top-news-1350×250-leaderboard-1

Mahakama ‘yamtia hatiani’ Selasini kisa Mbatia

Dar es Salaam.  Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imemuamuru Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi, Joseph Selasini kumuomba radhi mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, James Mbatia kwa kosa la kumkashfu.

Mahakama hiyo imemuamuru Selasini kumuomba radhi Mbatia kwa tuhuma alizozitoa dhidi yake za ubadhirifu wa mali za chama.

Alidai kuwa, aliuza mali za chama hicho na baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2020, alifanya ushawishi kwa Rais ili ateuliwe kuwa mbunge.

Selasini ameamuriwa kumuomba radhi Mbatia kwa kauli hizo za kashfa, kupitia vyombo vya habari vya Mwananchi Digital na Wasafi Media.

Pia, Mahakama hiyo imemuamuru Selasini, mbunge wa zamani wa Rombo, kumlipa Mbatia, mbunge wa zamani wa Vunjo, fidia ya madhara ya jumla ya Sh10 milioni kwa kosa hilo.

Vilevile imeziamuru Kampuni za Mwananchi Communications Ltd, inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti na kuendesha mitandao ya kijamii pamoja na Kampuni ya Wasafi Media kumlipa Mbatia fidia ya Sh10 milioni kila moja kwa kuchapisha maneno ya kashfa aliyoyatoa Selasini kwa Mbatia.

Mbali na kiasi hicho cha fidia, Mahakama hiyo pia imewaamuru Selasini, MCL na Wasafi kumlipa Mbatia riba ya asilimia saba ya kiasi hicho cha fidia kuanzia tarehe ya hukumu mpaka tarehe ya kukamilisha malipo yote ya fidia hiyo, pamoja na gharama za kesi alizozitumia Mbatia.

Amri hizo zimetolewa na Jaji Awamu Mbagwa katika hukumu yake ya Februari 28, 2025, iliyotokana na kesi ya madai ya kashfa aliyoifungua Mbatia dhidi ya Selasini.

Mbali na Selasini wadaiwa wengine katika kesi hiyo ya madai namba 59/2023 ni kampuni na watendaji na wamiliki wa vyombo vya habari kutokana na vyombo hivyo kuripoti kile alichokisema Selasini katika mkutano wake na vyombo vya habari.

Wadaiwa hao wengine walikuwa ni MCL, Mhariri wa Gazeti la The Citizen, Jamhuri Media Limited (kampuni inayochapisha gazeti la Jamhuri), Global Publishers and General Enterprises Limited na Nasibu (Naseeb) Abdul Juma (Diamond Plantinamuz), anayefanya shughuli zake kwa jina la Wasafi TV.

Mbatia ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa NCCR-Mageuzi tangu Julai Mosi, 1992 akiwa na kadi ya uanachama namba 000006, alikuwa mwenyetiki wa chama hicho Taifa mpaka alipovuliwa uanachama Septemba 24, 2022.

Ndiye aliyemkaribisha Selasini katika chama hicho na kumteua katika kamati ya utendaji ya chama hicho.

Katika kesi hiyo, Mbatia alidai kwa nyakati na maeneo tofati jijini Dar es Salaam na Dodoma, Selasini huku akijua alitoa taatifa za uwongo na za kashfa dhidi yake, zilizoharibu hadhi, zilizochapishwa na kusambazwa na vyombo hivyo vya habari.

Kwa mujibu wa hati ya madai, Selasini katika mkutano wake huo na vyombo vya habari ulifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jesho la Wokovu, Kurasini, Temeke, Dar es Salaam, Mei 21, 2022.

Katika mkutano huo Selasini alisema baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Mbatia alianza kufanya ushawishi ili aweze kuteuliwa na Rais kuwa mbunge katika viti 10 vya Rais, na Rais alimkatalia na ndipo Mbatia akaanzisha vita na Rais.

Septemba 24, 2022  Selasini akiwa katika ukumbi wa mikutano wa St, Gaspar jijini Dar es Salaam, bila haki na kwa nia ovu alitoa taarifa za kumhusisha na ubadhirifu wa mali za chama zilichapishwa na kusambazwa na Mwananchi Digital. 

Mei 2022 Selasini katika mahali pasipofahamika alisambaza taarifa za uwongo na za kashfa dhidi yake kwa umma kuwa Mbatia alipokea pesa kutoka kwa hayati Rais John Magufuli, Sh500 milioni.

