Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa amesema watatafuta kila namna kupata rasilimali fedha zitakazowawezesha kujenga makasha ya mahakama mtandao kwenye magereza yote nchini ifikapo mwaka 2027.
Bashungwa ameyasema hayo leo Machi 21, 2025 wakati akikabidhiwa makasha mtandao 10 yaliyotengenezwa na Mahakama Tanzania.
Amesema kutumika kwa makasha hayo kutakuwa ni daraja litakalounganisha mahabusu na haki huku yakisaidia kupunguza gharama za usafiri na maaharisho ambayo yangeweza kutokea kutokana na kutofikishwa kwa mahabusu mahakamani.
Amesema pia mahakama mtandao inarahisisha upatikanaji wa huduma za kimahakama, kuokoa gharama za uendeshaji, kupunguza msongamano wa wananchi mahakamani, kuwezesha mahakimu kupata rejea za hukumu na nyaraka mbalimbali kwa urahisi na kuwabaini mawakili vishoka ambao wamekuwa wakiharibu mwenendo wa kesi.
“Yatahakikisha ulinzi wa taarifa na nyaraka pamoja na kuokoa muda wa wananchi katika utafutaji wa haki badala yake muda mwingi kuutumia katika shughuli za uzalishaji, hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania,” amesema.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel amesema wamegawa makasha hayo kwa magereza 10 ikiwemo matatu ya jijini Dar es Salaam ambayo ni Ukonga, Segerea na Keko, Uyui (Tabora), Isanga (Mbeya na Dodoma), Butimba (Mwanza), Maweni (Tanga) na Kisongo (Arusha).
“Kilichofanyika hapa mheshimiwa Jaji ama Hakimu hana haja ya kuwapokea wafungwa kule mahakamani, badala yake mifumo ya Tehama inatumika kufanya kazi hii. Jaji atakapokuwa pengine yuko Dar es Salaam,”amesema.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa akikata utepe kama ishara ya kupokea makasha ya mahakama mtandao. Hafla hiyo ilifanyika katika Gereza Kuu la Isanga Mkoani Dodoma.
“Bukoba ama Mwanza anaweza kushughulikia mahabusu ama mfungwa aliyeko mahabusu ya Isanga Dodoma bila jaji kusafiri ama mfungwa kusafirishwa,”amesema.
Amesema mahakama imefanya kama alama tu ya kuonyesha kuwa jambo hilo linafanyika kwa namna gani na kuwa kontena moja lenye futi 20 kulinunua tu lenyewe ni kati ya Sh6 milioni na Sh7 milioni.
Profesa Gabriel amemuomba Bashungwa kuhakikisha wadau wengine wanachangia katika ununuzi na utengenezaji wa makasha hayo kwa kuwa nia ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona kuwa haki inayendeka kwa gharama nafuu na mwenye haki apate haki.
Pia, amesema kupitia makasha hayo wafungwa na mahabusu sasa wataweza kutoa malalamiko yao katika Kituo cha Huduma kwa Wateja cha Mahakama ya Tanzania kuhusu kesi zilizowapeleka katika magereza.
Aidha, amesisitiza utunzaji wa makasha hayo na kuyatumia na kuwa wataendelea kutoa ushirikiano mahali patakapohitajika ili shughuli hiyo iweze kwenda kwa kasi na kuleta manufaa.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP), Jeremiah Katundu amesema kuna jumla yanmagereza 129 Tanzania Bara yenyenuwezo wa kuhifadhi jumla ya wahalifu 29,902 kwa siku lakini 26,917 na kuwa idadi hiyo no ndogo ukilinganisha na uwezo wa kuhifadhi wahalifu.
Amesema hayo ni matokeo ya uboreshwaji wa huduma za haki jinai unaofanywa na Serikali ya awamu ya sita lakini ushirikiano mzuri uliopo baina ya vyombo vya mnyororo wa haki jinai.
“Tunashukuru mahakama ya Tanzania kwa kufanikisha huduma ya mahakama mtandao.kwa sasa magereza takribani 66 yana mahakama mtandao.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama Profesa Elisante Ole Gabriel akimkabidhi Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Jerehemiah Katundu ufunguo kama ishara ya kukabidhiwa makasha ya mahakama mtandao.
“Vilevile katika bajeti ya jeshi mwaka huu 2024 /25 zilitengwa Sh1.3 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitakavyotumika kwa ajili huduma ya.mahakama mtandao magerezani,” amesema.
Amesema wameshapokea Sh696.8 milioni ambapo mchakato wa ujenzi uko katika hatua za awali.
Aidha, amesema jeshi limeingia makubaliano na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa ajili ya kufunga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika vituo 96 vya Jeshi la Magereza kwa gharama ya Sh1.3 bilioni.
Pia, vituo 26 vimeingizwa katika mradi wa Taifa wa kidigitali ambapo vitaunganishwa na Mkongo wa Taifa pamoja na kupatiwa vifaa vitakavyotumika kwa.ajili yamkuendesha shughuli za mahakama mtandao.
Crédito: Link de origem