top-news-1350×250-leaderboard-1

Maduka 19 ya kuuza mbegu matatani, Morogoro

Morogoro. Taasisi ya kudhibiti ubora wa mbegu nchini (TOSCI) imeweka zuio kwenye maduka 19 ya mbegu baada ya kukutwa yakiuza mbegu za mbogamboga zisizokuwa na  lebo iliyotolewa na taasisi hiyo.

Hivyo taasisi hiyo imeelekeza kuwa  maduka hayo yasifunguliwe hadi yatakapokidhi vigezo vya uuzaji wa mbegu hizo.
Hatua ya kuweka zuio kwenye maduka hayo imekuja leo Juni 10, 2025 baada ya wakaguzi wa mbegu kutoka TOSCI makao makuu mkoani Morogoro kufanya ukaguzi kwenye maduka ya pembejeo, ambayo pia yanauza mbegu za mazao mbalimbali zikiwemo za mbogamboga.

Mkaguzi kutoka TOSCI, Nugwa Fortunatus amesema wakulima na wafanyabiashara wa mbegu nchini wametakiwa kutambua na kutumia mbegu zenye lebo ya ubora wa mbegu inayotolewa na taasisi hiyo  ili kupanda mbegu bora na kuwa na uhakika wa mavuno.

“Kwa sasa mbegu zote za mbogamboga na nafaka zinawekwa lebo ya kuthibitisha ubora wake  ambalo wakulima wanapaswa kulizingatia wanaponunua mbegu hizo ili kuepuka kupata zisizo na ubora,” amesema Nugwa.

Nobert Lugonza ambaye ni mmoja wa timu ya wakaguzi kutoka TOSCI amesema mbegu bora lazima iwe na lebo ya ubora ambayo itakuwa na sehemu ya kukwangua kama vocha, itakayomuonesha mkulima namba ya kumpa majibu yenye ubora na uhakika wa mbegu husika.

Amesema mbegu yoyote ambayo haina sehemu hiyo ya kukwangua na kukuletea ujumbe wa ubora, hiyo sio bora na hivyo amewataka wakulima kuwa makini wanapokwenda kununua.

Mmoja wa wauzaji wa maduka ya mbegu kutoka mtaa wa John Mhenge mkoani Morogoro, Amani Mushi ameishukuru TOSCI kwa kuweka utaratibu wa lebo za kudhibitisha ubora wa mbegu kwa sababu tangu wawaletee lebo hizo wamekuwa na uhakika wa biashara.

Naye mkulima wa mbogamboga kutoka Mgeta, Prosper Mkunule amesema kukosekana kwa ubora wa mbegu husababisha mazao hayo ya mbogamboga kushindwa kustawi na wakati mwingine kushindwa kuota kabisa, jambo ambalo ni hasara kwao.

“Kilimo cha mbogamboga kinatumia fedha nyingi kuliko kilimo cha mazao ya nafaka, mtu anaweza akalima mahindi au mpunga kwa kutumia mbegu aliyohifadhi ndani tangu mwaka juzi na akavuna, lakini kwa sisi wakulima wa mbogamboga lazima tutumie mbegu bora za kununua madukani hivyo tukipata isiyokuwa bora hapo hatuwezi kuvuna hata kidogo,” amesema Mkunule

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.