top-news-1350×250-leaderboard-1

Kijana alivyoepa kifungo akishinda rufaa mbili bila wakili

Musoma. Kijana Focus Malindi (23) aliyefungwa miaka 30 na kutakiwa kumlipa fidia ya Sh1 milioni kikongwe wa miaka 81 kwa madai ya kumbaka, ameendelea kumshinda Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) mara mbili katika hatua ya rufaa.

Alipokamatwa Mei 12, 2021 katika Kijiji cha Nyakatende wilayani Musoma kwa tuhuma za kumbaka kikongwe huyo, alikuwa na umri wa miaka 19. Katika rufaa iliyokatwa na DPP, amejitetea mwenyewe kortini na ameshinda.

Ni mara ya pili anamshinda DPP, ya kwanza ikiwa Agosti 26, 2022 mbele ya Jaji Frank Mahimbali alipokata rufaa kupinga adhabu hiyo.

Sasa ameshinda mbele ya jopo la majaji watatu wa mahakama ya rufani katika rufaa iliyokatwa na DPP.

Hukumu ya jopo la majaji Dk Mary Levira, Benhaji Masoud na Deo Nangela imetolewa leo Machi 27, 2025. Katika hukumu ya rufaa iliyokatwa na DPP, wameeleza Jamhuri haikuthibitisha shtaka hilo.

Awali, kijana huyo alitiwa hatiani akahukumiwa adhabu ya kifungo na kutakiwa kumlipa kikongwe huyo fidia ya Sh1 milioni akidaiwa Mei 12, 2021 alitenda kosa hilo, baada ya kumkimbiza mwanamke huyo alipotoka shamba na wakati huo akiwa ametoka kuoga kisimani.

Mashahidi wa Jamhuri walidai kikongwe huyo alipokuwa njiani kurudi nyumbani, alikutana na mrufani akiwa ameshika panga. Ilidaiwa alimshambulia, kurarua nguo alizovaa na kwa kutumia nguvu akambaka mara mbili.

Mshtakiwa alikamatwa saa 4:00 usiku siku hiyohiyo, kikongwe siku iliyofuata alipelekwa hospitali na daktari akathibitisha sehemu zake za siri zilikuwa na michubuko. Mshtakiwa alifikishwa mahakamani mwezi mmoja baadaye.

Katika mahakama, chini ya kiapo, alikiri kukamatwa Mei 12, 2021, alidai alipigwa na kulazimishwa kukiri kumbaka kikongwe huyo, lakini alikana tuhuma hizo akiwa kortini.

Mahakama ya Wilaya Musoma baada ya kusikiliza ushahidi wa pande mbili, ulifikia hitimisho kuwa Jamhuri imethibitisha shtaka pasipo kuacha shaka, ikamtia hatiani na kumhukumu kifungo na fidia ya Sh1 milioni.

Alivyoshinda mara ya kwanza

Baada ya kuhukumiwa, hakuridhishwa na uamuzi huo akakata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, akipinga kutiwa hatiani na adhabu aliyopewa.

Rufaa ya Focus Malindi dhidi ya DPP ilisikilizwa na Jaji Mahimbali aliyekubali sababu za rufaa na kuamuru kubatilishwa kutiwa kwake hatiani na adhabu, akaamuru aachiwe huru.

Katika hukumu aliyoitoa Agosti 26, 2022 Jaji Mahimbali alisema upande wa mashitaka (DPP) haukuwa umethibitisha shtaka pasipo kuacha shaka kwa vile mwathirika alishindwa kuithibitishia mahakama kama aliingiliwa sehemu zake za siri au la.

Jaji alisema hicho ni kipengele muhimu katika kosa la kubaka, hivyo anaona hakuna uthibitisho wa kutendeka kosa hilo.

DPP hakuridhishwa na hukumu ya Jaji Mahimbali iliyomwachia huru Malindi, hivyo kupitia rufaa ya jinai namba 542 ya mwaka 2022, akawasilisha sababu za rufaa akisema mahakama iliyomwachia ilikosea kisheria na kimantiki.

