Dodoma. Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetangaza nafasi za kuandikishwa jeshini kwa vijana wa Kitanzania wenye elimu ya sekondari hadi elimu ya juu.
Nafasi hizo zimetangazwa leo Jumatano Aprili 30,2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Kanali Gaudentius Ilonda alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya jeshi hilo jijini Dodoma.
Amezitaja nafasi hizo ni kwa vijana wataalamu wa tiba ikiwemo madaktari waliobobea (specialist) katika fani za daktari wa upasuaji, daktari wa upasuaji wa mifupa na viungo, wa magonjwa ya kibofu na njia ya mkojo, mtaalamu wa kusoma picha za magonjwa kama za X-ray, MRI, CT, wa masikio, pua na koo, daktari wa usingizi, wa magonjwa ya ndani, wa macho, wa saratani.
Wengine ni madaktari wa uchunguzi wa sampuli za mwili kwa ajili ya upimaji wa magonjwa, wa magonjwa ya akili, wa huduma za dharura, wa magonjwa ya damu, wa tiba za wanyama, mhandisi wa tiba na vifaatiba, taalamu wa maabara ya meno na daktari wa afya za abiria na wahudumu wa anga.
Pia Kanali Ilonda ametaja wengine wanaohitajika ni mafundi mchundo wa aluminium welding, welding na metal fabrication.
Amezitaja sifa za waombaji kuwa ni pamoja na awe Mtanzania mwenye kitambulisho cha Taifa, awe na afya nzuri na akili timamu na hajapatikana na hatia yoyote ya makosa ya jinai mahakamani na kufungwa.
“Awe na cheti halisi cha kuzaliwa, vyeti vya shule na vyeti vya taaluma. Awe hajatumikia Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo au Kikosi cha Kuzuia Magendo,”amesema.
Kanali Ilonda ametaja sifa nyingine kuwa awe amehitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) au kwa mujibu wa Sheria na kutunukiwa cheti.
Pia amesema kwa vijana wenye elimu ya kidato cha nne na kidato cha sita wawe na umri usiozidi miaka 24, wenye elimu ya stashahada ni umri usiozidi miaka 26. Kwa vijana wenye elimu ya juu umri usizidi miaka 27 na madaktari bingwa wa binadamu umri usizidi miaka 35 ya kuzaliwa.
Kanali Ilonda ametaja taratibu za kutuma maombi kuwa yote yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe makao makuu ya jeshi hilo jijini Dodoma kuanzia Mei Mosi hadi Mei 14,2025.
“Maombi hayo yawasilishwe yakiwa na nakala ya kitambulisho cha Taifa au nambari ya Nida, nakala ya cheti cha kuzaliwa, shule na vyuo pamoja na nakala ya cheti cha JKT kwa waombaji waliomaliza mkataba wa kujitolea na nambari ya simu ya mkononi ya mwombaji,”amesema.
Crédito: Link de origem