Jumamosi iliyopita tulisherehekea miaka 61 ya Muungano wetu huu adhimu na wa kipekee. Kwa hakika, Muungano wetu umeimarika, umepevuka, na umekomaa kiasi kwamba sasa tuko tayari kuchukua hatua ya pili ya kuudumisha kwa kuungana kuwa na serikali moja, nchi moja, chini ya Rais mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hili Rais Samia Suluhu Hassan ana uwezo kamili wa kulitekeleza.
Muungano huu ulipoasisiwa, lengo lilikuwa kuunda taifa moja chini ya Rais mmoja na Serikali moja.
Baba wa Taifa la Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, alikubali mapendekezo hayo kwa kusema, “Wewe Rais, mimi Makamu.”
Hata hivyo, Mwalimu Julius Nyerere aliona ni mapema mno, akihofia kwamba ingeonekana kama Tanganyika imeimeza Zanzibar. Hivyo, alishauri twende hatua kwa hatua kwa kuanzisha mfumo wa Serikali mbili.
Mwaka 1977, baada ya vyama vya TANU na ASP kuungana na kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM), bado tuliendelea na mfumo wa Serikali mbili, tukilenga hatimaye kuwa na Serikali moja.
Ni muhimu kukumbuka kuwa Muungano huu, uliotokana na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, ulifanikishwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu tu ya mazungumzo.
Ikiwa jambo kubwa kama hili liliwezekana kwa muda mfupi, basi kama Rais Samia ataamua kwa dhamira ya dhati kufanya mabadiliko madogo ya Katiba yetu ili kuwezesha uchaguzi huru na wa haki Oktoba mwaka huu, muda uliopo unatosha kabisa kwa sababu bado tunayo miezi sita kabla ya uchaguzi mkuu.
Katika suala la kero za Muungano, Rais Samia amefanya kazi kubwa ya kupongezwa.
Katika kipindi cha miaka 55 ya Muungano, marais watano waliomtangulia waliweza kutatua jumla ya kero saba tu kati ya ishirini na tano zilizokuwepo.
Rais Samia alipokabidhiwa uongozi Machi 17, 2021, alikuta zikiwa zimebaki kero 18. Katika kipindi cha miaka mitatu pekee, amefanikia kuzitatua kero 15, wastani wa kero tano kwa mwaka na sasa zimebaki kero tatu tu.
Kasi hii ya kutatua kero za Muungano ndiyo inayothibitisha kuwa sasa Muungano wetu umepevuka na uko tayari kwa hatua mpya ya Serikali Moja.
Ikiwa Rais Samia ataamua kuongoza mchakato wa kufanya mabadiliko madogo ya Katiba kabla ya Uchaguzi Mkuu, anaweza kabisa kulitekeleza jambo hili ndani ya uwezo wake wa kikatiba.
Katika historia ya Muungano wetu, wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume, ilikuwa marufuku hata kuhoji Muungano.
Akiwa Makamu wa Rais, Samia kwa mara ya kwanza viongozi wa juu wa Serikali waliruhusu wananchi kujadili Muungano kwa uhuru. Hili linaonesha wazi dhamira yake ya kweli katika kuimarisha Muungano wetu.
Kwa msingi huu, kwa haki na kwa halali kabisa, Rais Samia anastahili kupewa nishani ya juu ya Muungano na tumpeni maua yake sasa.
Kuhusu mabadiliko ya Katiba
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Ibara ya 98, inatoa utaratibu wa kufanya mabadiliko ya Katiba: Ibara ya 98(1)(a) Mabadiliko yanayohusu Bara pekee yanahitaji kuungwa mkono kwa kura za theluthi mbili ya wabunge wote.
Ibara ya 98(1)(b): Mabadiliko yanayohusu Zanzibar yanahitaji kuungwa mkono kwa kura za theluthi mbili ya wabunge wa Bara na theluthi mbili ya wabunge wa Zanzibar.
Mchakato wa mabadiliko hayo unachukua si zaidi ya siku 30:
Mosi, Serikali inawasilisha ombi kwa Rais kwa hati ya dharura.
Pili, Rais akiridhia, ndani ya siku 7 tangazo linachapishwa kwenye Gazeti la Serikali na Muswada wa Mabadiliko unapelekwa Bungeni. Tatu, Muswada unasomwa mara ya kwanza, unatangazwa kwa siku 14 kwa ajili ya kukusanya maoni na nne, Muswada huo unachambuliwa na Kamati za Bunge kabla ya kusomwa mara ya pili na ya tatu na kupitishwa.
Kwa kuwa bado tunayo miezi sita kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, ikiwa kuna dhamira ya dhati ya kufanya uchaguzi huru na wa haki, muda unatosha kabisa kutekeleza mabadiliko haya.
Tunaahidi kuendelea kuulinda Muungano huu kwa gharama yoyote ile.
Mungu Ibariki Tanzania! Mungu ubariki Muungano wetu adhimu na adimu.
Crédito: Link de origem