top-news-1350×250-leaderboard-1

Mwalimu kortini akidaiwa kughushi cheti cha ndoa, kuisababishia NHIF hasara ya Sh13 milioni

Dar es Salaam. Mwalimu wa Shule ya Msingi Mtongani, Consolata Kyaruzi (40), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kughushi cheti cha ndoa na kuisababishia hasara Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Kyaruzi amefikishwa mahakamani hapo Ijumaa, Aprili 25, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi na wakili wa Serikali, Fatma Waziri.

Mshtakiwa amesomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya.

Akimsomea mashtaka hayo, Waziri amedai shtaka la kwanza ni kughushi cheti cha ndoa, tukio analodaiwa kulitenda Juni 17, 2021 jijini Dar es Salaam katika ofisi za NHIF.

Mshtakiwa Consolata Kyaruzi (aliyejifunika uso na mtandio) akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa kesi ya kughushi cheti cha ndoa.

Inadaiwa siku ya tukio, kwa nia ya kudanganya, Kyaruzi alitengeneza cheti cha ndoa na kuonyesha ameolewa na Hermenegild Moshi, kitu ambacho alijua kuwa ni uongo.

Shtaka la pili ni kujipatia usajili kinyume cha sheria, tukio analodaiwa kulitenda Julai 19, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, ambapo mshtakiwa alijipatia usajili wa Hermenegild Damas Moshi kutoka NHIF kwa kujitambulisha kuwa Moshi ni mume wake na anastahili kupata huduma ya bima ya NHIF.

Iliendelea kudaiwa katika shtaka la tatu kuwa aliwasilisha nyaraka za uongo ofisi za NHIF zilizopo Kinondoni, tukio analodaiwa kulitenda Julai 19, 2021.

Kyaruzi anadaiwa siku ya tukio, kwa nia ovu, aliwasilisha shahada ya ndoa kwa mtumishi wa NHIF aitwaye Gwelino Wissa, wakati akijua kuwa nyaraka hizo ni za uongo.

Shtaka la nne ni kuisababishia NHIF hasara ya Sh13 milioni. Mshtakiwa anadaiwa kati ya Januari 2021 na Desemba 2022 kwa kutumia kadi hiyo ya uanachama wa NHIF, na kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh13,486,265.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, hivyo wakaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea hoja za awali (PH).

Hakimu Lyamuya alitoa masharti ya dhamana kwa mshtakiwa aambayo ni kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho pamoja na kitambulisho cha Taifa (Nida).

Pia, wadhamini hao wanatakiwa kusaini bondi ya Sh10 milioni. Mshtakiwa alikamilisha masharti ya dhamana na yupo nje.  Kesi imeahirishwa hadi Mei 25, 2025 kwa ajili ya Serikali kumsomea hoja za awali mshtakiwa.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.