top-news-1350×250-leaderboard-1

Mtihani kidato cha sita, ualimu kuanza kesho, Necta yatoa onyo

Dar es Salaam. Watahiniwa 134,390 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha sita kuanzia kesho Jumatatu, Mei 5 hadi Mei 26, 2025.

Pia mtihani wa ualimu ngazi ya stashahada Tanzania Bara na Zanzibar utaanza Mei 5 hadi Mei 19, 2025.

Kutokana na mitihani hiyo, Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetoa wito kwa wadau mbalimbali wakiwemo wananchi kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na miongozi yote, ili kuwezesha mitihani hiyo kufanyika kwa ufanisi.

Aida, limewataka watahiniwa kuepuka njia zote zisizo sahihi katika kufanya mitihani hiyo.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Mei 4, 2025 na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohamed alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Dk Mohamed amesema mtihani wa kidato cha sita utafanyika katika shule za sekondari 982 na vituo vya watahaniwa wa kujitegemea 245 huku ule wa ualimu ukifanyika katika vyuo 68.

Kuhusu usajili wa watahiniwa, Dk Mohamed amesema kati ya watahiniwa wa shule 126,957 waliosajiliwa, wavulana ni 64, 581 sawa na asilimia 50,87 na wasichana ni 62,376 sawa na asilimia 49.13.

“Watahaniwa wenye mahitaji maalumu ni 453 ambapo kati yao wenye uoni hafifu ni 300, wasioona 16, wenye uziwi 58, wenye ulemavu wa akili wanne na wenye ulemavu wa viungo vya mwili 75,” amesema Dk Mohamed.

Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea 7,433 waliosajiliwa, wavulana ni 4,782 sawa na asilimia 64.33 na wasichana ni 2,651 sawa na asilimia 35.67.

“Mwaka 2024 idadi ya watahiniwa wa shule wa kujitegemea waliosajiliwa walikuwa 113,536, hivyo kuna ongezeko la watahiniwa 20,854 (asilimia 18.37) kwa mwaka 2025, ukilinganisha na mwaka 2024,” amesema Dk Mohamed.

Kati ya watahiniwa hao wa kujitegemea, wenye mahitaji maalumu wako 151 ambapo kati yao wenye uoni hafifu ni 142 na wasioona ni tisa.

Kwa upande wa ualimu, watahiniwa 10,895 wamesajiliwa kufanya mtihani huo na kati yao 3,100 ni wa ngazi ya stashahada na 7,795 ngazi ya cheti.

Katibu huyo amesema mwaka 2024 idadi ya watahiniwa wa ualimu waliosajiliwa walikuwa 11,435, hivyo kuna upungufu wa jumla ya watahiniwa 540 (4.72) kwa mwaka 2025 ukilinganisha na mwaka 2024.

Dk Mohamed amesema maandalizi yamekamilika, ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa mitihani husika, vitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mitihani hiyo katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Vilevile, amezitaka kamati za mitihani, kuimarisha usalama wa vituo na wasimamizi walioteuliwa wafanye kazi yao kwa weledi na uadilfu.

Amesema anaamini watahiniwa wameandaliwa vizuri katika miaka miwili hivyo ni matumaini yake kila mmoja atafanya mitihani hiyo kwa kuzingatia kanuni zilizopo.

Kwa jamii ameiomba kutoa ushirikiano unaotakiwa katika kuhakikisha mitihani hiyo inafanyika kwa amani na utulivu.

“Wananchi wanaombwa kuhakikisha hakuna mtu yoyote asiyehusika na mitihani anaingia kwenye maeneo ya shule na vyuo katika kipindi chote cha mitihani ili kusaidia mitihani hiyo kufanyika kwa amani na usalama,” amesema katibu huyo.

Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti wadau wa elimu kuhusu mitihani hiyo wamesema wana imani walimu watakuwa wamewaandaa vema watahiniwa hao.

Ofisa Mtendaji Mkuu Taasisi ya ubunifu katika elimu Tanzania (EIT), Benjamin Nkonya amesema kama wametekeleza wajibu huo inavyotakiwa ni wazi hata suala la udanganyifu halitakuwepo.

Nkonya ambaye pia alikuwa mjumbe wa kupitia sera upya ya elimu, amesema miaka saba ijayo suala la udanganyifu ambalo Necta imekuwa ikionya kila wakati, litakwisha kwa kuwa kutokana na sera mpya ya elimu ya mafunzo ya amali ni wazi hata katika soko la ajira wataangalia zaidi ujuzi alionao mhusika.

“Udanganyifu wa mitihani umekuwepo kutokana na wanafunzi wengi walisoma ili wapate cheti kitakachowawezesha kupata ajira, lakini kwa sera mpya ya elimu, sasa mwanafunzi ataangaliwa zaidi ujuzi alio nao na sio cheti,” amesema Nkonya.

Mtendaji huyo ameshauri kuwa kila kada inapaswa kujumuisha somo la ujasiriamali linalohusiana moja kwa moja na taaluma husika, ili mhitimu aweze kujitegemea hata kabla ya kuajiriwa.

Kwa mfano, kwa upande wa walimu amesema inapaswa kufundishwa namna ya kuanzisha shule binafsi ili kuondokana na mtazamo wa kufundisha darasani pekee na kuwachapa watoto. Hii itawasaidia walimu si tu kujiajiri, bali pia kuajiri wenzao na kuongeza fursa za ajira katika sekta ya elimu.

Mchambuzi na mtafiti wa masuala ya elimu, Muhanyi Nkoronko, amesema kupungua kwa idadi ya walimu wanaofanya mtihani wa kuajiriwa ikilinganishwa na mwaka 2024, kunachangiwa na sababu mbalimbali, ikiwemo masilahi duni wanayopewa walimu wanapoingia kazini.

Ameeleza kuwa sababu nyingine ni urasimu uliopo sasa katika mchakato wa kupata ajira za ualimu, hali inayowakatisha tamaa wahitimu wengi.

“Siku hizi, ili upate ajira ya ualimu ni lazima upitie hatua ya usaili, tofauti na zamani ambapo mtu alipotoka chuoni alikuwa anaajiriwa moja kwa moja. Hali imekuwa ngumu, hivyo baadhi ya watu wanaamua kusomea fani nyingine zisizo na vikwazo vingi,” amesema Nkoronko.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.