top-news-1350×250-leaderboard-1

Kamishna Dkt. Doliye achambua mafanikio yaliyopatikana katika hifadhi ya NCAA chini ya Rais Samia

Na Hamis Dambaya, Dodoma

Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Dkt. Elirehema Doriye amesema kuwa mamlaka hiyo imefikia malengo ya ongezeko la watalii na ukusanyaji wa mapato kwa miaka minne mfululizo kutokana na mchango mkubwa wa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Tanzania; The Royal Tour.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma siku ya Jumatatu tarehe 10.03.2025 Dkt. Doriye amesema tangu mwaka wa fedha 2021/2022 mpaka kufikia sasa kumekuwa na ongezeko la idadi ya watalii na mapato ambapo kwa mwaka huu wa fedha mpaka kufikia mwezi Februari idadi ya watalii waliotembelea hifadhi hiyo wamefikia 830,295 na kiasi cha fedha kilichokusanywa ni shilingi bilioni 212,023,179,256.68.

“Ni matarajio yetu mpaka tunafunga mwaka huu wa fedha kukusanya shilingi bilioni 230  na mpaka sasa kwenye ukusanyaji wetu wa mapato tumeshakusanya asilimia 92 jambo ambalo kwetu sisi tuliopo kwenye sekta ya utalii tunaona wazi kuwa filamu ya Tanzania: The Royal Tour iliyooongozwa na mheshimiwa Rais Dkt. Samia imeleta mapinduzi makubwa ya kuongezeka kwa watalii,” alisema Dkt. Doriye.

Kamishna huyo wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro amesema kutokana na mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuonesha njia ya namna ya kutangaza utalii mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kubuni njia zaidi za kutangaza vivutio vilivyopo na hivyo kuendelea kuongeza mapato ya serikali.

Kuhusiana na  miundombinu ya utalii ndani ya hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Doriye amesema serikali ya awamu ya sita katika kipindi cha miaka minne imeweza kutoa jumla ya shilingi bilioni 14.993 ambazo zimetumika katika ukarabati wa barabara, miundombinu ya maji na ununuzi wa magari na mitambo ambayo imesaidia kurahisisha huduma  mbalimbali kwa watalii.

“Pamoja na vipaumbele vingi vya serikali ya awamu ya sita, bado tumekuwa tukipata fedha kwa wakati katika kuhakikisha kuwa hakuna huduma ambayo inasimama, kutokana na hali hii tunawaahidi watanzania kuwa tutaendelea kutekeleza kwa ukamilifu majukumu yetu matatu ya kusimamia uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.” Dkt. Doriye aliwaeleza waandishi wa habari katika mkutano huo.

Kuhusiana na uhifadhi na mapambano dhidi ya ujangili, Dkt. Doriye aliwahakikishia watanzania kwamba Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ipo salama kwani imefanikiwa kuondoa vitendo vya ujangili kutokana na kuwa na askari wa kutosha sambamba na kutumia teknolojia ya kisasa katika kusimamia ulinzi wa wanyamapori katika maeneo inayoyasimamia.

Katika mkutano huo Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro alibainisha kuwa serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na kuhama kwa hiyari katika eneo la hifadhi kwenda kijiji cha Msomera na maeneo mengine ili kuboresha maisha ya wananchi ambapo tayari mamlaka imekamilisha ujenzi wa nyumba nyingine 1,508 ambazo  ziko tayari kwa ajili ya wananchi kuhamia na pindi miundombinu mingine ya kijamii ikikamilika zoezi la kuwahamisha wananchi litaendelea.

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imefanikiwa kutekeleza majukumu yake kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan huku ikiendelea kulinda hadhi yake kimataifa ikiwemo kupokea tuzo mbalimbali ambapo mwaka 2023/24 ilifanikiwa kuwa kivutio bora cha Utalii Barani Afrika.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.