Makamu mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Zanzibar Hamad Mkadam amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, wakati akipatiwa matibabu ya afya kwenye moja ya hospitali kisiwani Pemba.
Mkadam amefariki ikiwa ni mwezi mmoja na siku nne umepita tangu achaguliwa kuendelea kuhudumu kwenye nafasi hiyo katika uchaguzi uliofanyika Februari 2,2025 jijini Dar es Salaam.
Hadi anafariki alikuwa amehudumu kwenye wadhifa huo kwa miongo miwili na nusu, alianza kukalia nafasi hiyo pasi na upinzani katika kipindi chote cha utawala wa aliyekuwa mwenyekiti na mwanzilishi wa chama hicho Augustino Mrema aliyefariki dunia Agosti 21, 2022.
Taarifa za kifo chake, zimethibitishwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Richard Lyimo, “Tumepata pigo Mukadam amefariki, sababu ya kifo chake ni tatizo la moyo ulipanuka ambapo maradhi hayo yamemsumbua kwa muda mrefu, alikuwa akipatiwa matibabu kwa bahati mbaya amefariki dunia, ni pengo kubwa ndani ya chama.”
Amesema viongozi wa chama hicho watakutana kujadiliana kuhusu msiba huo na wanatarajia kumtuma mmoja wa viongozi kwenda kuwawakilisha kwenye maziko yake Pemba.
“Tutakuwa ofisini tukijadiliana lakini nataka kukuambie yule ni Mwislamu na mara nyingi huwa wanawahi kufanya mazishi, na hali ninavyoiona hatuwezi kuwahi kwenye mazishi lakini baada ya kikao tutatuma mwakilishi,” amesema Lyimo
Amesema Mukadam ameshika wadhifa huo kwa zaidi ya miaka 25 huku akieleza alianza kuongoza tangu kipindi cha mwanzilishi wa chama hicho, Augustino Mrema.
“Kifo chake ni pigo alikuwa muhimili wa utulivu visiwani Zanzibar kutokana na uzoefu na unguli wake kwenye siasa,” amesema.
Richard amesema Mukadam alikuwa mwanachama mtiifu hakuwa na uchu wa madaraka hata baada ya kutokea kifo cha Mrema Agosti 21, 2022 alichaguliwa na Sekretarieti ya chama hicho kushika nafasi hiyo kwa muda, lakini hakung’ang’ania.
Crédito: Link de origem