top-news-1350×250-leaderboard-1

Othman: ACT Wazalendo tulijishusha ili kuingia SUK lakini…

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud amesema chama hicho kilikubali kujishusha na kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (Suki) ili kujenga mshikamano na kuboresha maisha ya Wazanzibari.

Amesema licha ya jitihada hizo zilizofanywa na ACT Wazalendo, ikiwemo kuzungumza na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na Rais Samia Suluhu Hassan, bado hakuna matunda ya kuridhisha yaliyopatikana katika kuleta hali ya umoja na mshikamano.

ACT Wazalendo, ilingia kwenye mvutano na Serikali ya Zanzibar, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, ambapo chama hicho, kilidai mchakato huo uligubikwa na dosari mbalimbali ikiwemo viongozi na wanachama wao kujeruhiwa na wagombea wao kuporwa ushindi.


Kutokana na hilo, aliyekuwa mgombea wa urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad (marehemu) na ujumbe wa chama chake waliketi meza na moja ya mazungumzo na Dk Mwinyi ili kumaliza tofauti zilizozaa SUK.

Katika makubaliano hayo, ACT iliweka masharti mbalimbali kuchunguza matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa uchaguzi na kufanyika kwa marekebisho ya mfumo nzima wa uchaguzi, ili uwe huru na haki.

Akizungumza jana Jumatatu Juni 16, 2025 na wanadiaspora wa Zanzibar waishio Uingereza, Othman amedai baada ya kuchukua kijiti kutoka kwa mtangulizi wake, Maalim Seif alikutana na Dk Mwinyi na kumwambia kuwa matamanio yake ni kushirikiana naye ili kuivusha Zanzibar kutoka ilipokuwa.

Othman ameleeza hayo kupitia video fupi iliyotumwa kwenye vyombo vya habari iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano Katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

“Nilimwambia nataka tuunganishe Wazanzibari, tujenge misingi ya kiistaarabu ya kuijenga Zanzibar ili tuachie nchi iliyosimama kwa misingi endelevu. Nilimwambia nitume lolote unalotaka na kama kuna maeneo naweza kukusaidia nipo tayari,” amesema.

“Kama haitoshi nilikaa na chama changu nikawaambia tuingalie Zanzibar, siyo ACT tuachane na siasa za mashindano kwa sababu Zanzibar inahitaji mpango wa muda mrefu ili kutoka ilipo. Niliwaambia tukubaliane yapi yataionyoosha Zanzibar ili tukae na viongozi wenzetu tunawaeleze na sisi tupo tayari kufanya naye (Dk Mwinyi)  kazi kwa muda mrefu,” amedai.


Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, yupo ziarani nchini Uingereza amefichua kuwa mpango wa chama hicho, ulikuwa ni kuwania ubunge na uwakilishi, lakini kwa urais waliamua kumuachia Dk Mwinyi aendelee kuongoza.

“Tulijitoa kwa haya kwa maslahi ya Zanzibar, sasa leo tunavyoonekana tunagombea nataka mjue hatogombei kwa furaha au ndio lilikuwa lengo letu? Bali lengo letu lilikuwa tunataka Zanzibar inyooke, ndio maana tulitengengeza waraka unaofafanua haya,” amesema.

“Licha ya kufanya yote haya inaonyesha wenzetu wanaelekea kusini sisi kaskazini, tulijishusha na kujiteremsha lakini tulipofikia ni hapo. Kila kiongozi mstaafu tumefikia ili atusaidie kuondoka katika mkwamo, lakini hatujakata tamaa, tunaendelea na jitihada za…,” amesema Othman.

Katibu wa Kamati Maalumu ya Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis, amesema chama hicho, kimeshangazwa na hatua ya Othman kueleza hayo akiwa Uingereza kikisema ni matumizi mabaya ya muda.

Mbeto amesema si kweli kilichosemwa na Othman makubaliano ya kimsingi kati ya CCM na ACT ni kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar yanayotajwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.

“Si kweli kama  kulikuwa na mpango wa kugawana madaraka kama inavyodaiwa na Othman au wakati wa Hayati Maalim Seif alipokuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar,” amedai Mbeto.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.