Moshi. Mbunge ametekwa nyara na watu wasiojulikana akiwa anashiriki ibada, amepatikana akiwa ametupwa katika shamba la kahawa lililopo akiwa hajitambui.
Tukio la kutekwa nyara kwa mbunge huyo lilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii muda mfupi tu baada ya kutekwa, ambapo video iliyosambaa mitandaoni ilionyesha gari hilo likiondoka kwa mwendo kasi kutoka nje ya kanisa hilo.
Mbunge huyo wa Juja, nchini Kenya, George Koimburi ambaye alitekwa an watu wasiojulikana na kutupwa eneo la Kibichoi, kaunti ya Kiambu amekutwa akiwa hai.
Taarifa iliyochapishwa na gazeti la Nation la Kenya, imeeleza kuwa Mbunge huyo aliyetekwa nyara Jumapili ya Mei 25,2025 na watu wasiojulikana waliokuwa na gari aina ya Subaru Forester, amepatikana akiwa hajitambui katika shamba hilo.
Mbunge huyo ambaye ni mshirika wa karibu wa aliyekuwa Makamu wa Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, alitekwa mara tu ibada ilipomalizika katika kanisa la Full Gospel lililopo Mugutha na alipopatikana alipelekwa hospitali ya Karen.

Mbunge wa Juja, nchini Kenya, George Koimburi akiwa hajitambui baada ya kutelekezwa shambani.
Kalonzo Musyoka, mmoja wa viongozi wa muungano wa Kenya Kwanza, amelaani tukio hilo huku vyama vya upinzani vikipanga kukutana kesho Mei 27,2025 kujadili kile kilichodaiwa ni manyanyaso yanayoletwa na utawala wa Kenya Kwanza.
Baada ya tukio hilo, mke wa Mbunge huyo, Ann Koimburi alinukuliwa akisema watu waliomteka mumewe walijifanya kama sehemu ya waumini na ndipo baadaye walimchukua kwa nguvu na kumwingiza kwenye gari bila kujitambulisha.
“Tulikuwa ndio tumetoka tu kanisani na ni utaratibu wa kawaida kwa mheshimiwa (mumewe) kusalimiana na watu, lakini ghafla watu wawili walimgeuka na kumlazimisha kuingia kwenye gari na kuondoka naye kwa mwendo wa kasi,”alidai.
Seneta wa Kiambu, Karungo wa Thang’wa alinukuliwa akidai kuwa watu wanaoaminika kuwa maofisa wa usalama ndio waliomteka nyara mbunge huyo, akidai huo ulikuwa mpango wa kumkamata uliokuwa umepangwa wiki iliyopita.
Kulingana na taarifa hizo, dereva wa pikipiki, maarufu Bodaboda ndiye aliyembaini mbunge huyo na katika mahojiano ya awali amelalamika kupigwa na watekaji hao, na polisi wamejiweka kando na tukio hilo wakisema wanachunguza.
Taarifa zilizomkariri Ofisa wa Polisi ambaye hakutaka kutajwa kwa kuwa si msemaji, zilieleza…polisi hivi sasa wanachunguza ni namna gani wasamaria wema waliompata mbunge huyo katika shamba hilo, walitambua kuwa yupo hapo.
“Simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikani tangu Ijumaa (Mei 23,2025) wakati polisi walipotaka kumkamata na operesheni hiyo ilisitishwa. Polisi walijaribu kumkamata alipokuwa anaondoka Juja, lakini alitoroka na bodaboda,”alieleza.
Hata hivyo, kulingana na taarifa hiyo, dereva wake alikamatwa na kupelekwa makao makuu ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na alipohojiwa alisema bosi wake ndiye alimwambia amshushe katikati ya barabara.
Hii ni baada ya kubaini kuwa alikuwa akifuatiliwa na polisi kwa lengo la kumkamata, ambapo alishuka haraka na kupanda Bodaboda na tangu siku hiyo simu zake zilikuwa hazipatikani hadi polisi walipoona taarifa kuwa ametekwa.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, jana na leo polisi walifika eneo ambalo inadaiwa utekaji ulifanyika pamoja na eneo ambalo alipatikana ametupwa ambapo maelezo ya mashuhuda mbalimbali yalirekodiwa na Polisi.
Crédito: Link de origem