top-news-1350×250-leaderboard-1

Njia tatu za Kimungu kuleta amani penye mgogoro, chuki

MAANDIKO: MWANZO 33:1-20 (Mistari 1-3 na 11)

Bwana Yesu asifiwe. Suala la kutoelewana limekuwa changamoto katika maisha ya mwanadamu. Migogoro katika ndoa, dini, siasa, koo, kazini nk. Matokeo yake ni kushuka kwa uchumi, siasa kuyumba, mmomonyoko wa maadili, kukosa umoja, vita nk. Wengine wanaamini katika waganga, vita kama suluhisho ila wanasahau dawa ya kupata amani ni maridhiano.

Maridhiano ni hali ya pande mbili zilizokuwa hazielewani hapo awali kuja kwenye meza ya amani kwa kila upande.

Hatua tatu za Kimungu za kutusaidia kupitia maridhiano.

1. Kuwa na mpango mkakati (Mstari wa1-2)

Yakobo na Esau, watoto wa Isaka wanapatana wenyewe baada ya Essau kuuza haki ya mzaliwa wa kwanza kwa Yakobo kwa chakula. Isaka akambariki Yakobo badala ya Esau, lakini Esau akapanga kumuua Yakobo kwa kuiba mbaraka wake za mzaliwa wa kwanza, Yakobo akakimbilia mafichoni, baada ya miaka 20 akatuma wajumbe kumjulisha Esau kuwa anarudi. Lakini Yakobo akapanga kwa uangalifu familia yake kimakundi ikiwa Esau atakuja kwa shari.

(Methali; Kinga ni bora kuliko tiba)

Ndugu, kutafuta amani kunahitaji maandalizi maana lolote linaweza kutokea wakati wa mchakato. Ikumbukwe migogoro mingi (siyo yote) husababishwa na shetani na tamaa zetu. Amani hutoka kwa Mungu, ni pande mbili zinazokinzana, kazi ya shetani ni kuharibu lakini kazi ya Mungu ni kuleta uzima/amani.

Yatupasa kupanga ni wakati gani, naenda na nani, tunakutana wapi (si kila sehemu inafaa). Je, mtu huyo yuko katika hali gani (mood). Pengine kafiwa, kafukuzwa kazi, kaibiwa au anaumwa. Je, akiwa na hasira nimpokeeje. Yote haya ni mipango mkakati.

Luka 14:28 “Kwa maana ni nani kati yenu, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba ana kiasi cha kuumaliza?”

Yesu anatufundisha kuwa kabla ya kufanya maridhiano au jambo lolote tunahitaji kuwa na mipango mkakati ili tuweze kufikia lengo lililokusudiwa. Kaa chini ufikirie nini kitatokea ikiwa hutaweza kufanikiwa na njia gani ya kutumia.

Namna ya kuwa na mipango mkakati:

Maombi; Mungu akusaidie hiyo mipango.

Hali ya utulivu wa kina,  kwani wengine huzua migogoro zaidi.

2. Kutoa baadhi ya mali zako – (Mstari wa 11)

Yakobo anamtolea Esau zawadi za mifugo kuonyesha shauku ya amani na kufidia makosa yake, haikuwa tu ishara ya ukarimu, bali juhudi za kurejesha uhusiano na kuomba msamaha wa kweli kwa matendo yake ya zamani.

(Methali: matendo yana nguvu kuliko maneno). Ndugu, kutoa mali kwa wale tuliokosana nao ni njia mwafaka kwa upatanisho. Kila mtu ana cha kutoa alichobarikiwa na Mungu. Unatoa ulichonacho, si usichonacho. Luka 19:8 … “Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini; na ikiwa nimemnyang’anya mtu kitu chochote kwa mashtaka ya uongo, namrudishia mara nne. Zakayo baada ya kutembelewa na Yesu anatoa mali ili kuleta amani. Sisi tuliozaliwa mara ya pili na kujazwa na Roho Mtakatifu, tunahitaji kutoa mali zetu ili kupata amani.

 Muda wako, kuwa wa kwanza kutafuta upatanisho,

toa kilicho kwenye uwezo wako.

3. Unyenyekevu – (mstari wa 3)

Unyenyekevu ni hali ya kujishusha/ kutokuwa na kiburi.

Tunamwona Yakobo akiinama mara saba kuonyesha unyenyekevu kwa Esau. Namba 7 Kibiblia ni ukamilisho wa kitu. Alijishusha kwa kaka yake. Yakobo anarudi baada ya miaka 20 ingawa alikuwa tajiri, ni kwa sababu ni nyumbani.

(Methali; Tembea popote ila nyumbani ni nyumbani)

Ndugu, kutoelewana kati ya pande mbili kunaweza kutokea maana binadamu si malaika, haijalishi kwa muda gani, mara ngapi, au umbali gani, tunachopaswa kujua ni kwamba ikiwa tunahitaji amani na ndugu zetu, unyenyekevu haukwepeki. Unyenyekevu ni muhimu kuliko nafasi zetu, vyeo, hadhi na umri. Unyenyekevu si kuongea taratibu, kutembea polepole au kutabasamu kila wakati, unyenyekevu ni kujishusha mbele ya wengine.

Filipi 2:8. “Naye alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtiifu hata mauti, naam, mauti ya msalaba.”

Ili kuwa na maridhiano ya Kimungu tunahitaji hatua 3 ambazo ni kuwa na mipango mkakati, kutoa baadhi ya mali zetu na unyenyekevu. Mungu ametupatanisha kwake kwa njia ya Kristo msalabani, tunaweza kupatana sisi kwa sisi, bila kuhesabu makosa yetu dhidi ya mwingine

Una mgogoro na mtu lakini hujui pa kuanzia, fuata hatua hizo na zitakusaidia na Mungu wa mbinguni mwenye upendo na huruma nyingi hatakuacha katika nia yako njema. Umejaribu kutafuta amani bila mafanikio, ukitafuta amani ndiyo unazalisha mengine. Hakuna maridhiano yasiyowezekana kwa Yesu.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.