Dar es Salaam. Chama cha Demokarasia na Maendeleo (Chadema) kinakabiliwa na mtihani mwingine wa kurudi katika uchaguzi kujaza nafasi zinazoachwa wazi na viongozi wake wanaokihama chama hicho.
Viongozi hao hadi sasa wapo katika ngazi za kanda, mikoa, wilaya, majimbo na kata, baadhi wakiwa katika kundi linalounda G55, la waliokuwa wagom,bea ubunge na udiwani linalopingana na uamuzi wa chama hicho kutoshiriki uchaguzi, wakati walikwishafanya maandalizi.
Aida, viongozi hao, wanajumuisha waliokuwa wajumbe wa sekretarieti ya Chadema katika uongozi uliomaliza muda wake chini ya uenyekiti wa Freeman Mbowe.
Miongozi wanaoachia ngazi na kuopndoka, wamo wajumbe wa kamati kuu, baraza kuu na mkutano mkuu pamoja na mabaraza ya mikoa na wilaya. Pia wamo waliokuwa kwenye nafasi hizo kwenye uongozi uliomaliza muda wake.
Licha ya ajenda iliyoko mezani ya uamuzi wa kutoshiriki uchaguza kutokana na kampeni yake ya kupigania mabadiliko ya sheria na mifumo ya uchaguzi, sekeseke hilo linakolezwa na mpasuko uliotokana na uchaguzi wa ndani ya chama.
Uchaguzi huo uliomwingiza Tundu Lissu madarakani na kumtupa nje Freeman Mbowe aliyeongoza chama hicho kwa miaka 20, uliacha mpasuko mkubwa na kinachoonekana ni kuwa wengi wa wanaohama ni waliokuwa wanamuunga mkono Mbowe.
Waliofungua mlango wa hamahama ni waliokuwa wajumbe wa sekretarieti – manaibu katibu mkuu, Benson Kigaila (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar), aliyekuwa mkurugenzi wa itifaki na mambo ya nje, John Mrema, aliyekuwa katibu mkuu mstaafu wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Catherine Ruge na katibu wa zamani wa sekretarieti, Julius Mwita.
Mwita na Ruge waliendelea kuwa wajumbe wa sekretarieti katika uongozi mpya hadi walipoamua kukaa kando, wakiungana na wenzao wanaotegemewa kujiunga na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) wakati wowote.
Ukiacha wale waliokuwa kwenye uongozo uliopita viongozi waliojiuzulu nafasi zao waliokwisha kuhama hadi leo Alhamisi, Mei 15, 2025 ni pamoja na Henry Kilewo, aliyekuwa mwenyekiti wa mkoa wa kichama wa Kinondoni, Patrick Assenga, mhazini wa Kanda Pwani na Emma Kimambo, mhazini Kanda ya Kaskazini.
Wengine Gervas Mgonja, mwenyekiti wa Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema, katibu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Khadija Mwago, Mwenyekiti wa Bawacha Wilaya ya Mbagala.
Wamo pia Devotha Minja, mwenyekiti wa Kanda ya Kati, Helman Kiloloma, mwenyekiti wa Mkoa wa Temeke, Katibu wa Wilaya ya Segerea, Asha Abubakari, Katibu wa Bawacha Kanda ya Kaskazini, Rachael Sadick na Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Kilimanjaro, Grace Kiwelu.
Vumbi hilo halijawaacha Esther Fulano, aliyekuwa Katibu wa Bawacha Kanda ya Victoria, Doris Mpatili, Mwenyekiti Kamati ya Mafunzo Kanda ya Victoria, Hanifa Chiwili – Katibu wa Kamati ya Maadili ya Kanda ya Pwani, Mwenyekiti wa Mkoa wa Pwani Kusini na Mussa Katambi na aliyekuwa makamu mwenyekiti wa kanda ya magharibi.
Wengine ni Mwenyekiti wa Bawacha wilaya ya Kilombero, Suzan Kiwanga, Mwenyekiti wa Bavicha Wilaya ya Kilosa, David Chuduo, aliyekuwa mwenyeliti wa Bawacha wilaya ya Kilosa, Sheila Mluba na mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Tabora, James Kabepele.
Wamo pia Mwenyekiti wa wilaya ya Kishapu, Boniface Masanja, Katibu wa Bawacha mkoa wa Shinyanga, Furahisha Wambura, katibu wa jimbo la Msalala, Yussuf Paulo na Hamza Kinyema aliyekuwa Mwenyekiti Temeke.
Hali ikiwa hivyo, Msemaji wa G55, Mrema amesema: “Kuna kundi kubwa linaendelea kuachia ngazi, hawa ni wachache tu lakini kama tulivyosema ni wengi sana.”
Wakati Mrema akieleza hayo, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Dk Rugemeleza Nshala alipotafutwa na Mwananchi kujua utaratibu wa kujaza nafasi za viongozi wanaohama, ameanza kwa kusema “kwanza chama bado ni imara na hakiwezi kutetereka.”
“Tutakuja na mpango mahsusi wa kujaza nafasi hizo lakini lazima kufahamu walioondoka si wengi, wamekubali kuondoka na kwenda kutumika,” amesema Dk Nshala.
