Dar es Salaam. Wadau wa siasa nchini Tanzania wamekuwa na maoni tofauti juu ya kile kinachoendelea ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kwa sasa Chadema kuna mvutano baada ya kuibuka kwa kundi la G55 la watia nia ubunge wa mwaka 2020 na 2025 likijumuisha baadhi ya vigogo wanaokubaliana kwamba No Reforms, lakini si kuzuia uchaguzi wakisema kwa mazingira ya sasa jambo hilo haliwezekani.
Tangu kumalizika kwa uchaguzi wa ndani ya Chadema Januari 21, 2025 kwa Tundu Lissu kuibuka mshindi dhidi ya Freeman Mbowe aliyekuwa anatetea nafasi ya uenyekiti kimekuwa na minyukano ya ndani kwa ndani.
Mbowe alikubali matokeo na kuwapongeza walioshinda akiwemo Lissu na kuwataka kwenda kutibu makovu yaliyotokana na uchaguzi huo. Makundi ya Lissu na Mbowe yamekuwa wakinyukana mitandaoni.
Ni katika mkutano mkuu huo wa uchaguzi uliomwingiza Lissu madarakani, ndio ambao awali ulipitisha azimio la no reforms, no election. Na sasa operesheni ya no reforms, no election (bila mabadiliko hakuna uchaguzi) inaendelea mikoa ya kichama ya kanda ya Kusini yenye mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Wakati Chadema ikiwa na msimamo wa No Reforms, No Election G55 imepinga hatua hiyo jambo ambalo viongozi wakuu wa chama wakiwatafsiri ni wasaliti na wanaokwenda kinyume na uamuzi wa chama hicho.
Kutokana na upinzani huo, baadhi wenyeviti wa kanda wameanza kuwaandikia barua wakitakiwa kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua kwa saini zao kuonekana katika waraka wa G55, wenye hoja tisa za kuitaka Chadema ishiriki uchaguzi huku ukiwa na kichwa cha habari ‘ushauri kwa chama.’
Hata hivyo, G55 wanatafsiri hatua ya kuwataka kujieleza ni kama ubepari ndani ya Chadema na kwamba kuwa na maoni mbadala hakupaswi na ukifanya hivyo inaonekana ni usaliti au uadui.
Ni kutokana na hilo, Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) imeandaa mjadala wa X Space ukiwa na mada ‘Yanayoendelea Chadema yana athari gani kwenye demokrasia?. Wadau mbalimbali wameshiriki mjadala huo uliodumu kwa dakika 120.
Mwandishi mwandamizi wa habari za siasa wa Mwananchi, Peter Elias akichokoza mada hiyo amesema mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe unaoendelea ndani ya Chadema unakipunguzia nguvu katika harakati zake za kisiasa.
“Migogoro ndani ya vyama vya siasa imekuwa ikividhoofisha vyama husika, na tumekuwa na mifano kwa vingi vilivyokuwa na migogoro vilidhoofika na kupoteza nguvu zake na kuwa vya kawaida,” amesema Peter.
Peter amewashauri viongozi wa chama hicho kutoa fursa kuwasikiliza wanaokwenda tofauti na msimamo huo, huku akieleza si jambo baya wakifanya hivyo kwani wanaweza kupima na kuona kama inaweza kuwafaa.
Wakati Elias akieleza hayo, Mdau wa siasa, Makene Naliyaga ameshauri pande mbili zinazotafautiana ndani ya Chadema kuketi meza moja ili kupata mustakabali wa pamoja.
Naliyaga amesema anaiona Chadema inavyokwenda kupunguza nguvu yake yenyewe, lakini endapo wakivuka salama na kuwa na umoja, chama kitakuwa kimeimarika zaidi katika mapambano ya siasa za kudai haki.
“Ukiwatizama G55 wanakubaliana kwa ajenda moja No Reforms lakini kuhusu No Election wanashindwa kuweka wazi umma nini wanachokihitaji. Uongozi wa Chadema wanapaswa kuketi meza moja na G55 ili kutafuta mwafaka wa pamoja na mwisho wa siku kuwa na ajenda moja itakayoaminiwa na umma.
“Tofauti na hapo hii hali ya wananchi kuwaamini na kuwaona kama ni watetezi wao wa kweli itakuwa ngumu na hatimaye tutakosa upinzani wenye nguvu,” amesema Naliyaga.
Kada wa Chadema, Gervas Lyenda ameshuku baadhi ya makada wa Chadema kutaka falsafa zilizokuwa zinatumika na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe katika uongozi mpya unaongozwa na Tundu Lissu ni sababu ya mgogoro unaotamalaki miongoni mwao.
Lyenda amedai karibu asilimia 99 ya wanaounda kundi la G55 ndani ya Chadema ni wale waliokuwa wakimuunga mkono Mbowe wakati wa kampeni za uchaguzi wa ndani uliofanyika Januari 21, 2025.
