Liwale. Katika kukabiliana na changamoto ya wanyamapori waharibifu na wakali katika vijiji 64 kati ya 76 vilivyopo Liwale, Serikali kupitia Mamlaka ya Wanyapori Tanzania (Tawa) wamekuja na matumizi ya teknolojia ya ndege nyuki (drone) ili kuwadhibiti wanyama hao hasa tembo.
Hayo yamebainishwa leo Mei 30, 2025 na Mhifadhi wa Wanyamapori Wilaya ya Liwale, Philipo Orio wakati akiwasilisha taarifa yake ya mradi wa matumizi ya teknolojia ya ndege nyuki mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ally Ussi.
Amesema Wilaya ya Liwale imepatiwa ndege nyuki tatu zenye thamani ya Sh62 milioni ili kukabiliana na wanyamapori hao hasa tembo ambao wamekuwa wakifanya uharibifu wa mali za wananchi na pia kuwajeruhi.
Orio amesema ndege nyuki hizo zimesaidia kufukuza na kudhibiti makundi ya tembo 11 yenye zaidi ya tembo 220 ambao walikuwa wanafanya uharibifu kwenye maeneo ya makazi na mashamba ya wananchi katika vijiji vya Ngumbu, Mirui, Naujombo Mtungunyu, Ngunja na chigugu.
“Tutafanya kazi kwa ufanisi mkubwa kutokana na matumizi ya teknolojia hii ndege nyuki kwani tembo adui yake mkubwa ni nyuki na hizi droni zina mlio wa nyuki, hivyo hawataweza kuingia mara kwa mara kwenye makazi na mashamba ya watu,” amesema Orio.
“Hizi ndege nyuki tumezitoa katika maeneo ya kituo cha Selous Liwale na Tanapa na kufanya Wilaya ya Liwale kuwa na ndege nyuki tatu,” amesema.
Ameongeza kuwa ndege hizo zina uwezo wa kusafiri umbali wa kilomita 15 kwa eneo ambalo halina vizuizi kama milima na upepo mkali na pia zinafanya kazi usiku na mchana.
Mhifadhi kutoka Tawa, Peter Lema amesema wameanza kutumia ndege nyuki tangu Machi 2025 ambapo walikuwa wanatumia ndege hizo kwa kufukuza tembo na wanyama wakali, amesema kabla ya ndege nyuki walikuwa wanatumia njia ya risasi, pilipili na mabomu ya mshindo mkubwa.
“Mwanzoni tulikuwa tunawakabili tembo kwa kiwapiga risasi, mabomu yenye mshindo mkubwa pamoja na pilipili lakini sasa hivi tumepata ndege nyuki tutafukuza tembo kwa wepesi kabisa,” amesema Lema.
Mkazi wa Liwale, Zuhura Ng’ambe amesema tembo wamekuwa wakiharibu mazao yao na ameshukuru ujio wa ndege nyuki ili kusaidia kuondoa wanyama hao.
“Tunashukuru Serikali kutuletea hii teknolojia ya ndege nyuki, matumaini yangu ni kwamba hawa wanyama tembo wataondoka kwenye maeneo ya watu na kuishi kwa amani na mazao yetu tutaweza kuvuna,” amesema Ng’ambe.
Kwa upande wake, kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Ismail Ally Ussi amewataka wananchi wasichukue jukumu la kuua tembo kwani wakifanya, hivyo watafanya tembo hao kuondoka.
“Niwaombe wananchi wenzangu tusiwaue wanyama wetu, tembo, kwani tunapowaua wataondoka wakati tunawahitaji,” amesema Ussi.
Ndege nyuki hizo zinarushwa bila rubani wakati zinaongozwa kutoka ardhini kwa kutumia vifaa maalumu (remote control).
Mwenge wa uhuru umekagua, kuzindua na kuona miradi sita yenye thamani ya Sh1 bilioni ambapo umekimbizwa kilomita 165 katika Wilaya ya Liwale mkoani Lindi.
Crédito: Link de origem