top-news-1350×250-leaderboard-1

Mapya yaibuka dereva Mtanzania anayeshikiliwa Sudan Kusini

Dar es Salaam. Dereva Mtanzania, Juma Maganga (45) anayeshikiliwa nchini Sudan Kusini akitakiwa kulipa fidia ya zaidi ya Sh938.7 milioni baada ya kusababisha kifo anatarajiwa kufikishwa mahakamani Machi 28, 2025.

Kwa mujibu wa Gabriel Kiliki, mmiliki wa gari alilokuwa akiendesha Maganga, dereva huyo anatarajiwa kufikishwa katika mahakama ya kimila.

Pia amesema mwanasheria waliyempata anataka malipo ya Dola 1,000 za Marekani (Sh2.6 milioni) ili asimamie kesi hiyo.

Mkuu wa utawala kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Uganda, Haikael Shishira alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia suala hilo aliomba apewe muda ili alifuatilie.

“Naomba nifuatilie nijue nini kinachoendelea na nani alikabidhiwa suala hilo, nitakurudia,” amesema Haikael alipozungumza na Mwananchi kwa njia ya simu saa 6:47 mchana. Alipotafutwa kwa nyakati tofauti hadi saa 11:57 jioni hakuwa amepatikana, simu yake iliita bila kupokewa.

Suala hilo linashughulikiwa kutoka Uganda kwa sababu Tanzania haina ubalozi Sudan Kusini.

Kiliki amesema mwanasheria huyo amewaeleza katika mahakama za kimila adhabu kwa mtu aliyeua bila kukusudia ni ng’ombe 31 wanakadiriwa kuwa sawa na Dola 27,000 (sawa na Sh71.5 milioni).

Maganga anashikiliwa na Polisi mjini Juba, Sudan Kusini baada ya kumgonga mwanamume aliyefariki dunia Februari 14, mwaka huu alipokuwa akipeleka mahindi ya msaada nchini humo. Gari na mzigo vinashikiliwa.

Familia ya marehemu ilidai fidia ya zaidi ya Sh925.075 milioni kutoka kwa familia ya dereva na mmiliki wa gari aliye Tanzania.

Kiliki amelieleza Mwananchi kuwa: “Tulimuuliza (mwanasheria) kama adhabu inajulikana yeye ataenda kufanya nini akasema atajitahidi kukata rufaa Mahakama ya Afrika Mashariki kupinga adhabu hiyo hukumu itakapotoka,” amesema.

Amesema mazungumzo ili kufikia makubaliano na mwanasheria huyo yanaendelea ingawa hamfahamu vizuri.

Rehema Mongi, mke wa Maganga amelieleza Mwananchi ugumu wa maisha anaopitia akilemewa na majukumu ya kutunza familia.

“Mume wangu anapelekwa mahakamani kwa mara ya kwanza, anahitajika mwanasheria sijui naanzia wapi naishia wapi. Nimepoteza mwelekeo.

“Mahitaji ya hapa nyumbani na ya huko Sudan yanatushinda, sielewi hata napata wapi fedha kwa sababu kule Sudan hawana utaratibu wa kuhudumia mahabusu ni sisi wenyewe ndugu ndio tumuhudumie chakula, maji na kila kitu,” amesema.

Amesema mtoto wa kiume wa Maganga aliyekuwa naye Sudan ajali ilipotokea ndiye amebeba jukumu la kuhakikisha mzazi wake anakula kila siku.

“Nauli kwa siku kwenda gerezani kumpelekea baba yake mahitaji ni Sh10,000 ya Uganda kwenda na kurudi.  Kwa hiyo asubuhi na jioni nauli tu ni Sh20,000,” amesema.

Anasema nyumbani anaishi na watoto wanne, wadogo watatu wanasoma na mwingine ni mchanga. Pia mwanaye aliye Sudan na baba yake ameacha mke na mtoto mchanga wa miezi sita.

“Mkwe wangu nipo naye hapa nyumbani, nina mdogo wangu wa kike mwenye changamoto ya ugonjwa wa akili naishi naye hapa, mambo ni mengi sielewi nieleze kipi niache kipi, mimi ni fundi cherehani ila kwa sasa nimeshindwa kabisa hata kushona,” amesema na kuongeza:

“Afya yangu si nzuri, mama yangu alishafariki dunia, baba yangu ni mgonjwa wa muda mrefu ananitegemea kwa asilimia kubwa.”

Maganga akitarajiwa kufikishwa mahakamani, Machi 16, 2025 mmiliki wa gari alipewa gharama za fidia zinazopaswa kulipwa ili dereva na gari viachiwe.

Familia ya marehemu ilidai fidia ya Pauni ya Sudan milioni 213.06 (sawa na Sh938.71 milioni). Kiasi hicho kinahusisha pia gharama za msiba.

Mchanganuo wa fidia ulihusisha Pauni za Sudan 161.5 milioni kwa ajili ya familia, msiba siku ya pili ulitumia Pauni 10.09 milioni, siku nyingine ya msiba Pauni 19.24 milioni na gharama nyingine zikiwa Pauni 21.46 milioni.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.