Shinyanga. Mpango wa kunusuru kaya maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) umeendelea kuleta matumaini kwa maelfu ya Watanzania, huku zaidi ya kaya milioni 1.3 zikinufaika na mpango huo.
Hayo yamesemwa jana Aprili 5, 2025 kwenye taarifa iliyotolewa na ofisa habari na mawasiliano wa Tasaf, Christopher Kidanga katika mkutano mkuu wa waandishi wa habari mkoani Shinyanga.
“Kaya hizo zimenufaika kupitia ruzuku za elimu, afya na uanzishaji wa miradi ya uzalishaji mali, hatua iliyosaidia kupunguza kiwango cha umaskini nchini.
“Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha kuwa kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi kimeshuka kutoka asilimia 39 hadi asilimia 36, huku umaskini wa chakula ukipungua kutoka asilimia 9.2 hadi asilimia 8.0,” amesema Kidanga.
Kidanka amesema katika Mkoa wa Shinyanga pekee, jumla ya kaya 33,691 zimenufaika na mpango huo ambapo baadhi ya wanufaika wameweza kujenga nyumba za kisasa kwa kutumia mabati na mbao, huku wengine wakinunua chakula na vifaa vya shule kwa watoto wao.
Pia, amesema zaidi ya Sh23 bilioni zimelipwa kwa wanufaika katika halmashauri tatu za mkoa wa Shinyanga kama ruzuku ya uzalishaji mali,
“Mbali na ruzuku, mpango huo pia unahusisha mikopo kupitia ushirikiano kati ya TASAF na taasisi mbalimbali za kifedha ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na FESLIB, ambapo watu 15,524 tayari wamepatiwa mikopo kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi,” amesema Kidanga.
Mmoja wa wanufaika wa mpango huu, Amina Ramadhani kutoka Kata ya Ndala, amesema kuwa fedha hii imemsaidia, kwani awali alikuwa akipata mlo mmoja na kwa shida.
“Nashukuru sana Serikali kwa kuleta huu mpango. Hii pesa, ukiipanga vizuri katika bajeti, utaona matunda yake. Hata mimi, matunda nayaona, ingawa kidogo. Ninachokipata, pia najishughulisha na biashara ya matunda ili fedha iweze kuwa kwenye mzunguko,” amesema Amina.
Mhitimu wa mpango wa Tasaf kutoka Kata ya Ndala, Pendo Wilson amesema kuwa alikuwa mnufaika wa mpango huo kwa kipindi cha miaka 15 na amehitimu Julai, 2024, akiwa na mafanikio makubwa.
“Kupitia mpango huu wa kunusuru kaya maskini, nimefanikiwa kujenga nyumba ya kisasa, kuvuta maji, na kwa sasa naendelea na mchakato wa kuweka umeme ndani. Hivi sasa tunakula milo mitatu kwa urahisi, na watoto wanapata fursa ya kwenda shule,” alisema Pendo.
Aidha, Kidanga alisema kuwa mafanikio haya yamechangiwa na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, wananchi, na wadau wa maendeleo, na kuahidi kuwa juhudi zaidi zitaelekezwa katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kuinuka kiuchumi.
Mpango wa TASAF ulianzishwa mwaka 2000 kwa lengo la kusaidia wananchi maskini kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Hadi sasa, mpango huu umeendelea kuwa chombo muhimu katika mapambano dhidi ya umaskini nchini.
Crédito: Link de origem