Dk Nshala amesema wakija na utaratibu wa kuziba nafasi hizo, watatangaza kwa umma na amewataka wananchama na wapenzi wa chama hicho kuwa watulivu katika kipindi hiki.
Akiangalia hali hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema Chadema inapitia mtihani mzito wakati baadhi ya viongozi ngazi mbalimbali wakihama huku mwenyekiti wake, Tundu Lissu akikabiliwa na kesi ngumu ya uhaini.
“Vilevile viongozi wengine wanaendelea na kampeni ya No reforms no election wanasumbuliwa zaidi, mara wakamatwe na polisi, wapigwe mabomu…ni kipindi ambacho chama kinapitia misukosuko mingi,” amesema.
Dk Mbunda amesema ni kipindi ambacho alitamani wanachama wasiendelee kubomoka kwa sababu wanaongeza maumivu kwa chama, ingawa hiyo ni hali ya kawaida katika siasa na inaweza kutokea kama hamna maelewano mazuri.
“Kila anayeondoka anasema alikuwa kambi ya Freeman Mbowe, hawatujali, tunatengwa kwa hiyo kuna ahida ya hizi kambi mbili – Mbowe na Tundu Lissu na upande mmoja umekosa uvumilivu. Na inawezekana huo ni mwanzo, mwisho wa siku inaweza kutokea Mbowe mwenyewe akahama,” amesema.
Dk Mbunda alisema ugumu uliopo ni kuwa kila mmoja anayeondoka hasemi anaenda jukwaa gani? Ni jambo linaloonekana ni mkakati unasukwa na mtu wa mwisho atakuja kusema wanahama wanaenda wapi?
“Kipindi kama hiki kwa chama, unaweza kusema viongozi wao wanaingizwa kwenye tanuri la moto ili tuone wanatoka kama dhahabu au ni viongozi wasiofaa, kwa sababu bado wafuasi wanaowaunga mkono ni wengi,” alisema.
Dk Mbunda amesema hata akifuatilia kwenye mitandao ya kijamii, wengi wanaohama ukisoma maoni ya watu wanasemwa vibaya na inatoa picha wanaohama si kwamba wana watu, inawezekana wanaondoka kwa ushawishi viongozi.
“Huwezi kusema wanaondoka na watu, hakuna aliyewahi kusimama na kusema anaondoka na watu 1,000, viongozi wanahama lakini hatujui huko chini wana watu kiasi gani. Chama kipo kwenye mtihani wa kujenga imani kwa wanachama wake na wananchi kwa ujumla,” amesema.
Alisema ujumbe unaopatikana ni chama kinaenda kufa na ilikuwa makosa kuchaguliwa kwa Lissu na John Heche lakini ukiangalia ajenda yao ya No reforms no election ni hoja yenye nguvu na inamsingi.
“Mtu yeyote mwenye akili timamu na aangalii mambo kwa misingi ya mahaba ataiunga mkono, na ukiangalia uchaguzi pekee ambao vyama vya upinzani viliingia na kufurahia ni mwaka 2015 na ulitoa wabunge wengi,” alisema Dk Mbunda.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa (UDSM), Dk Matrona Kabyemela alisema anadhani kwa kipindi hiki haya hayana budi kutokea kwa sababu hizo ndizo siasa.
“Maana kwenye siasa kuna maslahi mapana na ya mtu binafsi na inategemea unayafikiaje!. Wale wanao hama ni haki yao ya msingi kama wanaona chama hakitawafikisha wanapopataka kwa sasa ama kwa maslahi yao au ya jamii,” amesema.
Kulingana na Dk Matrona amesema chama hicho kinapitia pagumu baada ya mwenyekiti wake kuwekwa kizuizini na inaweza ikawakatisha tamaa baadhi ya wafuasi na viongozi ambao hawajakomaa
“Nini kifanyike chama ni kujitafakari namna kinavyosaka viongozi, maana kazi mojawapo ya chama ni kuibua viongozi. Mara nyingi nimeona Chadema ikiwa na wafuasi wengi ambao hawako pamoja kutokea chini kwahiyo ni rahisi kuwapoteza,” amesema.
Akitolea mfano Dk Matrona alitolea mfano CCM wana kitu kinaitwa nyumba kumi, hii ni mbinu kubwa ya kuwaweka pamoja wafuasi, kuwaratibu na kuwatunza na kuwasoma nia yao na utayari wao wa kulinda maslahi ya chama
“Mtu akija kuchaguliwa lazima adhibitishwe na wajumbe ambao wanakuwa wanamjua. Kufanya hivyo inawapunguzia kuwa na viongozi wasio wazuri, wenye kulalamika lalamika,” amesema.
Dk Matrona amesema kwakuwa democrasia ni mchakato, Chadema waendelee kutengeneza mtandao thabiti utakao fika mpaka vijijini na huko ndo kuna viongozi ambao wanaweza kusimama na chama katika majira yoyote
“Viongozi kujiona yatima nadhani wakati mwingine ni mtazamo au namna uongozi mpya unavyo hakikisha unawaleta pamoja wafuasi wake nadhani muda ulikuwa mfupi kwa mwenyekiti kuondoa hizo tofauti kabla hajawekwa kuzuizini,” amesema.
Crédito: Link de origem