Dodoma. Mahakama Kuu ya Tanzania imefuta maamuzi ya kumfuta uanachama na kumuondoa James Mbatia katika nafasi ya uenyekiti wa taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi, ikisema maamuzi hayo yalikuwa batili kisheria.
Mbatia alipotafutwa na gazeti hili kuzungumzia amepokeaje hukumu hiyo amesema “Ninaishukuru mahakama kwa kutenda haki. Siku zote nililalamika kuna ubatili katika uamuzi ule na leo mahakama imethibitisha. Mimi ndio mwenyekiti halali”.
Mahakama imetoa uamuzi huo wakati tayari Machi 2025 chama hicho kikiwa kimechagua viongozi wapya na Msajili wa Vyama vya Siasa kubariki safu mpya, ambapo Haji Khamis alichaguliwa kurithi mikoba ya Mbatia.
Uamuzi huo umetolewa lMei 28, 2025 na Jaji Abdi Kagomba wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma wakati akitoa uamuzi katika maombi ya mapitio ya mahakama (judicial review) aliyoyafungua dhidi ya bodi ya wadhamini ya chama hicho.
Katika uamuzi wake huo, Jaji Kagomba amesema uamuzi wowote ambayo hauzingatii haki ya asili unapaswa kufutwa hivyo mahakama inafuta uamuzi wa kumfuta uanachama na kumvua uongozi Mbatia, uliofikiwa Septemba 24, 2022.
Kupitia maombi hayo namba 18 ya 2023, Mbatia aliyewakilishwa kortini na wakili Edson Mchau, aliwasilisha maombi hayo akiomba mahakama ifanye mapitio yaliyofanywa na wajumbe wa mkutano mkuu na kuyatolea amri tatu.
Moja ni kwamba mahakama itamke kuwa uamuzi wa kumfuta uanachama na kumvua uongozi ulikiuka haki ya msingi ya kusikilizwa na kwamba sababu zilizotolewa kuhalalisha uamuzi huo, hakiwa na maana wala msingi wowote.
Pia, alikuwa ameiomba mahakama itoe amri kwa wajibu maombi ya kumzuia mjibu maombi kumfuta uanachama na kumuondoa katika wadhifa wake wa mwenyekiti wa taifa bila kuheshimu sheria za nchi na katiba ya NCCR-Mageuzi.
Akiwasilisha hoja kwa niaba ya Mbatia, wakili Mchau alisema wakati mkutano mkuu wa NCCR-Mageuzi ulifanyika Septemba 24,2022, mteja wake hakupewa taarifa yoyote hadi ilipofikia Septemba 30, 2022 alipopata taarifa ya mkutano huo.
Kwa mujibu wa wakili huyo, hiyo inaonyesha kuwa NCCR-Mageuzi walikiuka kifungu cha 6(c)(5) cha sheria ya vyama ya siasa ya mwaka 2019 na kukiuka kifungu cha 10(4) cha Katiba ya NCCR-Mageuzi kinachotoa haki ya kusikilizwa.
Wakili huyo alidai kitendo hicho kilikiuka kifungu cha 14(1) cha haki ya kiongozi kujitetea mbele ya mkutano mkuu na wakakiuka pia kifungu cha 13(6) cha Katiba ya Tanzania ya 1977 kinachotoa hakikisho la haki ya kusikilizwa.
Katika hoja ya pili, wakili huyo alisema wakati msingi wa tuhuma alizopewa mteja wake ilitokana na taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya 2019/2020, hakuna mahali popote katika ripoti hiyo ambako Mbatia ametajwa.
Alisema kulingana na kifungu cha 26(2)(a) na (b) na 26(7) cha Katiba ya NCCR-Mageuzi, mali za chama zinakuwa chini ya uangalizi na usimamizi wa Baraza la Wadhamini la NCCR-Mageuzi na sio mwenyekiti kama alivyokuwa Mbatia.
Akijibu hoja hizo, wakili Novatus Muhangwa aliyekuwa akiiwakilisha Bodi ya wadhamini ya NCCR-Mageuzi, alisema muombaji alikuwa hapingi uamuzi wa Kamati Kuu iliyoketi Mei 21, 2022 uliomsimamisha nafasi ya uenyekiti taifa.
Alieleza kuwa uamuzi wa kumsimamisha uongozi hauwezi kutenguliwa na mahakama hiyo kwa kuegemea maombi yaliyopo kwani kwa kufanya hivyo itakuwa ni sawa na kuunda kesi mpya kutoka kwenye shauri hilo.
