top-news-1350×250-leaderboard-1

Naibu Mufti: Kumwalika tajiri mwenzako si kama hujafuturisha, aipongeza TCB kugusa makundi yote

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

Naibu Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Hassan Chizenga ameipongeza Benki ya Biashara Tanzania(TCB) kwa kufuturisha makundi mbalimbali ikiwa ni moja ya ibada muhimu katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, huku akisema hata tajiri anastahili kualikwa.

Sheikh Chizenga aliyemwakilisha Mufti Mkuu wa Tanzania, ameyasema hayo wakati wa hafla ya futari maalum iliyoandaliwa na benki hiyo Machi 28, 2025 katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam ambapo ilijumuisha watu mbalimbali ikiwamo viongozi wa dini, watoto yatima kutoka vituo tofauti, wateja wao, wafanyakazi wa TCB, na Jumuiya ya Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi.

Naibu Mufti huyo amesema kuwa TCB imefanya jema kukaa na wateja wake na watu wengine kufuturu pamoja na kukiri kuwa hafla hiyo imekuwa tofauti na sehemu nyingine alizowahi kualikwa katika kipindi hiki.

“Mwaliko hata kama umewahi kujadiliwa katika mitandao, kumwalika tajiri mwenzako si kama hujafuturisha, utakuwa umefuturisha si binadamu? Lakini pale utakapomwalika tajiri halafu ukamwalika na mtu ambaye huna nasaba naye hata katika mizunguko yako ya kila siku. na huna namna ya kukutana naye, ukamwalika yatima, ukamwalika mtu wa chini. Nyinyi mmepatia sana na mmeenda mahali ambapo Mungu anapopataka”, ameeleza Naibu Mufti.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Adam Mihayo amesema dhamira ya benki hiyo ni kushirikiana na Serikali katika kujenga uchumi imara.

Amesema kwa kutambua unyeti wa baadhi ya sekta wamekuwa wakizigusa moja kwa moja ili kupunguza mzigo kwa serikali lakini pia ni sehemu ya kurudisha kwa jamii.

“TCB tunaamini kuwa benki sio tu taasisi ya fedha bali ni mshirika wa maendeleo ya jamii, tumekuwa mstari wa mbele katika kusaidia miradi yenye matokeo chanya kwa jamiia tukigusa sekta mbalimbali ikiwamo afya, elimu ,pia kusaidia taasisi za kidini katika miradi mbalimbali.

“Tumeendelea kutoa misaada kwa kuimarisha miundombinu katika elimu ikiweo kusaidia madawati katika baadhi ya shule lakini pia tumetembelea katika hospitali na kutoa misaada bila kusahau makundi yenye uhitaji.” amesema Mihayo.

Mihayo ameeleza kuwa ushiriki wao katika hafla kama hiyo ya kufuturisha, unaimarisha dhamira yao ya maendeleo jumuishi kwa kila mtu.

Ameongeza kuwa dhamira yao ni kuimarisha maendeleo jumuishi kwa jamii lakini pia kuendelea kutoa huduma bora kwa Watanzania huku akisisitiza matumizi ya huduma za kidigitali za benki hiyo.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.