Na Mwandishi Wetu
Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango ametoa wito kwa Watanzania kukemea vitendo vya ukatili ulioshamiri dhidi ya wanawake na watoto na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa dhidi ya wahusika.
Ametoa kauli hiyo leo Machi 3,2025 mkoani Kigoma wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Kanda ya Magharibi.
Dk. Mpango ametaja baadhi ya vitendo hivyo kama mauaji, ubakaji, ulawiti, kupigwa, kunyanyaswa, kunyimwa haki za kumiliki ardhi na mali nyingine za familia, urithi, fursa za elimu, ukeketaji, adhabu kubwa zisizowiana na kosa alilotenda mtoto.
Amesema baadhi ya vitendo hivyo vinafanywa na wanafamilia au ndugu wa karibu na sehemu kubwa ya vitendo hivyo havitolewi taarifa kwenye vyombo vya sheria ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa na kuongeza kuwa wakati mwingine, baadhi ya mila na desturi katika jamii hutumika kuwakandamiza wanawake na watoto.
Aidha Makamu wa Rais ametoa rai kwa Kongamano hilo ambalo idadi kubwa ya washiriki wake ni wanawake na ambao ni walezi wa familia, kuelekeza nguvu pia katika kumlinda mtoto wa kiume ili kumhakikishia usalama wake.
Amesema uwekezaji jitihada kidogo kwa mtoto wa kiume imepelekea mtoto wa kiume kujikuta katikati ya matatizo lukuki yakiwemo matumizi ya madawa ya kulevya, ushoga na aina nyingine za ukatili.
Crédito: Link de origem