Wakati rufaa ilipoitwa kusikilizwa mbele ya majaji watatu, DPP aliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Monica Hokororo, wakati mrufani, Malindi alisimama mwenyewe kortini.

Wakili Hokororo alisema mahakama ilikosea kisheria kwa maelezo mwathirika hakuthibitisha kubakwa, akairejesha mahakama ukurasa wa tisa wa nyaraka za rufaa.

Alisema katika ukurasa huo, ni jambo lililo wazi kuwa kikongwe huyo alisema alibakwa na mrufani, akieleza kwa kutolewa madai hayo, yalitosha kumaanisha kitendo cha udhalilishaji kilitendeka.

Hokororo alieleza ushahidi wa mwathirika uliungwa mkono na shahidi wa pili na wa tatu kwa sababu, wa pili alieleza alimuona mrufani akimkimbiza bibi, baadaye bibi akamweleza shahidi amebakwa na Focus.

“Hapohapo wakati akimweleza shahidi wa pili, alimtaja mrufani kuwa ndiye mhusika. Ushahidi wa mwathirika uliaminika hasa ikizingatiwa aliweza kumtaja aliyemfanyia kitendo hicho katika hatua na nyakati za mwanzo kabisa. Ni wazi kuwa mahakama ya rufaa ya mwanzo ilichukua mtizamo usio sahihi ulioifanya ikafikia kumwachia kimakosa mrufani,” alisema.

Mrufani akijibu wasilisho hilo, aliiambia mahakama alikamatwa saa 4:00 usiku kwa tukio lililotokea saa 4:00 asubuhi na baada ya kukamatwa, alipelekwa moja kwa moja nyumbani kwa mwathirika.

Alidai akiwa hapo, alipigwa kisha akapelekwa polisi na katika ushahidi wa shahidi wa tatu wa Jamhuri anakubali walimpeleka kwa bibi huyo lakini hakuiambia mahakama kwa nini hawakumpeleka moja kwa moja polisi.

Pia aidai wakati tukio linadaiwa kutokea Mei 12, 2022 saa 4:00 asubuhi, mwathirika hakupelekwa hospitali kuchunguzwa hadi siku iliyofuata, akahoji ni kwa nini ilikuwa hivyo kama kweli bibi huyo alibakwa.

Hoja ya tatu alisema askari polisi aliyepeleleza kesi hiyo hakuitwa na Jamhuri kutoa ushahidi na kwa maoni yake, yeye ndiye mtu sahihi ambaye angeweza kuiambia mahakama nini aliona katika uchunguzi na ukweli wa tukio lenyewe.

Majaji katika hukumu walisema jambo linalohitaji majibu ni kama kulikuwa na ucheleweshwaji wa kumfikisha mtuhumiwa mahakamani baada ya kukamatwa, kama upo ni nani anaweza kuelezea sababu na muda halisi?

Baada ya majaji kuibua hoja hiyo, Wakili Hokororo alikiri hilo na kwa kuangalia kumbukumbu za mwenendo wa kesi kuhusu siku aliyokamatwa na siku aliyofikishwa mahakamani, kuna tofauti ya mwezi mmoja.

Hata hivyo, Hokororo alisema ingawa ucheleweshaji huo ni kinyume cha kifungu cha 32 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), hilo halikuathiri haki ya mtuhumiwa kwa kuwa mwisho wa siku alifikishwa mahakamani.

Vilevile pamoja na kukiri mpelelezi ambaye hakuitwa kutoa ushahidi angekuwa shahidi bora kufafanua ucheleweshwaji huo, alisema hilo halikuwa na athari kwani Jamhuri ilithibitisha shtaka bila kuacha shaka yoyote.