Kuhusu hoja ya Mbatia kuwa hakupewa haki ya kusikilizwa, wakili huyo alisema kwa kutazama hoja za Mbatia, kwa upande mmoja anaeleza hakupewa nafasi ya kujitetea lakini upande wa pili hakupewa fursa ya kutosha ya kujitetea.
Wakili huyo alisema Mbatia alipewa nafasi ya kutosha ya kujitetea bila kukiukwa kwa kifungu chochote cha Katiba ya NCCR-Mageuzi au ile ya Tanzania.
Alieleza kuwa uamuzi wa kumfukuza Mbatia ulianzia kwenye kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya NCCR-Mageuzi iliyokutana Mei 21,2022 mbacho ndicho kilimsimamisha muombaji katika nafasi yake ya mwenyekiti wa taifa.
Wakili huyo alisema uamuzi wa kumsimamisha Mbatia katika wadhifa wake huo, haukuwa unatakiwa upate baraka za mkutano mkuu kama ambavyo anadai na kwamba alichotakiwa ni kuupinga uamuzi huo wa NEC ambao hakuupinga.
Kuhusu kutopata wito wa mkutano mkuu, wakili huyo alisema Septemba 20, 2022, mtu aliyetajwa kuwa ni Rajabu Kazimoto alipewa barua ili kumpelekea Mbatia, lakini Mbatia alikataa kusaini kitabu (dispatch book) akitaka atumiwe kwa email.
Wakili huyo aliirejesha mahakama katika aya ya 5 ya kiapo cha Kazimoto na kusisitza kuwa Mbatia alishaisoma barua hiyo na kubakia nayo na kwamba kwa maelezo hayo ya Kazimoto, anaamini muombaji alipata wito wa kikao.
Kulingana na wakili huyo, kama Mbatia alikuwa hakubaliani na uamuzi wa NEC, alipaswa kukata rufaa kwenye mkutano mkuu kupitia kifungu cha 23(3)(j) cha Katiba ya chama na kwamba kufungua maombi amewahisha suala hilo.
Katika uamuzi wake, Jaji alisema mahakama inawajibika kujibu maswali matatu, moja ni iwapo muombaji alinyimwa haki ya kusikilizwa kabla ya uamuzi kutolewa na mkutano mkuu uliofanyika Septemba 24,2022 na kumvua uongozi.
Swali la pili ni kama sababu zilizowafanya wajumbe kufikia uamuzi wa kumvua uongozi na kumfuta uanachama zilikuwa na uhalali na tatu kama muombaji anastahili nafuu anazoziomba kupitia maombi hayo ya mapitio ya mahakama.
“Katika shauri hili malalamiko ya muombaji yako wazi. Kwamba anapinga uamuzi wa mkutano mkuu kumvua uongozi na kumfuta uanachama. Kama wakili wake alivyosema, mteja wake hapingi uamuzi wa NEC wa kumsimamisha uongozi,” alisema
Akinukuu kiapo cha Mbatia, Jaji alisema “Muombaji anapinga maamuzi ya Mkutano mkuu wa Taifa wa Septemba 24,2022 ambao hauna uhusiano wowote na maamuzi ya NEC kwani yalimezwa (overtaken) na mkutano mkuu.”
Jaji alisema ni jambo lisilobishaniwa kuwa muombaji alikuwa mwanachama wa NCCR-Mageuzi na mwenyekiti wa Taifa na kwamba jambo linalobishaniwa ni mwaka alijiunga kuwa mwanachama, kama alijiunga 1992 au baadaye.
Kulingana na Jaji, hoja hiyo haina maana kwa kuwa pande zote mbili zinakubali kuwa muombaji alikuwa mwanachama wa NCCR-Mageuzi na mwenyekiti wa taifa kabla ya kufanyika kwa maamuzi ya kumvua uongozi na kumfuta uanachama.
“Kwa maoni yangu, kuanza kuhoji unakwenda hadi kwenye uamuzi wa mkutano mkuu. Kama asingekuwa mwanachama basi ule mkutano mkuu wa kumfukuza uanachama usingefanyika. Unamfukuzaje mtu ambaye siyo mwanachama?”alihoji.
“Baada ya kupitia kiapo cha mjibu maombi, nakubaliana na wakili Mchau kuwa mgogoro kuhusu tarehe ya uombaji kujiunga na NCCR-Mageuzi ilitoka kwa wakili kwa sababu haionekani popote kwenye kiapo cha mjibu maombi,” ameeleza Jaji.
