Dar es Salaam. Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa mwaka wa fedha 2025/26, yenye thamani ya Sh6.9 trilioni, itatumika katika sekta mbalimbali ikiwemo maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge, wawakilishi, na madiwani unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025.
Maeneo yaliyopewa kipaumbele katika bajeti hiyo ni utekelezaji wa maendeleo yenye dhima ya Serikali inayoendelea na miradi inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo, miradi ya kimkakati inayoendelea na mipya itakayotekelezwa mwaka wa fedha 2025/2026,katika sekta za miundombinu, utalii, uchumi wa buluu na huduma za jamii.
Hayo yamebainisha leo Alhamisi Juni 12,2025 na Waziri Nchi, Ofisi Rais (Fedha na Mipango), Dk Saada Salum Mkuya wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya SMZ kwa mwaka wa fedha 2025/26 akiliomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha Sh6.9 trilioni.
Dk Mkuya amesema maeneo mengine ambayo bajeti hiyo imepanga kuyatumia ni kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kuwezesha ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa wizara na taasisi (ikiwemo vitendea kazi).
“Kusimamia hali ya amani, usalama na utulivu nchini kwa muda wote na mahitaji ya uendeshaji wa shughuli mtambuka ikiwemo kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalumu na huduma za wazee,” amesema Dk Mkuya.
Kwa mujibu wa Dk Mkuya, Sh6.9 trilioni ni ongezeko la Sh1.7 trilioni sawa na asilimia 34.7 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2024/25 ya Sh5.1 trilioni ambapo zitakwenda kutumika kuhakikisha masilahi ya lazima kwa watumishi wa umma na mahitaji ya matumizi ya Mfuko Mkuu wa Serikali.
Crédito: Link de origem