Kumfundisha mtoto kuhusu uchumi wa familia ni njia bora ya kumuandaa kwa maisha ya baadaye.
Mtoto anayepata elimu ya kifedha akiwa wadogo huwa na uelewa mzuri wa jinsi ya kutumia pesa kwa busara, kuweka akiba, na kufanya uamuzi mzuri wa kifedha anapokuwa mtu mzima. Unaweza kutumia mbinu hizi ili kumuandaa mtoto kiuchumi nyumbani:
Moja, mfundishe thamani ya pesa: Watoto wanapaswa kuelewa kwamba pesa hupatikana kwa bidii na inapaswa kutumiwa kwa busara.
Unapowapa pesa kwa ajili ya matumizi madogo kama vile kula shule au kununua vitu vidogo, waeleze umuhimu wa kupanga matumizi yao vizuri ili wasipoteze pesa kwenye mambo yasiyo ya lazima.
Mbili, mpe majukumu na malipo: Njia nzuri ya kumfundisha mtoto thamani ya kazi ni kumpa majukumu madogo nyumbani na kumlipa kwa kazi aliyofanya, kama vile kufagia, kuosha vyombo, au kusaidia kwenye bustani.
Hii inawafanya kuelewa kuwa pesa hupatikana kwa kufanya kazi na si kwa kupewa tu bila juhudi.
Tatu, mfundishe kuweka akiba: Mpe mtoto pesa kidogo na umfundishe kuweka sehemu ya hizo pesa kama akiba.
Unaweza kumpa chombo cha kuhifadhia akiba (kibubu) au kuwasaidia kufungua akaunti ya akiba benki. Mpe malengo ya muda mfupi na mrefu ili ajifunze jinsi ya kuvumilia na kusubiri kabla ya kutumia pesa yake.
Nne, mjengee tabia ya kuthamini bajeti yake: Watoto wanapaswa kuelewa umuhimu wa kupanga mapato na matumizi yao.
Unaweza kuwafundisha kutengeneza bajeti rahisi, kwa mfano, kama wanapewa pesa za matumizi kwa wiki, waelewe ni kiasi gani kinapaswa kutumika kwa chakula, akiba, na matumizi mengine. Hii itawasaidia kuwa na nidhamu ya kifedha wanapokua.
Tano, mfundishe kuhusu matumizi ya fedha kwa busara; Mfundishe mtoto tofauti kati ya mahitaji na matakwa. Kwa mfano, chakula, mavazi, na elimu ni mahitaji ya msingi, lakini michezo ya video au peremende ni matakwa.
Watoto wakielewa tofauti hii mapema, watakua na mazoea mazuri ya kifedha wanapokuwa watu wazima.
Sita, mjulishe kuhusu uwekezaji: Ingawa watoto ni wadogo, ni vyema kuwafundisha kuwa pesa zinaweza kuzalisha pesa zaidi kupitia uwekezaji.
Waeleze kwa njia rahisi kuhusu dhana ya kuwekeza, kama vile kununua hisa, kuweka pesa kwenye akaunti ya faida, au hata kuanzisha biashara ndogo ndogo kama kuuza vitafunwa kwa wenzao.
Saba, wahamasishe kujitegemea kiuchumi: Watoto wanaweza kuanza kujifunza mbinu za kupata pesa kupitia kazi ndogo ndogo kama kuuza barafu, kutengeneza mikufu, au hata kusaidia majirani kwa ada ndogo.
Kuwatia moyo kufanya kazi halali kutawasaidia kuwa na tabia ya kujitegemea kifedha badala ya kutegemea wazazi kila mara.
Nane, wafundishe athari za mikopo na madeni; Watoto wanapaswa kujua mapema kuwa kukopa kunaweza kuwa na athari mbaya ikiwa hakutasimamiwa vizuri. Waeleze kuwa si kila deni ni baya, lakini ni muhimu kuhakikisha kuwa unakopa kwa sababu sahihi na una mpango wa kulipa bila matatizo.
Tisa, mfundishe nguvu ya ushirikiano na kutoa msaada; Ni muhimu kuwafundisha watoto kuwa pesa si kwa matumizi yao binafsi pekee, bali pia kusaidia wengine. Waeleze umuhimu wa kutoa msaada kwa wahitaji na kushiriki katika miradi ya kijamii. Hii inawasaidia kukuza moyo wa ukarimu na kuwafanya wasiwe wachoyo wanapofanikiwa kiuchumi.
Kumi, wafundishe kwa vitendo: Watoto hujifunza zaidi kupitia matendo ya wazazi wao. Ikiwa wewe mwenyewe unadhibiti matumizi yako, unaweka akiba, na unafanya uamuzi mzuri wa kifedha, watoto wako wataiga tabia hizo na kuwa na nidhamu nzuri ya kifedha maishani mwao.
Crédito: Link de origem