudi ili kupata mafanikio katika utafutaji wa elimu na maisha kwa ujumla.
Amewatakia kheri wanafunzi hao katika mitihani, akiwasisitiza kuwa elimu pekee haitoshi bali heshima na mwenendo mwema ndiyo vitakapowapatia mwanga katika maisha.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Said, amesema tayari Serikali ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeandaa nafasi maalumu za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi watakaofanya vizuri kwenda kusoma nje ya nchi.
Hivyo, amewataka kujitahidi ili wanufaike na udhamini huo.
Baadhi ya wanafunzi, akiwamo Miriana Kheri amesema watazingatia jambo hilo na kuhakikisha wanatenda haki katika mifumo yao ya masomo na maisha.
Crédito: Link de origem