Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Maybelline New York, chapa inayoongoza duniani katika sekta ya vipodozi, imezindua rasmi bidhaa zake nchini Tanzania, hatua inayofungua ukurasa mpya katika upatikanaji wa vipodozi vya hali ya juu kwa watu wote.
Uzinduzi huu umefanyika kwa kishindo katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, likiwa ni tukio la kusherehekea uzuri, kujiamini, na ujumuishi, dhamira kuu ya Maybelline ya kuwawezesha wanawake kupitia vipodozi.
Hafla hiyo imefanyika katika Milimani City Mall Kioski, Dar es Salaam, ambapo wateja wa Tanzania walipata fursa ya kuona, kujifunza, na kujaribu bidhaa mbalimbali za Maybelline, zikiwemo foundations zinazolingana na rangi zote za ngozi, rangi nzuri za midomo, na mascara maarufu zinazojulikana kwa ubora wa hali ya juu na bei nafuu.
Lengo kuu la Maybelline ni kuifanya huduma ya vipodozi vya kitaalamu kupatikana kwa kila mtu kwa bei nafuu. Uzinduzi huu haukuhusu tu kutambulisha bidhaa, bali pia kuimarisha thamani ya urembo wa kila mtu na kuinua viwango vya urembo nchini Tanzania.
Meneja wa Maybelline New York, Debra Killingo, amesema kuwa ujio wa chapa hiyo nchini Tanzania ni hatua kubwa katika kuhakikisha vipodozi bora vinawafikia watu wengi zaidi.
“Maybelline New York ni zaidi ya vipodozi—ni kuhusu kujiamini, ubunifu, na kujieleza. Kuingia kwetu katika soko la Tanzania ni hatua muhimu katika kuhakikisha bidhaa za urembo za ubora wa hali ya juu zinapatikana kwa watu wengi zaidi, tukiwahamasisha wakubali uzuri wao wa kipekee,” amesema Killingo.

Baada ya uzinduzi huu, bidhaa za Maybelline zitapatikana katika maduka ya SH Amon pamoja na Maybelline Kiosk katika Milimani City Mall, hatua inayolenga kuhakikisha wapenzi wa vipodozi wanapata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.
Meneja Mkuu wa L’Oreal Afrika Mashariki, Victoria Karanja, amesema kuwa Maybelline inakuja sio tu kuongeza chaguo la vipodozi vya ubora wa kimataifa kwa wanawake wa Tanzania, bali pia kuchangia maendeleo ya sekta ya urembo na kuongeza fursa za ajira.
“Mwanamke anapaswa kuwa na uhuru wa kujiamini kwa kuwa mrembo, na sasa kupitia Maybelline, wanawake wa Tanzania watapata nafasi ya kuwa na mwonekano wa kuvutia kwa kutumia vipodozi vya hali ya juu,” amesema Karanja.

Maybelline New York ni chapa namba moja ya vipodozi duniani, inayotoa bidhaa za urembo za hali ya juu kwa kufuata mitindo ya kisasa. Inapatikana katika zaidi ya nchi 120, ikiwa na dhamira ya kuleta ubunifu, ujumuishi, na kuwawezesha watu kujieleza kupitia vipodozi vyao.
Uzinduzi wa Maybelline Tanzania unaashiria hatua kubwa katika sekta ya vipodozi nchini, ukiwaletea wanawake wa Kitanzania bidhaa za kimataifa zinazotambulika kwa ubora wake kote ulimwenguni.
Crédito: Link de origem