top-news-1350×250-leaderboard-1

Kengele ya hatari wanaolala saa chache

Geita. Katika dunia ya sasa iliyojaa starehe,matumizi ya  vifaa vya mawasiliano, usiku ni kama umepoteza jukumu lake la asili.

Wakati kiasili, usiku ni muda wa kupumzika, hivi sasa muda huo ndio unaotumika kwa wengi kufanya starehe. 

Ukiondoa kundi hili, lipo kundi jingine ambalo usiku ndio muda mwafaka wa kukesha wakicheza na vifaa vyao vya mawasiliano hasa simu za mkononi.Asipokuwapo WhatsApp, utamkuta Instagram au TikTok na mitandao mingine ya kijamii.

Lakini sio wafanyao starehe na watumia mitandao pekee, wapo wanaotumia usiku kama muda wa kufanya shughuli za kimaisha.

Hata hivyo, wasichokijua hali hii inaweza kuwagharimu kiafya kwa kukosa usingizi wa kutosha hivyo kujikuta wakikabiliwa na msongo wa mawazo, matatizo ya moyo na hata kupungua kwa kinga ya mwili.

Ushuhuda wanaolala muda mchache

John Kapaya, dereva bodaboda wa kijiwe cha Bomani mjini Geita, ni miongoni mwa  watu walioathiriwa na tabia ya kulala usingizi wa saa chache hali inayoathiri utendaji kazi wake.

Akizungumza na Mwananchi, anasema awali alikuwa akiamka alfajiri kuwahi wateja wake, lakini ikifika saa moja usiku hutoa pikipiki yake kwa ‘deiwaka’ na yeye kwenda kwenye kumbi za burudani na marafiki zake.

“Niliona kama napumzika na kukaa na marafiki baada ya kazi ngumu ya kuanzia saa 12 alfajiri. Nikiwa klabu tunakunywa na kupiga stori na marafiki hadi saa nane au saa tisa kuna wakati unakuta imefika saa kumi alfajiri bado niko klabu mwanzo ilikuwa kawaida ila baada ya muda hali yangu ilikuwa mbaya”anasema.

Anasema baada ya miezi michache ratiba ya kurudi nyumbani usiku ilianza kumuathiri maana alishindwa kuamka saa 12 alfajiri kama alivyokuwa awali na hata alipotoka saa tatu asubuhi alishindwa kufanya kazi na kusinzia na mwili kuwa mzito.

Kapaya anasema hali ilikua mbaya maana wateja wake walianza kumkwepa, kwani walipomtafuta  asubuhi hakupatikana. Lakini pia alipoteza umakini barabarani, na kuna wakati alihatarisha maisha yake baada ya kugonga gari.

“Nashukuru mke wangu alikaa chini na ndugu zangu walinishauri haikua rahisi kuachana na marafiki, maana niliokuwa nao kazi zao sio kama yangu kidogokidogo nilipunguza na sasa nimeacha pombe kabisa”anasema Kapaya.

Consalatha Peter (25) fundi cherehani  mkazi wa mtaa wa Mission Manispaa ya Geita, anasema: “Nimezoea kutumia muda mwingi kwenye TikTok na kuangalia tamthilia usiku mara nyingi nalala saa saba au saa nane usiku,  sasa hivi mwili unakuwa mzito hata kushona naona mwili hautaki nachoka sana,”

Madhara ya kulala muda mfupi

Daktari bingwa wa usingizi na ganzi salama kutoka Hospitali ya rufaa ya kanda Chato (CZRH) Amani Mollel, anasema hali ya kukosa usingizi wa kutosha hii ni tishio lisiloonekana, ambalo linaathiri afya na ustawi wa wengi bila wao kutambua.

Anasema usingizi wa kutosha ni muhimu kwa kurejesha nishati ya mwili, kuimarisha kinga, kudhibiti homoni, na kusaidia ubongo katika kujifunza na kukumbuka.

Dk Mollel anasema kiafya, watu wazima wanapaswa kupata angalau saa saba hadi tisa  za usingizi kila siku ili kuhakikisha afya njema ya mwili na akili.

Hata hivyo, matumizi ya muda mrefu kwenye burudani za usiku yanasababisha watu wengi kulala kwa muda mfupi, jambo ambalo lina madhara makubwa kwa afya.

Anasema watu wanaolala kwa muda mfupi hupata uchovu wa kudumu mchana, jambo ambalo linaweza kuathiri utendaji wao wa kazi, masomo  na maisha ya kila siku.

Dk Mollel anasema mtu anapochelewa kulala,  hupunguza ubora wa usingizi hasa pale anapokuwa kwenye matumizi ya muda mrefu ya simu, televisheni, au kompyuta.

