Vatican. Safari ya maisha ya duniani ya Papa Francis ilihitimishwa saa 7:30 mchana (saa 8:30 mchana saa za Afrika Mashariki na Kati) leo Aprili 26, 2025 baada ya mwili wake kuzikwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, mjini Roma, Italia.
Ibada ya mazishi ilianza saa 7:00 mchana (saa 8:00 mchana) ikiongozwa na Camerlengo, mbele ya walioainishwa na taarifa husika ya ofisi ya maadhimisho ya liturujia za kipapa kwa uwepo wa ndugu wa marehemu Papa Francis.
Ibada hiyo imeadhimishwa faragha na Kardinali Kevin Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia ambaye pia Camerlengo (kiongozi mkuu wa shughuli za Kanisa wakati kunapotokea kwamba kiti cha Papa kiko wazi kwa sababu mbalimbali).

Papa Francis ambaye jina lake la ubatizo ni Jorge Mario Bergoglio aliyezaliwa Desemba 17, 1936 jijini Buenos Aires nchini Argentina alifariki dunia Aprili 21, akiwa katika makazi yake kwenye nyumba ya Mtakatifu Marta.
Watu 250,000 kutoka sehemu mbalimbali dunia walishiriki Misa Takatifu ya kumwombea Papa huyo iliyoongozwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali.
Baada ya misa maandamano yalianza kutoka kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, njiani watu walijipanga kutoa salamu za mwisho kwa Papa jeneza leye mwili wake lilipopelekwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu ambako amezikwa.

Kardinali Giovanni Battista Re, katika mahubiri alitambua uwepo wa wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali za dunia waliofika mjini Vatican ili kutoa heshima zao kwa Papa Francis.
Licha ya changamoto ya ugonjwa aliyokuwanayo Papa bado hakusita kutoa salamu na baraka kwa mji wa Roma na dunia kwa ujumla wakati wa sherehe ya Pasaka Aprili 20, 2025.
Baadaye aliteremka kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kusalimiana na mahuaji wa matumaini waliokuwa wamefurika uwanjani hapo.
Kardinali Giovanni Bastisti Re alimzungumzia Papa Francis akisema: “Alikuwa na utu imara katika uongozi wa Kanisa na alikuwa Papa kati ya watu mwenye moyo wazi kwa wote.”
Aliwapendelea maskini, wakimbizi na watu waliohamishwa. Huruma na furaha ni maneno mawili muhimu ambayo alikazia katika upapa wake na wakati huo umuhimu wa udugu ulienea. Papa Francis alipaza sauti kwa ajili ya amani bila kukoma na kusisitiza kujenga madaraja na siyo kuta.

Baada ya litania, Kardinali Baldassarre Reina, Makamu wa Papa jimbo la Roma, aliongoza maombi ya Kanisa la Roma.
Kisha mapatriaki wa kiorthodox, maaskofu wakuu na wakuu wa makanisa ya miji mikuu ya Mashariki ya Kikatoliki walioko kwenye kanuni walikuja mbele ya jeneza kwa ajili ya maombi ya Makanisa ya Mashariki wakati nyimbo zao za kiutamaduni zikiimbwa.
Kwa mujibu wa mtandao wa Vatican News, hata wakati wa mazishi ya Papa Francis, kama ilivyokuwa miaka 20 iliyopita wakati wa mazishi ya Papa Yohane Paulo II, upepo ulifungua na kufanya kurasa za Injili zionekane zikifunguka juu ya jeneza kugeuka. Haya yote yalitokea katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mara moja kabla na wakati wa kunyunyizwa maji na Kardinali Giovanni Battista Re na pia kufukiza uvumba.
Kutokana na hali hiyo, mazishi ya Papa Francis yalihitimishwa kukiwa na shangwe za umati wa watu wakisindikiza jeneza kurejeshwa Kanisa kuu kwa msafara wa makardinali, hadi kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, kabla ya kuanza msafara wa mazishi kwa mwendo wa taratibu kuelekea Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Mkuu, mahali alikozikwa faragha.

Bila kupita kwenye uwanja, jeneza likiwa kwenye kigari cha kipapa lilielekea kwenda kanisa Kuu la Mtakatifu Maria ambako waamini walionekana kusimama nyuma ya vizuizi vilivyowekwa barabarani kukiwa na joto la jua, anga la bluu na mawingu meupe.
Picha za juu za Vatican zilionyesha msururu wa rangi nyeusi ya mavazi yalivovaliwa na viongozi wa kitaifa, nyekundu ya mavazi yaliyovaliwa makardinali takriban 250, zambarau zilizovaliwa na maaskofu 400 na nyeupe iliyovaliwa na mapadri 4,000 waliokuwapo.
Miongoni mwa wakuu wa nchi waliokuwepo katika mazishi hayo ni rais wa Argentina, Ufaransa, Gabon, Ukraine, Ujerumani, Ufilipino na Poland, mawaziri wakuu wa Uingereza na New Zealand, na familia nyingi za kifalme, akiwemo mfalme na malkia wa Hispania.
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango aliyehudhuria misa hiyo amesema namna bora ya kumuenzi Papa Francis ni kudumisha amani pamoja na kujali maskini.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya makamu wa Rais imesema Dk Mpango amesema hayo baada ya kumalizika kwa misa
Amesema Papa alikuwa mnyenyekevu na mtu aliyefanya jitihada kubwa za utafutaji amani maeneo mbalimbali duniani na kuacha alama, ikiwamo tukio la kuwabusu miguu viongozi wa Sudan Kusini ili waweze kuachana na mapigano.
Amesema kati ya nyaraka za mwisho alizosaini Papa ni pamoja na barua aliyomwandikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumtakia heri ya siku njema ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Katika misa hiyo, Dk Mpango ameongozana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania Vatican, Balozi Hassan Mwameta na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme.
Trump, Zelenskyy wakutana
Mazishi ya Papa Francis yamewakutanisha Rais wa Marekani, Donald Trump na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy. Kuna wakati wawili hao waliketi pamoja wawili pekee ikielezwa walikuwa na mazungumzo yenye mafanikio.
Baadaye zilionekana picha zikimuonyesha Trump, Zelenskyy, Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer na Emmanuel Macron wa Ufaransa wakizungumza.
Imeelezwa viongozi wakuu kutoka mataifa zaidi ya 150 duniani wameshiriki misa hiyo.
Papa Francis aliyehudumu kwa miaka 12 alijikita kuwatetea maskini na waliotengwa, huku akizitaka nchi tajiri kuwasaidia wahamiaji na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Akiwa na sifa ya unyenyekevu, anatarajiwa kuzikwa akiwa amebeba msimamo huo kukiwa na mabadiliko aliyoyafanya katika ibada za mazishi ya mapapa.
Katika wosia wa maisha ya kiroho, aliouandika Juni 29, 2022 Papa Francis aliomba kaburi lake liwekwe kwenye kikanisa cha Bikira Maria Afya ya Warumi.
Pia alitaka kaburi lake lichimbwe ardhini, rahisi bila mapambo maalumu bali libaki likiwa na maandishi ya pekee “Franciscus.”
Italia ilifunga anga la juu la Jiji la Vatican City na kupeleka majeshi ya ziada, yakiwamo makombora ya kujihami na ndege na boti za doria.
Baada ya maziko ya Papa Francis makardinali watakuwa na mkutano maalumu wa faragha kuchagua Papa mpya.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.
Crédito: Link de origem