top-news-1350×250-leaderboard-1

Kambaya: Vyama vya siasa siyo njia ya pepo, maendeleo yako CCM

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdul Kambaya, amewataka Watanzania kutambua kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana nje ya CCM, huku akisisitiza kuwa vyama vya siasa haviwezi kuwa daraja la mtu kuingia peponi au motoni.

Akizungumza jana, Aprili 11, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Ujenzi, wilayani Liwale, mbele ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, Kambaya amesema:

“Hapa kuna watu wanadhani ukiwa CCM ni kama uko motoni sababu tu uko CCM, na ukiwa chama kingine wanadhani kitakupeleka peponi. Dunia nzima hakuna chama hicho. Peponi na motoni utaenda kwa matendo yako, sisi tunashughulika na changamoto zako.”

Kambaya ameeleza kuwa maendeleo si suala la ahadi wala miujiza bali ni mchakato unaohitaji uongozi wa uzoefu, utulivu na uwezo, akisisitiza kuwa CCM ndicho chama pekee chenye uwezo wa kutatua changamoto za wananchi, hasa wa maeneo ya pembezoni kama Liwale.

“Wasidanganyike. Suala la maendeleo siyo la amri wala kupiga kelele. Ukipata changamoto, angalia chama chenye uwezo wa kukusaidia, na hicho ni CCM. Mnatakiwa kuchagua viongozi wanaojali na wanaojua kazi yao.” alisema.

Kambaya pia ametoa angalizo dhidi ya wanasiasa wanaotumia hoja za vurugu na migawanyiko, akitoa mfano wa fujo zilizowahi kutokea Liwale ambapo nyumba zaidi ya 20 zilichomwa moto.

“Hatuwezi kuwa watu wa vurugu. Tuna njia sahihi ya maendeleo—ni kura, siyo kelele wala chokochoko. Mpigieni kura CCM na Rais Samia ili maendeleo yaendelee.”

Amehitimisha kwa kusema kuwa CCM inatoa majibu, si ahadi za kuwarubuni watu, na kwamba uchaguzi ujao ni fursa kwa wananchi kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwa vitendo kupitia chama hicho.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.