top-news-1350×250-leaderboard-1

Mamlaka Mafunzo ya Amali Zanzibar kujenga vyuo vipya sita

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar (VTA) inatarajia kujenga vyuo vipya sita ambavyo vitajikita zaidi kutoa elimu katika Uchumi wa Buluu.

Kwa sasa mamlaka hiyo ina vyuo vitano ambapo vitatu vipo Unguja na viwili Pemba.

Akizungumza Machi 20,2025 Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar (VTA), Dk. Bakari Ali Silima, amesema wametanua wigo kwa vyuo vipya ili kuwawezesha vijana wengi zaidi kujiunga na kuweza kujiajiri.

Dk. Silima alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya miaka 30 ya Veta yanayofanyika jijini Dar es Salaam ambapo mamlaka hiyo pia imeshiriki.

“Vyuo vitano ulivyonavyo vimewekwa kisera kwamba kila mkoa uwe na chuo cha mafunzo ya amali lakini sera za sasa zinaaelekeza kwamba kila wilaya iwe na chuo, hivyo tuko katika maandalizi ya kujenga vyuo vingine sita ili kufikia lengo la kila wilaya kuwa na chuo,” amesema Dk. Silima.

Amesema pia vyuo vilivyokuwepo walishaanza kutoa fani za uvuvi kuendana na Sera ya Uchumi wa Buluu lakini wametanua wigo kwa vyuo vipya ili kuwawezesha vijana wengi zaidi kujiunga na kuweza kujiajiri.

Kwa mujibu wa Dk. Silima, mwaka 2020 walifanya utafiti kwa kushirikiana na Veta na kubaini asilimia 70 ya wahitimu wa mafunzo ya amali walikuwa wako katika mfumo wa ajira.

“Mafunzo ya ufundi stadi au amali ni ajira, ukiingia katika vyuo hivi unapata uwezo wa kujiajiri wewe mwenyewe kwahiyo, kila anayetaka kujiajiri kupitia ufundi ajiunge katika vyuo hivi na tumeweka somo la ujasiriamali kuwa la lazima ili kukuwezesha kuitumia taaluma uliyoipata kuweza kujiajiri wewe mwenyewe na ikiwa utaajiriwa sehemu nyingine hiyo ni faida ya ziada,” amesema Dk. Silima.

Mkurugenzi huyo wa VTA amesema pia wana makubaliano ya kushirikiana na Veta katika nyanja za kubadilishana mitaala, wataalam na kushirikishana katika mambo mbalimbali.

“Mfano tulipotengeneza mitaala kule Visiwani tulichukua baadhi ya wataalam kutoka Veta na kuiandaa kwa pamoja ndiyo maana tumekuja kushiriki katika maadhimisho ya miaka 30 ya Veta kwa sababu tulipoanza mwaka 2005 tulianza kwa kushirikiana nao na mpaka sasa tunaendelea kushirikiana.

Dk. Silima amesema mafunzo ya amali yanahusisha watu wote na kuitaka jamii kuacha dhana potofu kwa kudhani kuwa yanawahusu wale walioshindwa masomo ya sekondari.

“Kuna watu wengine wamejitokeza wana PHD (Shahada ya Uzamivu) lakini wamekuja kupata mafunzo ya amali, anapata mafunzo ya wiki tatu au sita ili akafanye kazi zake vizuri zaidi, kwahiyo hili linalozungumzwa kwamba wakitoka vyuo waje wajiunge ni la kutilia mkazo,” amesema Dk. Silima.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.