top-news-1350×250-leaderboard-1

Mo Dewji anavyoleta mageuzi kwenye jamii

Dar es Salaam. Sahau kujumuishwa mara nyingi na Jarida la Forbes katika orodha ya mabilionea wa Kiafrika, tajiri wa Kitanzania, Mohamed Gullam Dewji, maarufu MO ana sura nyingine katika jamii ya Kitanzania.

Ushiriki huu ni kando ya ule wa kwenye michezo ambao watu wengi humfahamu kwa ufadhili na kujitoa kwake.

MO amekuwa akitumia utajiri wake kubadilisha maisha ya Watanzania wengi katika nyanja za kijamii hususan katika uwekezaji wake.

Mmiliki wa kampuni ya Dangote kutoka Nigeria, Aliko Dangote, ameshika nafasi ya kwanza katika orodha hiyo ukiwa ni mwaka wa 14 mfululizo akiwa na utajiri unaokadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni 23.9, ikilinganishwa na Dola za Marekani bilioni 13.9 mwaka jana.

Katika orodha hiyo mpya ya 2025 iliyotolewa na Forbes Machi 29, 2025, MO anashika nafasi ya 12, akiwa na  utajiri wenye thamani halisi ya mali ya Dola za Marekani bilioni 2.2 akipanda kwa Dola za Marekani milioni 400 ikilinganishwa na Dola za Marekani bilioni 1.8 mwaka jana.

Raia wa Afrika Kusini, Johann Rupert, anashika  nafasi ya pili akiwa na utajiri wa Dola za Marekani bilioni 14, sawa na ongezeko la asilimia 39.

Anafuatiwa na mfanyabiashara wa Afrika Kusini, Nicky Oppenheimer na familia yake, wanaokamata nafasi ya tatu kwa Dola za Marekani bilioni 10.4.

Orodha ya mabilionea wengine wa Afrika na thamani ya utajiri wao kwenye mabano ni: Nassef Sawiris kutoka Misri (Dola 9.6 bilioni), Mike Adenuga kutoka Nigeria (Dola 6.8 bilioni), Abdulsamad Rabiu wa Nigeria (Dola 5.1 bilioni), Naguib Sawiris kutoka Misri (Dola5 bilioni), na Koos Bekker kutoka Afrika Kusini (Dola3.4 bilioni).

Pia wamo Mohamed Mansour kutoka Misri (Dola 3.4 bilioni), Patrice Motsepe wa Afrika Kusini na Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) (Dola 3 bilioni), Issaad Rebrab kutoka Algeria na familia yake (Dola3 bilioni), Mohamed Dewji wa Tanzania (Dola 2.2 bilioni), Michael Le Roux wa Afrika Kusini (Dola2.2 bilioni) na Othman Benjelloun na familia yake kutoka Morocco (Dola1.6 bilioni).

“Afrika Kusini imeweza kutoa idadi kubwa ya mabilionea mwaka huu, wako saba ikifuatiwa na wanne kutoka Nigeria na wanne kutoka Misri. Katika orodha hii pia wamo mabilionea watatu kutoka Morocco, mmoja kutoka Algeria (Issaad Rebrab), mmoja kutoka Tanzania (Mohamed Dewji), na mmoja kutoka Zimbabwe (Strive Masiyiwa),” inasema sehemu ya taarifa ya Forbes.

Mohamed Dewji, Mkurugenzi Mtendaji wa Mohamed Enterprises Tanzania Limited (METL), amekuwa akitumia sehemu ya utajiri wake kuwawezesha Watanzania, hasa kupitia ajira anazozalisha.

METL, iliyoanzishwa na baba yake MO miaka ya 1970, ni moja ya kampuni kubwa Tanzania, na Dewji ameitumia kufanikisha dhamira yake ya kuboresha maisha ya wananchi wa kawaida.

Mtazamo wake mkubwa umekuwa kufanya mabadiliko katika sekta zisizopewa kipaumbele, hasa kilimo, ambapo ameelekeza nguvu zake katika kufufua mashamba ya mkonge yaliyotelekezwa na kuzalisha ajira na fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi.

Uanzishaji wa Mo Cola umewawezesha Watanzania kunaojihusisha na biashara ndogo ndogo kupata fursa za kiuchumi huku akichagiza mapambano ya kibiashara na kampuni kubwa za vinywaji baridi duniani.

“Mtazamo huu umeisaidia METL kuwa mwajiri wa pili mkubwa Tanzania, baada ya Serikali, ikiwa imeajiri wafanyakazi 40,000 katika biashara zake 126,” MO ameliambia Mwananchi katika mahojiano maalumu.

