top-news-1350×250-leaderboard-1

Kamati ya Bunge yasistiza ukamilishaji wa mradi wa BRT Awamu ya Tatu kwa wakati

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeitaka Serikali kuhakikisha inamsimamia kikamilifu mkandarasi SINOHYDRO Corporation Ltd, anayejenga Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT3), ili ukamilike kwa wakati na kuanza kutumika kwa wananchi.

Akizungumza leo Machi 17, 2025, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Moshi Kakoso, alisema mradi huo unaoanzia katikati ya jiji la Dar es Salaam hadi Gongolamboto (km 23.3) ukikamilika utapunguza msongamano wa magari na kuchochea shughuli za kiuchumi.

“Serikali imewekeza fedha nyingi katika miradi ya BRT, hivyo ni lazima tija ionekane kwa kupunguza msongamano wa barabara na kuwawezesha wananchi kufika kazini na kwenye biashara zao kwa wakati. Tumejiridhisha na kasi ya ujenzi, lakini muda uliopangwa umesalia miezi minne tu. Tunahimiza mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati,” alisema Kakoso.

Aidha, aliishauri Serikali kuangalia upya usanifu wa barabara hizo ili kuhakikisha zinakuwa rafiki kwa watumiaji, hasa katika matukio ya dharura.

“Tunashauri wataalamu kuzingatia miundombinu wezeshi, hasa kupunguza kingo ambazo hazina ulazima ili kurahisisha matumizi ya barabara hizi kwa wananchi,” aliongeza Kakoso.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alisema mradi wa BRT Awamu ya Tatu umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2025.

“Namwagiza mkandarasi kuongeza idadi ya mafundi na vibarua ili mradi huu ukamilike kwa wakati. Pia, tunawaonya wafanyabiashara waliovamia maeneo ya ujenzi wa barabara hizi waache mara moja, kwani wanachelewesha kazi na kuhatarisha maisha yao,” alisema Kasekenya.

Alifafanua kuwa ujenzi wa barabara za BRT umekumbwa na changamoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao pembezoni mwa barabara, jambo ambalo limechangia ucheleweshaji wa mradi.

Meneja wa Mradi wa BRT3, Mhandisi Frank Mbilinyi, alisema Serikali kwa kushirikiana na mamlaka za mitaa inaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waache kuvamia maeneo ya ujenzi wa barabara.

Serikali inaendelea na mpango wa kuboresha miundombinu ya barabara jijini Dar es Salaam kwa awamu mbalimbali:

Awamu ya Kwanza: Kivukoni – Kimara – Magomeni – Morocco (km 20.9) – Imekamilika
Awamu ya Pili: Magomeni – Mbagala – Imekamilika
Awamu ya Tatu: Posta – Gongolamboto (km 23.3) – Ujenzi unaendelea
Awamu ya Nne: Katiki ya Jiji – Tegeta (km 29.13) – Ujenzi unaendelea

Mradi huu wa mabasi yaendayo haraka unalenga kuimarisha usafiri wa umma, kupunguza msongamano wa magari, na kurahisisha safari kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.