Unguja. Wakati mwili wa Sheikh Jabir Haidar Jabir ukiokotwa ukiwa umetelekezwa, polisi wamesema haujakutwa na majeraha yoyote huku mazingira ulikokutwa hayakuonesha dalili zozote za vurugu, hivyo inawezekana alipata madhara sehemu nyingine na kupelekwa katika eneo hilo.
Mwili wa Sheikh Jabir uliokotwa kando mwa barabara usiku wa kuamkia leo Mei 28, 2025 eneo la Kizimbani Bumbwisudi Mkoa wa Mjini Magharibi.
Kabla ya taarifa ya Polisi, kulikuwana na picha mnato zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonyesha sheikh huyo akiwa amelala chini kama mtu asiyejitambua.
Akizungumza leo Jumatano Mei 28, 2025 na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Richard Mchomvu amesema jana saa 5:00 usiku, Kituo cha Polisi Bububu kilipokea taarifa ya kuokotwa kwa mwili wa mwanaume maeneo ya Kizimbani.
Amesema baada ya kupata taarifa hiyo, Kaimu Mkuu wa upelelezi Wilaya ya Magharibi A, alifika katika eneo la tukio na kuuchukua mwili huo.
“Kaimu wa upelelezi alifika eneo la tukio na kufanya upelelezi wa awali na alipata kitambulisho kilichomtambulisha kwa jina la Jabir Haidari Jabir na aliuangalia mwili haukuwa na jeraha lolote,” amesema Mchomvu.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Richard Thadei Mchomvu akitoa taarifa kuhusu kuokotwa kwa mwili wa Sheikh Jabir Haidari Jabir leo Jumatano Mei 28, 2025 ofisini kwake Madema.
Kwa mujibu wa Kamanda Mchomvu, mazingira ulikokutwa mwili huo hayakuonesha dalili zozote za vurugu, hivyo ieleweke kuwa pengine alipata madhara sehemu moja na kupelekwa eneo hilo.
Amesema, mwili huo ulichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Amesema Jeshi la Polisi lilibaini kuwa marehemu alikuwa mkazi wa Fuoni na walikuwa wakiishi wawili yeye na kijana aliyekuwa akimsaidia kazi.
Mchomvu amesema, walipogundua kuwa ni mkazi wa Fuoni walifanya uchunguzi wa awali na walitambua alikuwa anaishi na kijana wa kazia, hata hivyo hakumtaja jina.
Amesema jana Mei 27, 2025 saa 12:00 jioni sheikh huyo alitembelewa na kijana ambaye alionesha kufahamiana naye na walikaa kwa muda sebuleni wakizungumza wakati huo kijana wake wa kazi alikuwa ndani.
“Jabir alizungumza na kijana huyo kama nusu saa wakatokea watu wengine watano ambao walijiunga pamoja na ilipofika saa 2:30 usiku waliondoka naye, kabla ya kutoka hausiboi alimuuliza anakokwenda, akamjibu kuwa atamjuza baadaye hivyo haikufahamika anakwenda wapi hadi mwili wake ulipookotwa,” amesema.
Hivyo, Kamanda amesema mpaka sasa chanzo cha kifo chake bad hakijajulikana.
“Na bado haijafahamika watu alioondoka nao wako wapi na sisi bado Jeshi la Polisi linapambana kufuatilia tukio hilo,” amesema kamanda huyo.
Amesema jeshi hilo linaendelea kufanya upelelezi ili kubaini alioondoka nao walienda wapi, alikufaje na kwa nini mwili wake ulikutwa maeneo hayo.
“Nataka kuwahakikishia wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kwa hatua ambayo tumeifikia tutawajua walioondoka naye na kitu kilichotokea, najua kuna minog’ono mingi mtaani ila hayo ndio yaliyopo mwili haukukutwa na jeraha lolote,” amesema Mchomvu.
Naye mtoto wa kaka wa marehemu, Mudthir Kassim Haidar amesema wamepokea taarifa hizo kwa masikitiko kwani jana aliondoka kwao na kwenda kwake akiwa mzima licha ya kwamba alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu na moyo lakini jana alikuwa salama.
“Jana baada ya kupata taarifa zinadai ameuawa kwa kupigwa lakini tunachokijua alitoka nyumbani akiwa mzima na amewasiliana na watu akiwa salama. Suala la kuwa ameuawa tunasubiri na kuwaachia jukumu hilo Polisi kama ameuawa au imekuwaje, wao ndio watatoa taarifa,” amesema.
Crédito: Link de origem