Aliongeza kuwa kampuni yake inakusudia kuajiri watu 100,000, akibainisha kuwa ajira zinazozalishwa na maisha yaliyoguswa yamekuwa na athari kubwa kwake.

Katika sekta ya huduma za kijamii na misaada wa kibinadamu, Dewji kupitia Mohamed Dewji Foundation (MDF) imefanya mabadiliko makubwa katika upatikanaji wa maji safi na salama nchini Tanzania.

Kwa kushirikiana na Wizara ya Maji, MDF imechimba visima katika vijiji mbalimbali, na kuboresha upatikanaji wa maji na salama kwa zaidi ya watu 11,350.

Mwaka 2023 pekee, taasisi hiyo ilichimba visima 18 na kukarabati mingine vinne, hivyo kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa jamii za vijijini unakuwa endelevu.

MDF inatarajia kuchimba visima 50 zaidi na kukarabati vingine 50 na kunufaisha Watanzania 15,000 zaidi.

Kama Mbunge wa Singida kuanzia 2005 hadi 2015, MO aliboresha upatikanaji wa maji ambapo asilimia ya wakazi waliopata maji safi iliongezeka kutoka asilimia 27-28 hadi asilimia 86-88.

MDF imejikita pia katika utoaji wa huduma za afya, hasa kupitia kambi za matibabu ya macho ambazo zimesaidia kurejesha uwezo wao wa kuona.

Mwaka 2024, taasisi hiyo ilifanya upasuaji wa mtoto wa jicho, uchunguzi wa macho, mgawo wa miwani na dawa, ikiwasaidia maelfu ya wananchi kurejesha uwezo wa kuona, hivyo kuimarisha uhuru wao wa kiuchumi.

MDF inakabiliana na changamoto za mgongo wazi na kichwa kikubwa (spina bifida and hydrocephalus), hali zinazoweza kusababisha ulemavu mkubwa au kifo ikiwa hazitatibiwa.

Mwaka jana, taasisi hiyo ilifadhili upasuaji na matibabu ya watoto walioathirika hatua iliyobadilisha maisha yao.

“Hii ni hatua iliyobadilisha mchezo mzima. Tunawaokoa watu ambao vinginevyo wangeweza kupoteza maisha au kuwa na ulemavu wa kudumu. Dhamira yangu ni kuonyesha kwamba hatua maalumu, zilizofadhiliwa vizuri, zinaweza kubadili jamii nzima kwa muda mfupi,” amesema MO.

Mnamo mwaka 2016, Dewji alijiunga na taasisi ya Ahadi ya Kutoa (The Giving Pledge), akijitolea kutoa angalau nusu ya mali yake kwa madhumuni ya hisani wakati wa maisha yake.

Anachukulia ahadi hii kama jukumu, lililozaliwa katika imani yake na maadili ya familia. “Wazazi wangu walinifundisha maadili ya hisani, hasa wajibu wangu kama Mwislamu kutunza wale wasio na bahati,” amesema.

Dewji pia ameendelea kufanya mabadiliko makubwa katika michezo, akiibadili timu ya soka ya Simba kutoka kuwa ya kawaida na kuwa klabu yenye nguvu kimataifa.

Chini ya uongozi wake, klabu imepanda kutoka orodha ya ubora zaidi ya nafasi ya 100 hadi kuwa miongoni mwa timu saba bora barani Afrika.

Ameanzisha ulipaji wa mishahara rasmi kwa wachezaji, badala ya mfumo wa awali ambapo wengine walikuwa wakilipwa kiasi kidogo cha Sh50,000.

Baada ya kuwekeza katika miundombinu, maendeleo ya wachezaji na ushirikiano wa kimataifa, Dewji ameiweka timu ya Simba kuwa na nguvu na ushindani katika soka la Afrika.

Maono yake yameenda mbali zaidi ya mafanikio uwanjani; anataka kutumia klabu hii kuwa jukwaa la uwezeshaji wa vijana na ushiriki wa jamii, akihamasisha kizazi kipya cha wanamichezo wa Kitanzania.

“Mimi ni shabiki wa Arsenal, lakini nataka kununua klabu barani Ulaya ili kuunda uhusiano kati ya vilabu vya soka vya Afrika Mashariki na vilabu vya Uingereza,” amesema Dewji.

Zaidi ya soka, Dewji amejikita katika uwekezaji kwenye mchezo wa ndondi, akiamini kuwa unakua kwa kasi kubwa nchini, na unaweza kuibua mabondia vijana, “Hii ni njia nyingine ya kusaidia vijana kupambana na umaskini,” ameongeza.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.