Dodoma. Homa uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2025 imezidi kutanda ndani ya Bunge baada ya Mbunge wa Kyerwa (CCM), Innocent Bilakwate kudai kuwa kuna kiongozi anahonga pesa kwa mabalozi ili asichaguliwe.
Amesema hatua ya kiongozi huyo ambaye pia ni mfanyabiashara wa kahawa imekuja baada ya Bilakwate kupambania maboresho ya bei ya kahawa.
Uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, utafanyika Oktoba mwaka huu huku tayari baadhi ya vyama vikiwa vimeshaweka wazi wagombea wao wa nafasi mbalimbali.
Bilakwate ameyasema hayo jana Jumatano, Mei 21, 2025 wakati akichangia katika mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2025/26.
Wizara hiyo iliomba kupitishiwa Sh1.2 trilioni katika mwaka 2025/26 huku Sh702.27 bilioni zikienda katika miradi ya maendeleo. Bajeti hiyo inatarajiwa kupitishwa leo Alhamisi, Mei 22, 2025.
Amesema vita dhidi ya bei ya kahawa bado ipo na baada ya yeye kupambana kuhakikisha kahawa inauzwa katika mnada, vita inayoendelea Kyerwa siyo ya kawaida.
“Ninapowaambia siku ya leo hawa waliokuwa wanawapangia bei wakulima wamezunguka katika kata zote wanakutana na mabalozi na wajumbe wao kuhakikisha kuwa wanawahonga fedha ili mimi ninayepambania bei ya kahawa nisirudi bungeni,” amesema.
“Lakini mimi ninaye Mungu anayenipigania, ninajua kama Mungu aishivyo, ninarudi bungeni. Katika vita hii sitomsahau mkuu wa wilaya na kamati yake ya ulinzi na usalama.”
“Mheshimiwa Mwasa (Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwasa), mama huyu ni mpambanaji kuhakikisha kahawa ya Kagera inaendelea kuleta tija kwa Taifa letu,” amesema.
Amesema hata hivyo wafanyabiashara hao wamekuja na biashara ya Butura ambapo wanachofanya wanapeleka fedha kwa mawakala wao.
“Hili nidhibitishe sitamtaja jina lakini itafika wakati nitamtaja, kuna kiongozi mmoja aliyeaminiwa mwaka jana alikamatwa na gunia sita za kahawa ambayo haionyeshi imepitia katika Amcos ipi,” amesema.
Amesema jambo lingine wanapeleka fedha taslimu ili wakulima wasipeleke kahawa nchini Uganda.
Bilakwate amesema mwaka jana alikwenda katika Kata ya Mlongo na kukuta wakulima wanapewa fedha taslimu Sh3,200 kwa kilo moja ya kahawa lakini kwenye mnada ni Sh4,500.
“Nilimpigia Mrajisi (wa vyama vya ushirika), akasema ngoja afuatilie na nikamwambia kiongozi mmoja ni kinara wa kufanya hiyo biashara. Sitamtaja kwa heshima ya chama changu,”amesema.
Amesema aliwahi kusema huko nyuma kuwa wakulima wapewe bei hali iliyopo kwenye soko, jambo ambalo halikupendwa na kiongozi huyo. “Anasema ninafuatilia maisha yake.”
“Mimi nimechaguliwa na wananchi ninahakikisha nawatetea, nahakikisha naipambania nchi yangu. Kahawa yangu isiende Kenya na nitahakikisha naifanya sitaogopa wala kuyumbishwa,” amesema.
Mbunge huyo amesema hatakubali kama mbunge kuwekwa katika mfuko wa mtu mmoja wakati wananchi wanateseka kwa kupewa bei ya ovyo.
Hata hivyo, alimshauri Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuwa wanaweza kupata bei nzuri zaidi ya iliyopo hivi sasa kwa kutafuta wawekezaji kwenye viwanda vya kuchakata.
Amesema hali hiyo itasaidia kahawa kuuzwa ikiwa imeshachakatwa hivyo kumpatia mkulima bei kubwa.
Crédito: Link de origem