Unguja. Mawaziri wawili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) wametofautiana ndani ya Baraza la Wawakilishi kuhusu utekelezaji wa utoaji wa asilimia 10 ya mapato ya halmashauri kwa ajili ya mikopo kwa makundi maalumu.
Mawaziri waliotofautiana ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, aliyeeleza kuwa baadhi ya halmashauri bado hazijatekeleza ipasavyo agizo la kuwasilisha asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya mikopo ya makundi maalumu, huku Waziri wa Nchi ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Masoud Ali Mohamed akisema halmashauri zote zimewasilisha michango yake.
Kutokana na kutofautiana kwa mawaziri hao, kumeibua mjadala kwa baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakitaka kujua kauli ipi sahihi na kuonesha kusikitishwa na mawaziri kutoa kauli mbili tofauti katika jambo moja.
Utofauti huo umebainika leo Alhamisi, Mei 22, 2025 wakati Waziri Masoud akijibu swali la Mwakilishi wa Kiwani, Mussa Foum Mussa aliyesema kumekuwapo na malalamiko kwamba baadhi ya Serikali za mitaa hushindwa kuchangia asilimia 10 ya mapato yanayotokana na makusanyo yao ya ndani kama ilivyoelekezwa na sheria.
Waziri Masoud amesema licha ya kwamba zipo changamoto ambazo hakuzitaja katika kuwasilisha michango hiyo katika ofisi za Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), kwa sasa Serikali za mitaa zote 11 tayari zimeshawasilisha michango yao katika ofisi hiyo, licha ya changamoto zilizopo.
Mei 14, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kazi na Uwekezaji, Waziri Shariff amesema hakuna halmashauri ambayo imekamilisha kiwango hicho, huku halmashauri ya Mjini ikiwa haijawasilisha mchango wake hata kidogo, hivyo kusababisha kusuasua kwa utoaji wa mikopo hiyo.
Mwakilishi wa nafasi za wanawake, Fatma Ramadhan Mohamed, amehoji kwa nini zinatolewa kauli mbili na wanashindwa kuelewa nani anazungumza ukweli, ilhali wapo wanawake na vijana wengi wanaokosa mikopo kwa sababu ya kutowasilisha michango hiyo.
Kauli hiyo imechangiwa pia na Mwakilishi wa Chumbuni, Miraji Khamis Mussa, na Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohamed Ali Suleiman, wakisema kauli hizo zinasikitisha na wanashindwa kuelewa nani yupo sahihi.
“Inasikitisha kuona mawaziri wanatoa kauli mbili tofauti kwa jambo lilelile, tunashindwa kuelewa ipi kauli sahihi. Wiki mbili hazijapita, tumeelezwa hapa kuhusu changamoto hii na Waziri wa Kazi, leo tunaelezwa vingine,” amesema Miraji.
Dk Mohamed amesema inaonesha wazi namna ambavyo kuna changamoto serikalini, kwani haiwezekani mawaziri watoe kauli mbili tofauti katika jambo moja.
Hata hivyo, Waziri Masoud amesimamia kauli yake kwamba ndiyo inatakiwa ichukuliwe, kwani ndiye anayesimamia halmashauri hizo na tayari fedha hizo zimeshawasilishwa, huku akiahidi kuwapelekea taarifa hiyo Wawakilishi hao ili waone.
Pia, Mwenyekiti wa Baraza aliyekuwa akiendesha kikao hicho, Abdulla Hussein Kombo, ameingilia kati na kusema kuwa kauli inayotakiwa kuchukuliwa ni ya Waziri Masoud aliyoitoa leo, na kusitisha mjadala huo.
Crédito: Link de origem