Dar es Salaam. Bado ni majanga. Unaweza kusema kwa uhakika kwamba unafuu uliotarajiwa na wakati wa Jiji la Dar es Salaam katika usafiri ya Mabasi Yaendayo Haraka haujapatikana.
Sasa ni takribani miaka tisa tangu kuanzishwa kwa usafiri wa mabasi hayo mwaka 2016, lakini9 mradi huo, hasa kwa awamu ya kwanza, lakini haujakidhi matarajio ya usafiri kwa wananchi kutokana na kero lukuki zinazoukumba, ikiwamo abiria kukaa muda mrefu vituoni kutokana na upungufu wa magari na njia husika kutokuwa na daladala.
Kutokana na uchache huo, watumiaji wanadai wa mabasi hayo maarufu Mwendokasi hutumia wastani wa saa moja hadi mbili kusubiri usafiri, wakati wangine waliokata tiketi hulazimika kuondoka vituoni kutafuta usafiri mwingine, hasa wa pikipiki ambao ni wa haraka lakini hatarishi.
Mbali na hayo, baadhi ya abiria wanaotumia usafiri huo wamekuwa wakipata majeraha ya kuvunjika viungo wakati wakigombea magari, kitendo ambacho si lengo la kuanzishwa kwa mradi huo.

Mwananchi leo Jumanne, Mei 27, 2025, imetembelea vituo vya mabasi yaendayo haraka kuanzia Kimara hadi Kivukoni na Kivukoni hadi Gerezani na kushuhudia abiria wakisota ndani ya vituo hivyo wakisubiri usafiri, kama ambavyo imekuwa kwa muda mrefu.
Vituo vya Kimara, Gerezani, Fire na Kivukoni ndivyo vinavyoonekana kuwa na idadi kubwa ya wasafiri nyakati za asubuhi na jioni huku mabasi yakiwa hayatoshelezi.
Kutokana na hali hiyo, Msemaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), Gabriel Katanga, amekiri kuwepo changamoto hiyo na kuwaomba radhi Watanzania kutokana na changamoto hiyo na kuwataka kuwa wavumilivu.
Ameahidi kuwa miezi miwili ijayo wanatarajia kupokea mabasi mapya 100 ambayo yatamaliza kero hiyo.
“Ni kweli hivi sasa kuna changamoto ya mabasi ambayo inatokana na yale ambayo tunatumia kuhudumu kukaa kwa muda mrefu tangu 2016. Yanaanza kazi saa 12 alfajiri na kupumzika saa 6 usiku,” amesema.

“Aidha, uwezo wa mabasi yenyewe kufanya kazi umeshuka, hivyo idadi ya mabasi tuliyotarajia kuwa barabarani imepungua, na ndiyo inasababisha kero,” amefafanua.
Sebastian John, mkazi wa Mbezi ambaye ni mtumiaji wa usafiri huo, amesema umekuwa kero badala ya msaada kwa wananchi.
“Unafika saa moja kituoni, unaondoka saa mbili au saa tatu. Sasa hii ni shida. Tumeshalalamika kwa muda mrefu, tunaahidiwa tu mabasi yanakuja bila mafanikio. Unapanda kwenye gari unaibiwa, unachafuliwa – usafiri si wa kistaarabu tena,” amesema.
John ameshauri Serikali iangalie namna ya kuwajumuisha wawekezaji wengine kwenye mradi huo ili yapatikane magari mengine kusaidia wananchi kuondokana na kero, badala ya kuendelea kutumia magari machache ambayo mengine ni mabovu.
Hosiana Patrick, mkazi wa Kigamboni, amesema tatizo kwenye mradi huo ni uchache wa mabasi na wingi wa abiria.
“Unaweza kutumia saa mbili upo kituoni tu nyakati za asubuhi au jioni. Usipojiongeza unaweza kukesha. Pia wapo hawa wanaokatisha tiketi, wao muda wote wanasema hawana chenji, hili ni tatizo,” amesema.
Naye, Maria Mlay, mkazi wa Kimara, amesimulia jinsi alivyopata majeraha kwenye mkono wake baada ya kusukumwa na abiria wenzake, wakati wa foleni ya kuingia kwenye basi la Mwendokasi.
“Nilikuwa naenda kazini asubuhi. Mwendokasi ilipofika, watu wakawa wanakimbilia; kila mtu anataka kupanda kwanza. Nilisukumwa, nikaanguka na kuumia mkono wa kushoto. Mpaka leo siwezi kuuinua vizuri,” amesema Maria.
Abiria mwingine, Ramadhani Komba, mzazi na mkazi wa Kimara Korogwe, amesema matumizi yake yameongezeka kutokana na kutumia bodaboda badala ya usafiri huo, ambapo pamoja na familia yake hutumia zaidi ya Sh3,000 asubuhi kuwahi kwenye majukumu.
Wapo waadhi ya majeruhi waliopokewa katika Kituo cha Afya cha Kimara waliripotiwa kuumia kutokana na kuumia wakati wa kupanda Mwendokasi, hususan wakati wa asubuhi ambapo abiria huwa ni wengi.
“Tunapokea majeruhi waliopata majeraha kutokana na msongamano na kusukumana wakati wa kupanda Mwendokasi, wengine huteleza na kuvunjika mkono au kuchubuka. Hali hizi zimekuwa za kawaida hasa nyakati za asubuhi,” ameeleza mhudumu mmoja wa afya kutoka kituo hicho, aliyeomba jina lake lihifadhiwe kwa kuwa si msemaji.

