Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Daraja la muda linalounganisha Kata za Bonyokwa na Kinyerezi ambalo lilikatika kutokana na mvua zilizoanza kunyesha limerejeshwa.
Daraja hilo lilikatika juzi kutokana na mvua kubwa zilizoanza kunyesha usiku na kusababisha wananchi wa maeneo hayo kukosa mawasiliano.
Mkandarasi Kampuni ya Nyanza Works aliyepewa kazi ya kujenga daraja la kudumu pamoja na barabara hiyo ya Bonyokwa – Kimara alianza kujenga daraja la muda baada ya kuondoa daraja la awali la chuma.
Machi 30,2025 Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, amefanya ziara katika eneo hilo kujionea hali halisi na kuwapa pole wananchi wa maeneo hayo.
“Nawapa pole kwa changamoto iliyojitokeza, Jimbo la Segerea hata mvua isiponyesha lakini maji yanayotoka sehemu nyingine bado yanakuja kutuathiri, mkandarasi atafute namna watu waweze kupita na kuongeza njia nyingine mbadala kwa sababu wananchi wengi wanatumia njia hii wakiwemo wa Mbezi, Ubungo na maeneo mengine,” amesema Bonnah.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kisiwani, Sulela William, amesema mawasiliano yanapokosekana wananchi hulazimika kutafuta njia mbadala hali inayoongeza gharama za usafiri hadi kufikia Sh 8,000 wakati eneo hilo hutembea kwa miguu au kulipa kati ya Sh 1,000 au 2,000 kwa usafiri wa bodaboda.
Diwani Kata ya Bonyokwa, Tumike Malilo, amesema wakazi wa Kisiwani wengi wanatumia njia hiyo na kushauri njia ya Masedonia na kabla ya Masedonia ziimarishwe ili kukitokea changamoto wasikose mawasiliano.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam, amemtaka mkandarasi huyo kuendelea kuimarisha njia ya zamani ili ipitike kama hapo awali.

Kwa upande wake Meneja Mradi kutoka Kampuni ya Nyanza Works, Injinia Gilbert Bahesha, amesema walikabidhiwa mradi huo mwaka 2024 na kuanza kuondoa daraja la zamani kisha kujenga la muda.
“Hatukutarajia kwamba mto utajaa haraka, kiasi cha maji kilichokuja kiliondoa daraja la dharura na kwa sasa tuko kwenye harakati za kuwezeshe njia nyingine mbadala.
“Kila kitu kiko ndani ya uwezo wetu na ratiba zinazingatiwa ili tuweze kukamilisha mradi kwa wakati,” amesema Injinia Bahesha.
Mbunge Bonnah pia amekagua miundombinu ya barabara na madaraja kama vile Daraja la Kavesu, Daraja la Kinyerezi Mtaa wa Kanga na Daraja la Kwa Mzava.
Crédito: Link de origem