Kuhusu iwapo Mbatia alivyimwa fursa ya kusikilizwa, Jaji alikubaliana na hoja za wakili Mchau kwamba wajibu wa kuthibitisha kama alipewa haki hiyo ni la wajibu maombi kwa sababu mleta maombi analalamika kuwa hakupewa haki yao.
Jaji alisema hoja ya wajibu maombi ni kuwa Mbatia alipelekewa barua akakataa kuipokea lakini ushahidi unaonyesha alipokea wito huo Septemba 30,2022 kwa njia ya EMS, ikiwa ni siku tano baada ya Mkutano mkuu kufanya maamuzi.
“Matokeo yake ni kuwa huu utetezi wa wajibu maombi kuwa mleta maombi alipelekewa wito wa kuitwa kwenye mkutano kujitetea haukuthibitishwa. Kwa hiyo wajibu maombi hawakutimiza wajibu wao wa kuthibitisha suala hilo,” amesema.
Akinukuu vifungu mbalimbali vya Katiba ya NCCR-Mageuzi, Jaji alisema Katiba ya chama hicho inampa haki mleta maombi kupewa nafasi ya kujitetea, lakini kwa kuwa katiba haikuzingatiwa, ni wazi Mbatia hakusikilizwa kabla ya uamuzi.
Kuhusu maombi ya Mbatia, Jaji amesema Aprili 7, 2025, NCCR-Mageuzi iliijulisha mahakama kwa barua kuwa Machi 29 na 30, 2025, chama hicho kilikuwa kimefanya uchaguzi wa viongozi wapya ikiwamo nafasi ya mwenyekiti wa taifa.
Katika barua hiyo, walikuwa wamemjulisha Msajili wa vyama vya siasa ambaye alibariki mabadiliko hayo ya uongozi na nyaraka kuhusiana na mkutano huo na majina ya viongozi wapya ziliambatanishwa na barua hiyo kwa mahakama.
Kuhusu mahakama kujulishwa kwa barua, wakili Jeremiah Mtobesya aliyekuwa katika timu ya mawakili wa Mbatia alipinga utaratibu huo akisema mahakama ikishapanga tarehe ya uamuzi, hakuna jambo jipya linaweza kuingizwa.
Mtobesya alijenga hoja maombi ya mteja wao hayajapitwa na wakati kwa kuwa maombi ya mteja wao ni kupitiwa kwa uamuzi uliofanywa na mkutano mkuu wa NCCR-Mageuzi hivyo mahakama imefungwa mikono kushughulikia jambo jipya.
Hata hivyo Jaji amesema kwa kuwa bado kulikuwa hakuna uamuzi wowote uliotolewa, mahakama ndio yenye mamlaka kamili na shauri hilo lakini akakubaliana na hoja za wakili Mtobesya kuwa korti haiendeshwi hivyo.
Jaji amesema uamuzi wa wajumbe wa mkutano mkuu wa NCCR-Mageuzi ulikiuka kanuni za haki ya msingi hususan kunyimwa haki ya kusikilizwa na kwamba hilo lilikiuka Katiba ya Tanzania Ibara ya 13(6) na Katiba ya NCCR-Mageuzi.
“Kwa kuwa ni msimamo wa sheria kuwa uamuzi unaotolewa bila kuzingatia misingi ya haki ya asili ni lazima ufutwe hata kama uamuzi huo unakuja baada ya mtu kusikilizwa,” ameeleza Jaji Kagomba katika hukumu yake na kuongeza kuwa:-
“Natoa amri ya kufuta uamuzi wa mkutano mkuu wa NCCR-Mageuzi wa Septemba 24, 2022 uliomfuta uanachama mleta maombi na kumuondoa katika nafasi ya mwenyekiti wa taifa kwa kuwa ni maamuzi yaliyokwenda kinyume na sheria.”
“Huwezi kumuondoa mleta maombi bila kumpa haki ya kusikilizwa,”alisisitiza Jaji na kueleza kuwa hawezi kutoa amri ya kuwazuia wajibu maombi kumuondoa kwenye wadhifa wake kwa kuwa itakuwa ni kubashiri jambo ambalo halijatokea.
Mahakama imeiamuru bodi ya wadhamini NCCR-Mageuzi kulipa gharama za kesi
Crédito: Link de origem