top-news-1350×250-leaderboard-1

Majaliwa: Dini zina mchango kuimarisha ustawi wa jamii

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema madhehebu ya dini yana mchango mkubwa katika kuimarisha ustawi wa jamii na kutoa huduma za kiroho.

Majaliwa amesema Serikali inathamini kazi kubwa inayofanywa katika maeneo mbalimbali, hususan katika kutoa huduma za kijamii na hivyo kuchangia kasi ya maendeleo ya Taifa.

Amezitaja baadhi ya huduma hizo kuwa ni za elimu, afya, maji, nishati, mafunzo kuhusu kilimo bora na ufugaji

Amesema kwa kutambua hilo, Rais Samia Suluhu Hassan wakati wote amekuwa akitekeleza kwa vitendo dhamira ya kukuza ushirikiano kati ya Serikali na madhehebu ya dini.

Majaliwa amesema hayo leo Jumamosi Mei 10, 2025 alipomwakilisha Rais Samia katika kilele cha dua maalumu ya kuombea viongozi wa kitaifa, amani, uchaguzi mkuu na kuwaombea mamufti na masheikh waliotangulia mbele za haki.

Dua hiyo imefanyika kwenye viwanja vya Msikiti wa Mohammed VI, Kinondoni, Dar es Salaam.

“Ni ukweli usiopingika sote tumeshuhudia kuwa Rais Samia Suluhu Hassan jinsi gani anawathamini, anawasilikiza na kuwashirikisha viongozi wa madhehebu ya dini katika masuala muhimu ya kitaifa,” amesema Majaliwa katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na ofisi yake.

Amempongeza Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir kwa kuandaa dua hiyo kwa ajili ya baraka na amani ya Tanzania wakati wa uchaguzi mkuu.

Tanzania inajiandaa kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

“Nikiri kwamba Serikali inatambua umuhimu wa sala na dua. Viongozi tunatekeleza majukumu yetu kwa salama kwa kuwa viongozi wetu wa dini na waumini wote mnatuombea dua. Hii ndiyo sababu Serikali imekuwa ikishirikiana na madhehebu ya dini katika shughuli zake,” amesema.

Mwenyekiti wa kamati ya dua hiyo kitaifa, Hajati Mwamtumu Mahiza amesema ni kwa ajili ya kuwaombea masheikh na mamufti walioleta mchango chanya katika dini ya Kiislamu.

Amesema dua hiyo ambayo imefanyika kwa siku tatu ililenga kuombea viongozi wakuu wa nchi na wote wanaoingia kwenye mchakato wa uchaguzi, pia kuombea amani nchini.

“Tunahitaji kuwa wanyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu anasema katika Quran kuwa niombeni nami nitawapa. Tunataka kuingia kwenye uchaguzi mkuu na kutoka tukiwa salama na wamoja,” amesema.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Alhamisi Mei 8 akifungua dua hiyo aliwasihi wananchi kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na amani kwa mustakabali mwema wa Taifa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Pia aliwataka Watanzania kujiepusha na matendo yanayoweza kuleta mgawanyiko.

Dk Mwinyi aliupongeza uongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kwa kuendeleza utaratibu wa dua ya kila mwaka na kuiombea nchi amani.

Akizungumzia kuhusu amani alisema ina umuhimu wa mkubwa katika uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu kabla, wakati na baada ya uchaguzi huo.

Alisema jukumu la kuwaombea dua masheikh, walimu na Waislamu walio hai na waliotangulia mbele ya haki na kuliombea amani Taifa ni miongoni mwa dalili za imani ya kweli kwa waumini wa dini ya Kiislamu.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.