Matumizi hayo anasema kabla ya kulala huathiri uzalishaji wa homoni ya ‘melatonin’, ambayo husaidia mwili kujiandaa kwa usingizi.

Anasema vifaa hivyo vinatoa mwanga wa buluu ambao hupunguza uwezo wa mwili wa kutambua kuwa ni muda wa kupumzika, hivyo kuchelewesha usingizi na kupunguza ubora wake.

Naye mtaalamu wa dawa za usingizi na ganzi salama kutoka Hospitali ya Katoro, Aloyce Damki anasema matumizi ya simu kabla ya kulala yamekuwa chanzo cha kuathiri usingizi .

“Kwa kawaida giza (usiku) husaidia uzalishaji wa kemikali muhimu kumfanya mtu kulala, kemikali hiyo inaitwa ‘ melatonin’ na huzalishwa kwenye sehemu ya ubongo iitwayo ‘pineal gland’. Kwenye mwanga kemikali hii huzuiwa kuzalishwa, hivyo kumzuia mtu kulala,” anaeleza.

Anasema usingizi mchache  pia hupunguza uwezo wa kufikiri na kuwa na kumbukumbu hafifu, kwani usingizi wa kutosha ni muhimu kwa ajili ya mchakato wa kujifunza na kuhifadhi kumbukumbu.

Anasema ukosefu wa usingizi huathiri uwezo wa ubongo kuchakata na kuhifadhi kumbukumbu mpya, jambo ambalo linaweza kuathiri utendaji kazini, shuleni, na hata katika maisha ya kila siku.

Dk Mollel anasema madhara mengine ya mtu kulala kwa saa chache, ni kuongeza hatari ya kupata shinikizo la damu na magonjwa ya moyo pamoja na aina ya pili ya ugonjwa wa kisukari.

Aidha, mtu anaweza kupata unene kupita kiasi, matatizo ya afya ya akili kama wasiwasi, huzuni, na hatari ya kupata magonjwa ya akili kama ‘skizofrenia’.

Anasema mwili unaponyimwa usingizi wa kutosha, mfumo wa mzunguko wa damu huathirika, hivyo kuongeza hatari ya magonjwa hayo sugu.

Anasema usingizi husaidia kurejesha na kuimarisha mfumo wa kinga za mwili, hivyo kukosa usingizi kunaweza kudhoofisha kinga ya mwili na kuongeza uwezekano wa kupata maambukizi na magonjwa mbalimbali kama mafua ya mara kwa mara.

Madhara mengine yanayotokana na kupata usingizi wa saa chache, ni kumsababishia mtu hasira, huzuni, na wasiwasi na kumuongezea hatari ya kupata msongo wa mawazo na mfadhaiko.

Kwa mujibu wa Dk Mollel,ubongo unahitaji muda wa kutosha wa kupumzika ili kudhibiti mhemko.

Anasema ukosefu wa usingizi hupunguza mwitikio wa mwili, na hivyo kuongeza hatari ya ajali kazini, barabarani, au nyumbani.

Mbali na madhara ya kiafya, kutumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii  usiku, kunaweza kuathiri muda wa kuwa na familia na marafiki na hali  hiyo inaweza kusababisha upweke,  au matatizo ya kiuhusiano.

Kwa mujibu wa utafiti  wa mwaka 2024 uliofanywa na Joel Matiku miongoni mwa wanafunzi 640 wa baadhi ya  vyuo vya maendeleo ya jamii nchini, asilimia kubwa ya wanafunzi hao hulala chini ya saa sita kwa siku  kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii na burudani za usiku.

Kidunia, takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 32.8 ya watu wazima hawapati usingizi wa kutosha, ikimaanisha kuwa takriban thuluthi moja ya watu wazima duniani, wanakosa usingizi wa kutosha hivyo kuathiri afya na ustawi wao kwa ujumla.

Dk Mollel anashauri watu wanaolala kwa saa chache, kupunguza muda wa burudani za usiku na kuweka ratiba thabiti ya kulala.

Pia anashauri kuzima simu na vifaa vya kielektroniki saa moja kabla ya kulala na kwa wale wanaotumia vilevi, wanashauriwa kupunguza pombe za jioni na kuepuka vinywaji vyenye ‘kafeini’.

“Fanya mazoezi ya kupumzisha mwili kama vile yoga au kusoma kitabu kabla ya kulala. Pia  tengeneza mazingira mazuri ya kulala…” anasema.

Anasema ingawa burudani za usiku na matumizi ya mitandao ya kijamii ni sehemu ya maisha ya kisasa,  ni muhimu kuwa na nidhamu katika matumizi yake ili kuhakikisha mhusika ana afya bora.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.