top-news-1350×250-leaderboard-1

Matukio ya wizi yaliyotikisa vituo vya polisi

Dar es Salaam. Matukio ya uvunjaji, wizi wa pikipiki na mifugo yanatajwa kuripotiwa zaidi katika vitu vya Polisi kwa miaka miwili mfululizo wa 2023 na 2024, Ripoti ya hali ya uhalifu ya Jeshi la Polisi inaeleza.

Kuwapo kwa matukio haya kunatajwa kusababishwa na hali duni ya kiuchumi, ukuaji wa miji, utandawazi, tofauti kubwa ya hali ya maisha kati ya walionacho na wasionacho, uhaba wa ajira kwa vijana, tamaa ya kumiliki mali.

Na ili kukabiliana na hali hiyo inashauriwa jamii hususan vijana kushiriki katika shughuli halali za ujasiriamali na uchumi ili kujipatia kipato.

Ripoti hii iliyochapishwa na ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha licha ya makosa ya kuwania mali kati ya mwaka 2023 na 2024 kupungua kwa asilimia 6.6 lakini bado uvunjaji katika nyumba za watu ni kilio.

Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2024, jumla ya makosa 21,870 yaliripotiwa yakilinganishwa na makosa 23,414 katika kipindi kama hicho mwaka 2023.

Kati ya matukio yaliyoripotiwa, uvunjaji uliongoza kwa kuwa na matukio 10,749, wizi wa pikipiki ulikuwa na matukio 3,851, wizi wa mifugo matukio yalikuwa 3,683 huku unyang’anyi wa kutumia silaha ulikuwa na matukio 1,027.

Mikoa ya kipolisi iliyoripoti idadi kubwa ya makosa ya kuwania mali kwa mwaka 2024 ni Kinondoni (1,864), Arusha (1,557), Dodoma (1,418), Tanga (1,157) na Kagera (1,076).

Mikoa ya kipolisi yenye idadi ndogo ya makosa ni Singida (141), Geita (148), Katavi (190), Simiyu (209) na Kaskazini Pemba (224).

Hata hivyo, haya yanatokea wakati ambao baadhi ya maeneo nchini yamekuwa yakiimarisha ulinzi jamii (ulinzi shirikishi) ili kuhakikisha kuwa watu wake wanakuwa salama kipindi chote.

Hilo linafanyika kwa ushirikiano wa viongozi wa mitaa na watu wanao waongoza kwa kuwa tayari kuchangia fedha kulingana na makubaliano yao kwa kipindi husika.

Baadhi ya maeneo hutoza Sh3,000 kwa mwezi, Sh2,000 au Sh1,500 kulingana na kile kilichokubalika.

“Wanasaidia kwa kiasi fulani kwa sababu yale matukio ya kuvunja mara kwa mara yamepungua, hata magari tunaweza kulaza nje kwa sababu wapo muda wote kuanzia saa sita usiku na wana zunguka mitaani,” anasema Anselm Antony mkazi wa Tabata.

Anasema licha ya kuwapo kwa udokozi ambao bado unafanyika lakini si kwa kiasi kilichokuwapo awali, jambo ambalo linawafanya kuwa na amani.

Pamoja na kuwapo kwa ulinzi shirikishi, baadhi ya maeneo watu wamekuwa wakitozwa hela lakini matukio hayo yanaendelea kushuhudiwa huku watu wakificha ushauri.

“Juzi tu hapa mtu kavunjiwa duka lake, ana CCTV kamera ili kuficha ushahidi ikafunikwa, watu wamesema likitokea tena tukio kama hili hawatalipa hela,” amesema Salum Salim mkazi wa Kimara King’ong’o.

Katika kukabiliana na matukio haya ya kuwania mali, Jeshi la Polisi limeeleza kuwa moja ya mikakati yake ni kuzishawishi taasisi za fedha ili ziweze kupunguza urasimu wa upatikanaji wa mikopo nafuu na kupunguza riba kubwa zinazotozwa katika mikopo hiyo.

Pia limetaka kuwapo kwa mpango endelevu ya utoaji elimu kwa umma ya ujasiriamali, Kuhamasisha jamii ijenge utamaduni na utaratibu wa kutoa taarifa kwa wakati kwenye vyombo vya dola wanapobaini viashiria vya uhalifu.

“Kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuibua fursa kwa vijana ili kujipatia kipato na kujiepusha na vishawishi vya kujiingiza kwenye uhalifu,” limeeleza Jeshi la Polisi.

Kuhusu wizi wa mifugo, Jeshi kwa kushirikiana na wizara ya mifugo imeendelea kuelimisha jamii ya wafugaji juu umuhimu wa uwekaji alama za utambuzi wa mifugo yao Kuendelea kupiga marufuku machinjio na minada isiyo rasmi.

Mbali na uvunjaji, wizi wa pikipiki na mifugo, matukio mengine yaliyoainishwa katika ripoti hii ni unyang’anyi wa kutumia silaha matukio yameongezeka kutoka 394 mwaka 2023 hadi kufikia 410 mwaka jana, huku matukio ya wizi yakitoka 315 hadi kufikia 374, mtawaliwa.

Wizi wa Magari matukio yalipungua kutoka 85 mwaka 2023 hadi kufikia 69 mwaka jana, kuchoma nyumba moto yakitoka 719 hadi kufikia 694 mwaka jana.

Matukio ya uhalifu wa kifedha yaliongezeka kutoka 862 mwaka 2023 hadi kufikia 924 huku matukio ya wizi wa silaha yakitoka 13 hadi matukio 19 mwaka jana.

Katika upande wa uharibifu wa miundombinu mwaka 2023 hakukuwa na tukio lolote lililoripotiwa lakini kwa mwaka 2024 yaliripotiwa matukio 70 katika vituo mbalimbali vya polisi.

Mtaalamu wa uchumi kutoka chuo kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Lutengano Mwinuka anasema umasikini unaweza kuwa sehemu ndogo inayoweza kumfanya mtu kuingia katika vitendo vya uhalifu lakini tabia hizo huanzia katika maadili na malezi.

“Watoto wanakuwa na marafiki wa aina gani inayoweza kuleta vishawishi na wakajikuta wanafanya uhalifu,” amesema.

Amesema jambo hilo linaweza kushughulikiwa kwa kuangalia mifumo ya kimalezi, makuzi katika taasisi mbalimbali ikiwemo za kidini na jamii kwa ujumla na kuangalia namna familia inavyoweza kuwalea watoto kuwa raia wema.

“Hii itamfanya mtu kuwa na tabia njema na kuwafanya watu wawe na mchango mzuri katika taifa,” amesema Mwinuka.

Mtaalamu wa Uchumi, Dk Felix Nandonde amesema hali ya maisha hasa kwenye makazi ya watu masikini huweza kuwa chanzo cha uhalifu ambao unahusisha uporaji wa mali ndogo.

“Ili kukabiliana na hili tuangalie namna ya kuhakikisha watu wanafanya kazi ili waweze kupata malipo stahiki yatakayowawezesha kukabiliana na hali za maisha kwa sababu wanaokaa bila kufanya kazi kwa muda mrefu huweza kujikuta wakitamani kufanya matukio ya uhalifu,” amesema.

Hilo liende sambamba kuhakikisha kodi tunazotozwa zinamuachia mtu kiasi fulani cha fedha zinazomtosha kuishi huku akisisitiza kuwa hii ni sehemu ambayo serikali inaweza kutumia kuhakikisha hali za maisha za watu haziteteleki.

Pia alitaka utungaji Sera kutoa kipaumbele kwa sekta zilizoajiri watu wengi huku akiweka bayana kwa nchi za Afrika kuwa ni kilimo hivyo ni vyema kuhakikisha uwepo wa nyenzo bora, uhakika wa masoko ili kuwatoa wananchi katika hasara wanayoweza kuipata.

Hata hivyo amesema ili kukabiliana na hali hii ni vyema kuhakikisha makundi mengine yenye ushawishi wakiwamo viongozi wa dini, watu wa ustawi wa jamii wanakemea suala hili kwani wana nafasi ya kufanya, hivyo kwa sababu watu wengine wanafanya vitendo hivi kutokana na tamaa ya kupata mali za haraka.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.