Majaji walisema hoja ya msingi inayopaswa kujibiwa ni ucheleweshwaji wa mtuhumiwa kufikishwa mahakamani na kueleza kuwa rekodi zilizopo zinaonyesha alikamatwa Mei 12, 2021 lakini akafikishwa kortini kusomewa shitaka Juni 9, 2021.

Kwa mujibu wa majaji, kutokutolewa maelezo ya ucheleweshwaji huo kunaibua maswali mawili. Mosi, kitendo kama hicho kinaleta dhana ya hukumu ya haki? na pili ni mjibu rufaa (Focus Malindi) hakubaguliwa na kitendo kama hicho?

Majaji katika hukumu wamesema kanuni inataka kila mtuhumiwa anastahili kusikilizwa kwa haki, kasi na ufanisi na kwamba, hiyo ni kama pacha katika haki zake za msingi. Hivyo, kukiukwa kwa haki hizo bila maelezo yoyote ni kukiuka haki za msingi za mhusika.

“Katika mamlaka yetu, haja ya kuhakikisha kuwa mfumo wetu wa haki jinai unatoa hakikisho la uharaka katika mchakato wa haki, na wa haraka umewekwa katika kifungu cha 32 cha CPA. Inataka mtu afikishwe kortini haraka iwezekanavyo.

“Tukikisoma hicho kifungu na kutazama rufaa iliyopo mbele yetu, hakuna kilichofanyika kuhusu mrufani na hakuna sababu iliyotolewa na upande wa mashitaka wakati wa usikilizwaji kuhusu matakwa ya kifungu hicho,” imesema hukumu.

“Sisi tunaona kwa vile mshtakiwa hakuwa na wakili, ulikuwa ni wajibu wa upande wa mashtaka kuisaidia mahakama kuhakikisha haki za mtuhumiwa za usikilizwaji wa haki zinalindwa, ikiwamo kutoa sababu kwa nini hakushtakiwa kwa wakati,” inasema hukumu ya majaji.

Majaji hao wamesema kutotolewa kwa maelezo kwa nini kulikuwa na ucheleweshaji katika kumfikisha mrufani mahakamani kwa wakati, kunafanya kuwepo kwa makusudi ya kuvunja haki zilizopo katika kifungu cha 32 cha CPA.

Kuhusu kama upande wa mashtaka ulithibitisha kesi dhidi ya mrufani katika Mahakama ya Wilaya ya Musoma, majaji walisema kwanza, mshtakiwa hakufikishwa mahakamani kwa wakati kama kifungu cha 32 kinavyotaka.

Pili, majaji wakasema katika utetezi wake wakati anadodoswa na mawakili wa upande wa mashtaka alieleza alikuwa na mgogoro na mtoto wa kiume wa mwathirika katika shauri hilo, lakini hakuna mahali popote ilifanyiwa kazi.

Tatu, majaji wamesema katika wasilisho lake, mrufani alisema upande wa mashtaka ulishindwa kumuita ofisa wa polisi aliyepeleleza tukio hilo lakini DPP akasema upande wa mashtaka haufungwi katika kuita idadi ya mashahidi.

Ni maoni ya majaji hao kuwa, kwa kuwa kulikuwa na ucheleweshaji wa kumfikisha mtuhumiwa kortini kwa wakati, mtu pekee ambaye angeondoa giza hilo kwa upande wa mashtaka ni polisi aliyepeleleza kesi hiyo.

Katika hitimisho lao, majaji wamesema kwa kuwa mpelelezi wa kesi hakuitwa kama shahidi kutoa upelelezi ikizingatiwa mrufani alicheleweshwa kufikishwa kortini bila maelezo, upande wa mashitaka unaacha maswali.

Majaji wamesema katika mashauri ya jinai, shaka yoyote inayojitokeza katika hadithi za upande wa mashtaka, mshtakiwa ndiye anayepewa faida ya shaka hiyo. Kutokana na hilo, wamesema kwa shaka hiyo, shtaka la ubakaji halikuthibitishwa.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.