Mei 26, 2022, Selasini akiwa Sinza Manispaa ya Ubungo alifanya mkutano na vyombo vya habari ambao ulirushwa na Global TV Online, alirudia kutoa taarifa za uwongo kuwa kulingana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Mbatia aliuza mali za chama.

Selasini alizitaja mali hizo ni shamba la Karege, Bagamoyo lenye ukubwa wa ekari 56, nyumba mbili zilizoko Bunju na nyingine moja Tarime.

Septemba 2, 2022 MCL ilichapisha taarifa za uwongo na za kashfa katika Gazeti la The Citizen zilizohaririwa na mdaiwa wa tatu (Mhariri wa The Citizen) kuwa Mbati alihusika kuuza mali za chama yakiwamo mashamba na nyumba sehemu mbalimbali za nchi iliyoripotiwa na The Citizen.

Oktoba 12, 2022 Wasafi kupitia chaneli yake ya Youtube ilifanya mahojiano na Selasini aliyedai Mbatia aliuza mali za chama likiwamo shamba la ekari 59, lililoko Kiromo.

Katika hati hiyo ya madai, Mbatia aliyewahi mwenyekiti wa chama hicho kabla ya kuvuliwa uanachama wa chama hicho, Septemba 24, 2022, aliyanukuu maneno hayo aliyoyatamka Selasini katika mikutano yake hiyo kwa nyakati na mahali tofauti.

Kwa kuzingatia taarifa hizo, alidai kuwa hadhi yake kama mtu maarufu katika jamii iliharibiwa.

Hivyo, aliiomba Mahakama itamke itoe hukumu ya tamko kwamba taarifa zilizosambazwa na wadaiwa ni za uwongo na za kashfa; kwamba zilishusha hadhi yake kwa familia yake, kwa kazi yake kama mwanasiasa anayeheshimika, na kwa ulimwenguni kwa jumla.

Pia, aliiomba Mahakama itoe amri kuwalazimisha wadaiwa kumuomba radhi kupitia vyombo vya habari, kwa taarifa hizo za uwongo na za kashfa walizozisambazaa dhidi yake, iamuru wadaiwa kwa umoja na kwa mmoja mmoja walimpe fidia ya Sh10 bilioni.

Vile aliomba Mahakama iamuru wamlipe Sh1 bilioni kama fidia ya madhara ya jumla kwa athari za kiakili na kisaikolojia aliyoyapata, iamuru wadaiwa wazifute taarifa hizo katika tovuti, mitandao ya kijamii, blogs magazetini na chaneli za Youtube.

Amri nyingine alizoziomba Mbatia ni zuio la kudumu dhidi ya wadaiwa na mtu yeyote anayefanya kazi chini ya mamlaka yao kuendelea kusambaza taarifa hizo za uwongo na za kashfa dhidi yake.

Mbatia pia aliomba alipwe riba ya asilimia 12 kwa malipo ya fidia aliyoyaomba, gharama za kesi na nafuu nyinine ambazo Mahakama itaona zinafaa.

Awali, Selasini baada ya kupewa nyaraka za kesi hiyo katika majibu yake alikana madai ya Mbatia na alisisitiza kuwa, taarifa alizosema ni za kweli.

Wadaiwa wengine wakikiri kuchapisha taarifa hizo lakini wakakana kuwajibika kwa madai kuwa waliripoti kile kilichozungumzwa na Selasini katika mikutano ya chama hicho.

Hata hivyo, baada ya usikilizwaji wa pande zote, Mahakama hiyo katika uamuzi wake imeamuru kuwa mdai, Mbatia ameweza kuthibitisha sehemu ya madai yake dhidi ya wadaiwa watatu.

Imebainisha kuwa, Mbatia amethibitisha sehemu ya madai yake dhidi ya Selasini kuwa alitoa taarifa za kashfa na MCL na Wasafi kwa kusambaza taarifa hizo bila kumpa nafasi mdai, Mbatia ya kujibu tuhuma hizo dhidi yake.

Kuhusiana na madai ya fidia ya Sh10 bilioni kama fidia ya hasara halisi, Mahakama imesema kuwa hakuweza kuthibitisha fidia ya kiasi hicho cha pesa.

Kuhusiana na madai ya malipo ya fidia ya madhara ya jumla, Mahakama katika uamuzi wake imeamuru alipwe fidia ya Sh10 milioni kwa kila mdaiwa ambaye amethibitisha madai dhidi yake.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.