Dar es Salaam. Viongozi wakuu na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) n
wamejitokeza kwa wingi makao makuu ya chama hicho Mikocheni kwenye uzinduzi wa jukwaa la kidijitali la kuchangia fedha .
Fedha hizo zinazokusanywa kupitia kampeni ya ‘Tone Tone’ na ‘Tone nimo’, zinalenga kuendesha kampeni ya ‘No reforms no election’ inayosimamiwa na chama hicho baada ya mkutano mkuu uliofanyika Januari 21, 2025 kuazimia hilo.
Kampeni ya vuguvugu la azimio hilo linalosimamiwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu linalenga kuishinikiza Serikali kufanya mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi, itakayotoa fursa sawa kwa vyama vyote kushiriki chaguzi huru na zinazoheshimu kura zinazopigwa na wananchi ili kupata viongozi bora.
Hivyo, baada ya kukusanywa fedha hizo zitatumika kama gharama ya kuwafikia wananchi kupitia mikutano ya hadhara maeneo mbalimbali nchini hadi vijijini, ili kutoa elimu na kuwaelewesha maana ya vuguvugu la ‘No reforms no election’.
Kampeni hiyo itadumu kwa miezi sita na kila mwananchi anapaswa kuchangia fedha na malengo waliyojiwekea kwa kuanza ni kukusanya Sh1 bilioni.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche amesema mabadiliko wanayopigania Watanzania lazima wahusike,Chadema itakuwa taasisi imara kama haitamtegemea mtu mmoja.
Ametolea mfano wakati wa uhuru hayati Mwalimu Julius Nyerere alichangiwa na wananchi kupigania uhuru.
“Tutakuwa wawazi kwa kila senti tutakayopokea ,mtu akichangia fedha zake atahitaji kuona nini kimekwenda kufanyika, kazi yetu itakuwa ni kushughulika na CCM” amesema.
Katika maelezo yake Heche amesema Chadema ina ruzuku ya Sh100 milioni fedha ambazo hazitoshi lakini kutokana na moyo wanachama wa chama hicho kujitolea ndio maana wanakiendesha chama.
Amesema ili chama hicho kiwe cha wanachama ni muhimu kila mtu mpenda mabadiliko akichangie ili kukifanya kuwa mikononi mwa wananchi.
Naye, Mjumbe wa Kamati kuu na Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya fedha, Godbless Lema, amewataka Watanzania kwa ujumla kujitojeza kuchangisha fedha ili viongozi waendelee kufanya kazi ya kujitolea kuwasaidia kutafuta haki zao.
“Katika chama chetu makatibu wanafanya kazi kwa kujitolea na hawalipwi ni muhimu tujitokeze kwenye kampeni hii itakayodumu kwa kipindi cha miezi sita,” amesema.
Amesema kampeni hiyo inalenga kujenga utamaduni mpya wa wananchi kuchangia wenyewe huku akitolea mfano Rais wa Marekani Dornald Trump ni tajiri na anatoka chama kikubwa lakini kinachangiwa.
“Tumetengeneza kitu kinaitwa nimo na tumekiunganisha kwenye Chadema dijitali na watakuwa wanachangia moja kwa moja na malengo yetu hadi kufikia mwezi wa sita watu milioni moja wawe wamejiunga,” amesema
Lema amesema wanahitaji watu wengi wachangie kidogokidogo na katika kipindi cha muda mfupi tunataka kufisha fedha Sh1 bilion.
Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Jacob Boniface, maarufu Boni Yai amesema katika kampeni hiyo kwa mtu ambaye atahitaji michango yake itangazwe hadharani hilo litafanyika na wengine wanaotaka kuchangia chochote wanaruhusiwa.
Amesema michango hiyo ni sadaka kwani kuna watu watahatarisha maisha yao kwa kulala barabarani hivyo kila mtu ana wajibu wa kutoa mchango huo kusaidia maendeleo.
“Kampeni hii ikizinduliwa naamini Dar es Salaam ambayo ni kanda yangu itaongoza kwa makusanyo, mwenye fedha yake kidogo achangie na si lazima iwe fedha hata kama utakuwa na mafuta nitakuwa tayari kuja kuchukua,” amesema
Askofu Amandus Mwamakula amesema viongozi wa dini walifanya kazi kubwa ya kuchangia mabadiliko Afrika ikiwemo Askofu Desmond Tutu wa Afrika kusini.
“Tanzania viongozi wa dini hatuwezi kuwa nyuma kuchangia mabadiliko, wala msijifiche katika kuchangia mabadiliko ya demokrasia, kusiwe na ubaguzi katika kuchagua chama cha kuchangia” amesema.
Wageni waliohudhuria katika mkutano huo ni Lissu aliyekuwa mgeni rasmi, Makamu Mwenyekiti , John Heche, Katibu Mkuu, John Mnyika, Aman Gulangwa,(Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara), Wakili Ali Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu Zanzibar.
Wengine ni Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Jacob Bonifas, Mwenyekiti Kanda ya Magharibi, Wakili Dickson Matata, Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema na aliyekuwa Mgombea wa nafasi ya mwenyekiti Charles Odero.
Crédito: Link de origem