Askari polisi katika Kituo kidogo cha Kimara ambaye pia hakutaka kuandikwa jina lake kwa kuwa si msemaji, amesema kukiwa na umati mkubwa hali inakuwa mbaya licha ya kuimarisha ulinzi na kuwataka abiria kufuata utaratibu wa kuingia kwenye magari.
“Asubuhi inakuwa balaa, huwa tunashiriki kusaidia watu kuwapeleka hospitali kwani wapo ambao hawawezi kugombania gari na tumekuwa tukisisitiza kufuata utaratibu uliopo, kwani usalama wao ni wa muhimu zaidi,” amesema.
Akijadili hali hiyo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Lawi Yohana amesema mfumo wa mwendokasi umeshindwa kufikia malengo ya awali ya kuongeza uwezo wa watu kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa haraka, jambo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi ya jiji kama Dar es Salaam.
“Moja ya matarajio ya mfumo huu ilikuwa ni kupunguza muda wa watu kuwa barabarani na kuwawezesha kutumia muda huo katika uzalishaji au shughuli za kibiashara. Lakini hali ya sasa ni tofauti. Wananchi wanapoteza saa nyingi wakisubiri magari au kupambana kuingia kwenye mabasi machache yaliyopo,” amesema mchumi huyo.
Kwa mujibu wa mchumi huyo, hali mbaya ya uendeshaji wa mfumo wa mwendokasi inatokana na idadi ndogo ya mabasi yanayofanya kazi, ukosefu wa matengenezo ya mara kwa mara na uharibifu wa miundombinu ya magari hayo.
Amesema duniani kote huduma bora za usafiri mijini zinaendeshwa kwa mfumo wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP), ambapo Serikali hujikita katika kupanga sera, kujenga miundombinu na kusimamia kanuni, huku sekta binafsi ikihusika moja kwa moja katika uendeshaji na utoaji wa huduma.
Hoja hiyo inaungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Mwinuka Lutengano, ambaye amesema kuna haja ya kushirikisha sekta binafsi katika uendeshaji wa huduma hiyo ili kuleta ufanisi.
“Hakuna jiji duniani lenye usafiri wa umma wa uhakika ambalo halijawekeza katika ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. Serikali ijikite kwenye sera, ujenzi wa miundombinu na usimamizi, lakini uendeshaji uachwe kwa sekta binafsi,” alifafanua.
Wakati wasomi hayo wakisema hayo, Msemaji wa mradi huo, Katanga amesema tayari Serikali imeagiza mabasi 100 mapya na kati ya hayo, moja limewasili nchini na linafanyiwa majaribio.
Amesema mabasi yanapoagizwa nje, mzalishaji hutoa basi la mfano la majaribio na baadaye hurudi kueleza changamoto au maeneo yenye kuhitaji maboresho kwenye usafiri huo.
“Ukisema ulete magari 100 nchini kwa mara moja ukaja kubaini yana changamoto, huwezi tena kurudisha magari hayo China,” amesema.
Katanga amesema ili wananchi waondokane na kero, mabasi 100 yanahitajika barabarani na sasa idadi iliyopo barabarani wakati mwingine ni 90 hadi 80, na ndiyo maana changamoto inatokea.
Kuhusu abiria kupata majeraha, Katanga amesema wameweka utaratibu mzuri wa kila abiria kupanda basi kwa ustaarabu na wapo askari wanaosimamia utekelezaji wa utaratibu huo.
“Utaratibu upo na unasaidia, lakini wakati mwingine watu wanavunja utaratibu,” amesema.
Akizungumzia huduma ya usafiri wa wanafunzi, Katanga amesema utaratibu wa kuhudumia wanafunzi ni mzuri na wamehakikisha hawapitii changamoto.
Amesema yapo mabasi mawili asubuhi na jioni ambayo hutoa huduma pekee kwa wanafunzi.
Ahadi iliyowahi kutolewa
Ahadi za ujio wa mabasi kutatua kero ya usafiri ndani ya mradi huo zimekuwa zikitolewa mara kwa mara, mathalan, Januari 2, 2025, na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, aliyesema sekta binafsi italeta mabasi hayo na yangewasili kati ya Februari na Machi, 2025.

Katika ahadi hiyo, alisema mabasi 177 yangetumika kwenye njia ya Kimara na 755 kwa njia ya Mbagala na huduma zingezinduliwa Machi.
Ukiachana na Msigwa, ahadi nyingine ilitolewa mwishoni mwa Januari mwaka huu na aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Dk Athuman Kihamia, aliyesema mabasi 250 yanatarajiwa kuwasili kutoka China.
Kwa mujibu wa Dk Kihamia, mabasi hayo yalikuwa katika hatua za mwisho za maandalizi na yangefika nchini kati ya Machi hadi Aprili.
Crédito: Link de origem