top-news-1350×250-leaderboard-1

NCAA yang’ara Tuzo za ubora PRST 2024

Na Mwandishi wetu

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imeendelea kung’ara katika ulingo wa mawasiliano na uhusiano wa umma baada ya kushinda Tuzo ya Ubora ya Chama cha Maafisa Uhusiano Tanzania (PRST) kwa mwaka 2024 kupitia kampeni yake bunifu ya “Merry & Wild: Ngorongoro Awaits.” Kampeni hiyo, iliyolenga kuhamasisha utalii wa ndani wakati wa msimu wa mwisho wa mwaka, imeweka historia kwa kuwavutia watalii wa ndani kwa wingi zaidi ya wageni kutoka nje kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa NCAA.

Kwa kipindi cha kuanzia tarehe 4 Desemba 2024 hadi 4 Januari 2025, jumla ya watalii wa ndani 44,386 walitembelea Hifadhi ya Ngorongoro, ikilinganishwa na 35,837 kwa kipindi kama hicho mwaka uliopita (2023/24). Hii ni ongezeko la watalii 8,549, sawa na asilimia 24%, ongezeko ambalo linadhihirisha mafanikio makubwa ya kampeni hiyo ya kimkakati.

Kampeni hii ilijikita katika kuonyesha vivutio vya kipekee vya Ngorongoro kwa kutumia mbinu shirikishi, ubunifu wa kidijitali, na ushawishi wa mitandao ya kijamii kwa kushirikisha vijana, familia, na makundi maalum ya kijamii. Miongoni mwa makundi yaliyohamasika kupitia kampeni hiyo walitoka katika mikoa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Dodoma, Arusha, Singida, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Tabora, Tanga, Manyara na Zanzibar.

Mbali na mafanikio hayo ya kitaasisi, Kaimu Meneja wa Idara ya Uhusiano kwa Umma wa NCAA, Hamis Dambaya, ameibuka mshindi wa Tuzo ya Nyota wa Dhahabu wa Uhusiano wa Umma Tanzania 2024. Tuzo hii hutolewa kwa wataalamu wa Uhusiano wa Umma waliotoa mchango mkubwa kwa kuonesha ubora wa mikakati, ubunifu wa hali ya juu, na athari chanya katika jamii kupitia taaluma yao.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt.Elirehema Doriye,kaimu Meneja Uhusiano kwa Umma wa mamlaka hiyo ameishukuru bodi ya wakurugenzi na menejimenti kwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa za kuelimisha umma katika kuimarisha utalii wa ndani.

“Juhudi za pamoja katika kuhakikisha kuwa Ngorongoro inatumia mbinu zote kujitangaza zinatokana na uimara wa bodi yetu na menejimenti,uwezo wa kuwa miongoni mwa maafisa habari bora nchini Tanzania kwangu mimi ni faraja kwamba bodi na menejimenti inanilea vizuri”,alisema Dambaya.

Tuzo hizo za PRST zinalenga kutambua na kuenzi mafanikio ya mawasiliano ya kimkakati katika sekta ya umma na binafsi nchini Tanzania, na mwaka huu NCAA imeonesha mfano bora wa namna taasisi za umma zinavyoweza kutumia mawasiliano kwa ubunifu ili kufikia malengo ya maendeleo na kuhifadhi urithi wa taifa.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.