“Wamekuwa waathirika wa uongozi mpya, ni kama walizoea kula wali nyama kila siku, sasa wanaona utaratibu umebadilika unatakiwa kula wali kwa dagaa haya mabadiliko yanafanya watu kupinga,” amesema Lyenda akitolea mfano yanayoendelea Chadema.
Lyenda ameshauri ni lazima viongozi wakubali kuijenga taasisi hiyo kwa wivu mkubwa, badala ya kuangalia makundi ya pande mbili yaliyojitokeza kipindi cha kampeni za uchaguzi ndani ya chama hicho.
“Hizo tofauti lazima ziishe na bahati nzuri hata wenzetu wa upande wa pili wameshaliona hilo lakini tunapishana, tutamaliza kwa mfumo upi ni muhimu kujua tumekomaa, tumekua hatuna haja ya kufundishana, uchaguzi wowote lazima kunakuwa na vijembe katika kushawishi wapiga kura,” amesema.
Kada mwingine wa Chadema, Yusuph Yusuph amehoji ukimya wa Mbowe unawapa wasiwasi kwa kushindwa kutoa maoni yake juu ya misukosuko inayopitia chama hicho.
Amesema kushindwa kutoa maoni yake au suluhu ya kumaliza kile kinachoendelea ndani ya chama hicho kinawapa wasiwasi baadhi ya wanachama hasa waliopo nje ya mfumo wa uongozi.
“Ni muhimu itumike hekima mwenyekiti na uongozi wake mpya, wamuite aliyekuwa kiongozi wetu Mbowe kuangalia hili linaloendelea la G55, mbona hatuoni maoni yake juu ya hili yupo kimya kuhusu no reforms, no election je, anaungana na wenzake? tunataka kauli yake,” amesema Yusuph.
Amesisitiza ni muhimu Mbowe aitwe wazungumze naye kusikia mtazamo wake na kuona ni ushauri gani anaweza kuutoa katika kusaidia kukivusha chama hicho katika kudhibiti kundi hilo la G55.
Alipoulizwa kwa nini maoni ya Mbowe yanahitajika Yusup amejibu: “Kuna taswira imejionyesha hili kundi ni lilelile lililokuwa linamuunga mkono wakati wa kampeni ni taswira iliyopo hasa kwa tuliopo nje ya uongozi.”
Hata hivyo, jitihada za Mwananchi kumpata Mbowe aliyeiongoza Chadema kwa takribani miaka 21 hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa.
Mchambuzi wa siasa, Dk Conrad Masabo amesema kinachoendelea ndani ya Chadema wakifanikiwa kuvuka salama watathibitishia umma kuhusu ukubwa wa chama cha demokrasia.
Hivi sasa ndani ya Chadema kumeibuka kwa kundi la G55 linalotaka Chadema ishiriki uchaguzi huku uongozi wa chama hicho, ukiweka msimamo wa ‘No Reforms No Election’ utekelezwe kama ulivyopitishwa na vikao halali ya chama.
“Hiki ni kipimo cha tatu cha kwanza ilikuwa kufanya maandamano, pili ni uchaguzi wao wa ndani na tatu ndio hiki kinachoendelea hivi sasa. Nalitazama hili kama kipimo cha demokrasia, hatupaswi kuhofu sana hajaanza Chadema bali kwa vyama vingine pia,” amesema.
“Nimesikiliza maoni ya G55 wakisema wanakubaliana na No Reforms, lakini hawakubaliani na No Election, kwenye mantiki ukisema No Reforms lazima upate ukamilisho wake ili upate maana. Ushauri wao Chadema waingie kwenye uchaguzi, sasa unapingaje uchaguzi ulioshiriki?
“Kwa hiyo naona mantiki yao haina mashiko kwa kiasi kikubwa, huenda wanaikubali ajenda hiyo lakini anayeitekeleza hawamkubali kwa namna anavyoitekeleza,” amesema Dk Masabo ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
‘G55 ni ishara ya demokrasia’
Mtaalamu wa sheria, William Maduhu amesema uwepo wa kundi la G55 ndani ya Chadema unaonyesha uwepo wa demokrasia pana ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Maduhu amesema linapofanyika jambo katika chama cha siasa ambalo hakuna wanachama hawahoji, basi inakuwa ni chama mfu. Amesema kinachoendelea hivi sasa ndani ya Chadema kinaonyesha ukubwa wa chama hicho kinachoweza kushika dola.
“Lakini pia inaonyesha ndani ya chama kuna demokrasia ya kutosha, tuongea ukweli kuna baadhi ya vyama vingine hata hilo kundi lisingepata fursa ya kutosha ya kuzungumza na wanahabari. Kuna baadhi ya vyama vikishatoa uamuzi, hakuna mwanachama anayehoji,” amesema Maduhu.
Crédito: Link de origem