top-news-1350×250-leaderboard-1

Kamati yataka maofisa Ugani, yakumbusha Azimio la Malabo

Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Kilimo imeitaka Serikali kuzingatia matakwa ya utekelezaji wa Azimio la Maputo (2003) na Malabo (2014) ili kuongeza Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwani bado haitoshi.

Maazimio hayo yanazitaka nchi wanachama kutenga asilimia 10 ya bajeti ya Taifa kwa ajili ya sekta ya kilimo lakini wakasema kwa Tanzania malengo hayajatimia bado.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deodatus Mwanyika akiwasilisha maoni ya kamati hiyo bungeni leo Jumatano, Mei 21, 2025 amesema licha ya ukweli kuwa bajeti ya Wizara ya Kilimo imeongezeka, lakini haijafikia malengo yanayotakiwa.

“Kamati inaishauri Serikali kuendelea kuongeza bajeti ya kilimo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa aidha, fedha hizo zitolewe kwa wakati ili kuwezesha kufikia malengo na mikakati iliyokusudiwa,” amesema Mwanyika.

Mwanyika amesema bajeti hiyo ikiongezeka itasaidia hata Serikali kuendelea kuajiri maofisa ugani ambao idadi yao bado ni ndogo ukilinganisha na mahitaji.

Amesema hali hiyo husababisha ofisa ugani mmoja kuhudumia eneo kubwa hivyo kukosekana kwa tija iliyokusudiwa.

“Kamati inaishauri Serikali kuona umuhimu wa kuendelea kutenga bajeti na kuajiri maofisa ugani wa kutosha ili kusogeza huduma kwa wakulima wengi zaidi na kuleta tija katika kilimo kama ilivyokusudiwa,” amesema.

Kuhusu upotevu wa mazao baada kuvunwa amesema bado ni tatizo kwani imebaki kwenye tarakimu mbili (asilimia 35) ikilinganishwa na shabaha ya kupunguza upotevu huo hadi asilimia tano ifikapo mwaka 2030.

Amesema hali hiyo inaweza kuathiri usalama na upatikanaji wa chakula cha uhakika wakati wote nchini, hivyo wakataka Serikali iendelee kuimarisha miundombinu na kukamilisha ujenzi wa maghala ya kutosha katika ngazi za vijiji, kata na wilaya.

Kamati imeitaka Serikali iendelee kushirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha maghala yanajengwa ya kutosha karibu na wananchi katika maeneo yote kulingana na mahitaji.

“Kamati inaishauri Serikali kuchukua hatua za makusudi na kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo hapa nchini na nje ya nchi, unakuwa wa uhakika,” amesema.

Kwa mara nyingine, kamati imeitaka wizara kuwekeza na kuimarisha taasisi za utafiti wa kilimo na kuwaongezea rasilimali watu na rasilimali fedha,  kwa ajili ya utafiti na ilenge kuwajengea uwezo watafiti wa kilimo ili wafanye kazi zao kwa ufanisi na kukuza sekta ya kilimo nchini.

Kwa upande wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wamesema ukusanyaji hafifu wa maduhuli ya mfuko wa maendeleo ya umwagiliaji unaipotezea Serikali mapato, hivyo iweke utaratibu utakaowezesha watumiaji wa maji kuwa na mchango.

Wameishauri Serikali kukamilisha mapitio ya sheria ya ushirika ili kutatua changamoto zinazotokana na usimamizi hafifu na kukosa uwajibikaji katika sekta ya ushirika.

Katika mchango wake, Mbunge wa Mchinga (CCM), Salma Kikwete amezungumzia suala la mbegu za asili ambazo amesema zimeanza kusahaulika.

Salma amesema katika kipindi cha ukoloni, Watanzania walidanganywa baada ya kuonekana mbegu za asili ni za kishenzi wakati haikuwa hivyo.

“Mbegu za asili ni muhimu sana tuendelee kuheshimu na kuzijali mbegu zetu, wakoloni walituaminisha wakatuambia mbegu zetu ni za kishenzi, hii siyo sawa kabisa lazima tujitafakari,” amesema Salma.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mariam Ditopile amesema sekta ya kilimo imeimarika lakini msukumo zaidi uwekwe maeneo ya vijijini.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.