Shinyanga. Ofisa maendeleo ya jamii kutoka Manispaa ya Shinyanga, Nyanjula Kiyenze amesema jumla ya vikundi 19 vimepewa mafunzo ya matumizi na usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 ili kujikwamua kiuchumi, kuondokana na umaskini na kusaidia kuirejesha kwa wakati.
Amesema; “Mafunzo ya usimamizi mzuri wa vikundi, utatuzi wa migogoro, usimamizi wa biashara, utunzaji wa kumbukumbu pamoja na msaada wa kisheria (MSLAC) kwa vikundi 19 yatasaidia katika biashara zenu na kufanikiwa kurejesha mkopo kwa wakati.”
Kiyenze ameyasema hayo leo Jumatatu Machi 24, katika ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
Jumla ya vikundi 19 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vimepatiwa mafunzo hayo.
Amesema washiriki wakiyazingatia mafunzo hayo, yatakuwa mwarobaini wa urejeshaji wa mikopo hususan ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalumu.
Naye Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Elias Masumbuko amesisitiza vikundi kuwa na nidhamu ya fedha na uaminifu katika kurejesha mikopo ili iweze kuwanufaisha wananchi wengi zaidi.
“Fedha hizi ni mapato ya ndani ambayo ni kodi za wananchi, niwaombe kuwa na nidhamu ya fedha hizi, kuweni waaminifu kurejesha kwa wakati ili vikundi vingine vipate kama ninyi mlivyopata, Serikali inafanya juhudi kuhakikisha wananchi wake wanajikwamua kiuchumi na kuondokana na umaskini,” amesema Masumbuko.
“Vikundi vingi huchukua mkopo bila na elimu ya biashara anayotaka kuifanya itakayomsaidia kujua soko la lilipo, matokeo yake hapati faida na kushindwa kurejesha wa wakati au kuamua kutoweka,” amesema Paul Makanyaga.
“Wengine huamua kupotezea lengo lililomfanya kuchukua mkopo huo mfano kutumia pesa hovyo kwa starehe binafsi na kujisahaulisha kwamba anatakiwa kurejesha,” amesema Happiness Henry.
Crédito: Link de origem