top-news-1350×250-leaderboard-1

Makalla atoa neno mjadala wa No reforms, No election mitandaoni

Moshi. Wakati kampeni maarufu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ya No reforms, No election ikiendelea kutawala kwenye  mitandao ya kijamii nchini, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema wanaotekeleza kampeni hiyo wanajifurahisha tu na uchaguzi upo palepale.

Kuanzia jana katika mitandao ya kijamii kumekuwa na wimbi la kufikisha ujumbe huo kwa kuandika kampeni hiyo kwenye eneo la maoni (comment) katika kila kitu kinavyowekwa mitandaoni bila kujali ni ukurasa wa nani.

Leo Jumapili Juni 8,2025, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema wanaoendeleza kampeni hiyo mitandaoni wanajifurahisha tu na kuwa uchaguzi utafanyika.

“Hata mngeposti comments  (maoni) mamilioni na mamilioni ya ‘No reforms no election’, uchaguzi upo palepale haisaidii tukiweka posti wewe njoo weka hicho unachotaka haisaidii uchaguzi hausogezwi utafanyika kama ulivyopangwa.”

“Hiyo ni nadharia tu kujifurahisha tu kwamba eeeh kila posti mkiweka ‘No reforms no election’ jifurahisheni uchaguzi upo palepale,”amesema Makalla.

Makalla amewataka Watanzania kuwakataa wagombea watakaowagawa kwa  misingi ya dini au makabila ili uchaguzi ufanyike kwa amani.

Jana Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alipoulizwa kuhusu suala hilo alijibu “Watu wameamua kufanya hivyo, tutafanyaje,”

“Watu wajiepushe na kampeni zisizokuwa na tija, watumie mitandao kama fursa ya kujifunza teknolojia mpya, wanapaswa kutambua na kujua kutumia mitandao vibaya ni kupoteza rasilimali fedha kwa kuwa wanatumia bando,” amesema Msigwa

Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema viongozi na wanachama wa chama hicho wanatakiwa kushikamana kukivusha na kuwakataa wanataka kununua ubunge au udiwani.

“Anayetaka kununua udiwani au ubunge huyo hafai, tufanye kazi tuchague viongozi ambao watatuvusha ili kazi ya kupiga kura kusiwepo kupoteza muda , Rais ashafanya kazi yake na ilani imetekelezwa vizuri,”amesema Boisafi

“Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, wakati utakapofika ndani ya chama na baadaye kwenye Serikali tunahitaji kushikamana, kwa sasa kuna baadhi yetu wanataka kukiuka miiko ya chama chetu, tunaambiwa rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea, maneno hayo naomba tukayaishi, tukatende haki kwa wale wanaostahili kupata haki bila kumwonea mtu yoyote au kwa kutokana na fedha zake au kutokana na jambo lingine lolote,”amesema Boisafi

“Tunajitambua tena vizuri sana ninawaomba kama Mwenyekiti wenu na kiongozi wenu tutende haki na tuchukie rushwa,”amesema Boisafi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Moshi mjini(CCM) Priscus Tarimo, amesema chama hicho hakijawahi kuanguka kwa sababu ya upinzani, kinaanguka kwa sababu ya kuzungukana.

“Tunaomba utupelekee shukurani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri alizofanya lakini mimi binafsi naomba umpelekee shukurani kwa kauli yake wakati anafunga mkutano mkuu juzi, aliposema hajatuma mtu, maana kuna wanaoonyesha namba kwamba wametumwa, sasa kwa sababu hajatuma mtu uwanja upo wazi twende tukapambane,”amesema Mbunge Tarimo

“Mheshimiwa Mwenezi(Makalla) ukiwa mkuu wa Mkoa hapa Kilimanjaro mwaka 2015 mimi nikiwa Katibu Mwenezi tulichapa jaramba hapa tukapata tulichokipata na hatujawahi kuanguka kwa sababu ya upinzani, tunaanguka kwa sababu ya kuzungukana, hizi dua zilizopigwa hapa zikafukuze roho ya kuzungukana,”amesema Mbunge Tarimo

Pamoja na mambo mengine, amesema mpaka sasa Serikali imetekeleza miradi tisa kati ya 10 isipokuwa ahadi moja ya Moshi kuwa jiji.

“Rais ameleta fedha kwenye ahadi tisa zinazohitaji fedha na imebaki ahadi moja ya jiji, kwa asilimia 90 hatumdai anatudai kura zake, hatukuwa na hospitali ya Wilaya tumepewa hospitali kule kata ya Ng’ambo inayogharimu zaidi ya Sh6.5 bilioni,”amesema.

Naye, Mbunge wa Siha, Dk Godwin Mollel amesema Serikali imefanya maboresho makubwa katika sekta ya afya, ambapo tangu Rais Samia aingie madarakani vifo vimepungua kutoka 556 mpaka 104 kwa mwaka.

“Dk Samia alingia na kukuta wanawake zaidi ya 556 wanafariki kila mwaka kutokana na matatizo ya uzazi, lakini leo amewekeza miundombinu na teknolojia na akasomesha madaktari kwa muda mfupi na vifo vya akina mama vikashuka mpaka 104,”amesema Dk Mollel.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.